Chris Brown, Diamond kimewaka
Muktasari:
- Hilo ndilo linaloonekana sasa kwa staa wa R&B Marekani, Chris Brown ‘Breezy’ na Diamond Brown, mama wa mtoto wake wa tatu, Lovely Symphani Brown.
KAMA kuna kitu kinachoweza kusababisha tofauti kubwa kwa wazazi basi ni suala la mtoto ni moja ya mzozo ambao husababisha chuki kubwa kwao.
Hilo ndilo linaloonekana sasa kwa staa wa R&B Marekani, Chris Brown ‘Breezy’ na Diamond Brown, mama wa mtoto wake wa tatu, Lovely Symphani Brown.
Wawili hao wameingia kwenye mvutano wa wazi, kila mmoja akitoa upande wake kuhusu malezi, matunzo na nafasi ya Chris katika maisha ya binti yao.
Sakata hilo limekuwa gumzo baada ya Diamond kufunguka kuhusu kile anachodai kuwa amekuwa akikabiliana nacho katika maisha yake binafsi, huku Chris akijibu kwa upande wake na kuweka wazi kuwa hataki kuzuiwa kuwa karibu na mtoto wake.
DIAMOND: BREEZY ANATISHIA WATU WANGU WA KARIBU
Diamond ameibua madai mazito dhidi ya Chris, akisema mwanamuziki huyo amekuwa akimtishia mpenzi wake wa sasa pamoja na kaka yake pacha.
Kwa mujibu wa Diamond, hali hiyo imeathiri mahusiano yake na hata kumfanya awe na hofu ya kuingia kwenye uhusiano mwingine.
“Chris amekuwa akimtishia mpenzi wangu wa sasa pamoja na kaka yangu pacha, vitendo hivyo vimesababisha mahusiano yangu kuvunjika na kunifanya niishi kwa hofu kubwa ya kuanzisha penzi jipya,” amesema Diamond
Lakini, malalamiko ya Diamond hayakuishia hapo, pia amedai kuwa Chris hatoi fedha za kutosha kwa ajili ya matunzo ya Lovely, jambo ambalo limeongeza uzito kwenye mvutano wao.
BREEZY: LOVELY NAMGHARAMIA MIMI
Chris Brown hajakaa kimya kwenye tuhuma hizo kwani alidai kuwa Diamond ndiye anayemzuia kuwa karibu na Lovely.
Breezy aliqndika kwenye ukurasa wake wa Instagram kuwa amekuwa anakosa nafasi ya kumuona binti yake kwa miezi kadhaa, huku akisisitiza kuwa amekuwa akigharamia mahitaji ya mtoto huyo.
“Mama wengine wa watoto wangu wote wananipa nafasi mimi kama baba kushiriki kikamilifu kwenye maisha ya watoto wangu, lakini Diamond amekuwa akiniwekea ugumu na kuninyima fursa ya kumwona binti yangu Lovely kwa miezi sasa, wakati mimi ndiye ninayegharamia kila kitu kuhusu maisha yake. Hii si haki hata kidogo," amesema Chris Brown.
Hapo ndipo mzozo wa sakata hili ulipoanza kuwaka zaidi, kwani kila upande unaonekana kuwa na simulizi yake kuhusu nani anapaswa kulaumiwa.
MA-EX WA BREEZY WAKO UPANDE WAKE
Baadhi ya wanawake ambao Chris amewahi kupata nao watoto, akiwemo Ammika Harris na Nia Guzman, wameonekana kumuunga mkono. Jada Wallace, anayetajwa kuwa mpenzi wake wa sasa, pia ameingia kwenye mjadala huo.
Kwa upande wao, wanamtetea Breezy wakisisitiza kuwa amekuwa akijitahidi kuwa baba anayeshiriki katika maisha ya watoto wake.
SHERIA YA MAREKANI HAITAZAMI JINA LA MTU
Kwa mujibu wa sheria za Marekani, mzazi anayeshindwa kutekeleza majukumu kwa mtoto anaweza kuchukuliwa hatua kali za sheria, bila kujali umaarufu au nafasi yake katika jamii.
Hatua hizo zinaweza kujumuisha kulipa faini ya Dola 5,000, kukatwa mshahara, kuzuiwa baadhi ya mali au kufungwa jela miezi sita.
Sheria hiyo inalenga kuhakikisha mahitaji ya mtoto hayapuuzwi pale mzazi anaposhindwa kutekeleza wajibu uliowekwa.
SAFARI YA MAFANIKIO YA BROWN
Chris Brown, amekuwa akijijengea jina kubwa katika tasnia ya muziki duniani, akiwa ameuza zaidi ya nakala milioni 140 za kazi zake za muziki. Mafanikio hayo yamemfanya kuwa miongoni mwa wasanii wanaouza zaidi katika historia ya muziki duniani.
Brown pia amejenga kundi kubwa la mashabiki waaminifu, huku akitajwa miongoni mwa wasanii wenye asili ya Afrika waliowahi kupata mapato makubwa kupitia ziara za muziki duniani.
Mbali na uimbaji, uwezo wake wa kucheza umekuwa ukilinganishwa mara kwa mara na ule wa mwanamuzikiwa zamani marehemu Michael Jackson, hasa kutokana na umahiri wake katika uchezaji.
Mwaka 2019, jarida la Billboard lilimtaja Brown kuwa msanii wa tatu aliyefanya vizuri zaidi katika muziki wa R&B na hip-hop katika muongo wa miaka ya 2010, akitanguliwa na Drake na Rihanna.
Katika kipindi cha kazi yake, Brown ameshinda tuzo 219 kati ya uteuzi 566, hatua inayoonyesha kiwango cha mafanikio aliyopata katika tasnia ya burudani.
Mbali na muziki, Brown amejikita pia katika uigizaji. Alianza kuonekana katika filamu mwaka 2007 kupitia filamu Stomp the Yard, huku pia akishiriki kama mgeni katika kipindi cha televisheni The O.C.
Baadhi ya filamu nyingine alizoshiriki ni This Christmas (2007), Takers (2010), Think Like a Man (2012) na Battle of the Year (2013).