Diamond kapuuza njia ya Harmonize na Rayvanny?
Muktasari:
- Diamond aliyetoka na ngoma yake 'Kamwambie' (2009), alikuja na EP kama sehemu ya utangulizi wa albamu yake ya nne akiwa ameiga utararibu huo kutoka kwa Harmonize na Rayvanny.
STAA wa Bongo Fleva kutoka WCB Wasafi, Diamond Platnumz hadi sasa ameachia Extended Playlist (EP) moja tu, 'First of All' (2022) ikiwa na nyimbo 10 ambazo kwa jumla zina urefu wa dakika 33.
Diamond aliyetoka na ngoma yake 'Kamwambie' (2009), alikuja na EP kama sehemu ya utangulizi wa albamu yake ya nne akiwa ameiga utararibu huo kutoka kwa Harmonize na Rayvanny.
First of All (2022) au FOA kama wengi wanavyoiita ni EP iliyochanganya ladha mbalimbali za muziki wa Afrika kama Bongo Fleva, Afrobeats, Soukous, Amapiano na Zouk. EP hiyo hiyo iliwashirikisha Focalistic, Pabi Cooper, Mbosso, Jaywillz, Adekunle Gold na Zuchu ambaye ni mkewe kwa sasa.
Kabla ya kuachiwa EP hiyo, Diamond alisema albamu yake mpya ipo mbioni kutoka na itakuwa na nyimbo 12 ingawa atalazimika kuachia EP kwanza kutokana ana nyimbo zaidi ya 50 ambazo zipo tayari. Utakumbuka hadi sasa Diamond ameachia albamu tatu ambazo ni Kamwambie (2010), Lala Salama (2012), na A Boy From Tandale (2018) iliyosimamiwa na Universal Music Group (UMG).
Mara nyingi albamu hujumuisha nyimbo kuanzia nane na kuendelea ambazo kwa jumla zinakuwa na dakika 30 hadi 80, huku EP ikiwa na nyimbo kuanzia nne hadi nane ambazo kwa jumla huwa dakika takribani 10 hadi 30.
Katika historia ya WCB Wasafi, Harmonize ndiye msanii wa kwanza kuachia EP na Februari 2019 aliachia EP yake 'Afro Bongo' yenye nyimbo nne akiwashirikisha wasanii kama Yemi Alade, Mr. Eazi na Burna Boy, wote kutoka Nigeria. Mara baada ya kuachana na WCB Wasafi, Harmonize aliachia albamu yake ya kwanza, Afro East (2022) ambayo ilizinduliwa na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete katika ukumbi wa Mlimani City.
Albamu ya Afro East ambayo ina nyimbo 18, Harmonize aliwashirikisha wasanii kama Burna Boy, Mr. Blue, Lady Jaydee, Morgan Heritage, Phyno, Skales, Yemi Alade, Mr. Eazi, Falz na Khaligraph Jones.
Baada ya Harmonize akafuata Rayvanny ambaye Februari 14, 2020, Siku ya Wapendanao (Valentine’s Day) aliachia EP yake ya kwanza 'Flowers' yenye nyimbo nane alizowashirikisha wasanii kama Mr Blue, Malkia Karen na Messia Marcoa.
EP hiyo ilifanya vizuri ambapo ndani ya kipindi cha mwezi mmoja ilipata 'views' zaidi ya milioni 20 kwenye mtandao wa YouTube pekee, huku ikija kushika nafasi ya pili kwa kupata 'streams' nyingi zaidi kwa mwaka 2020 ndani ya mtandao wa Boomplay Music.
Mwaka mmoja baadaye, yaani Februari 1, 2021 l, ndipo Rayvanny akaachia albamu yake ya kwanza tangu aanze muziki aliyoipa jina la Sound From Africa ikiwa na nyimbo 23 alizowashirikisha wasanii 20 kutokea Tanzania na nchi nyingine za Afrika.
Kwa muktadha huo, utoana Harmonize na Rayvanny walianza kutoa EP kisha ndipo albamu zao zikafuata.
Huu ni utaratibu ambao umekuwa ukitumiwa na wasanii wengi duniani kama sehemu ya kutangaza ujio wa albamu zao ambazo zipo mbioni kutoka. Ndicho Diamond alimaanisha pale alipotoa EP yake, First of All (2022) lakini miaka inazidi kukatika bila kutoa albamu, kitu ambacho pia alikuwa ameahidi kufanya hivyo. Mnamo Julai, Diamond akiongea na Jarida la Billboard huko Marekani, alisema sababu zinazomfanya kuchukua muda mrefu bila kutoa albamu, ni tabia ya mashabiki kutozipa uzito sawa nyimbo zote zilizopo katika albamu.
"Siwezi kuweka nyimbo mbovu kwenye albamu yangu, lakini unapotoa albamu mara nyingine, inaua baadhi ya nyimbo kwa sababu watu wanataka wimbo mmoja tu ndio upewe kipaumbele," alisema Diamond na kuongeza:
"Halafu nyimbo nyingine zinaonekana kama hazina maana, jambo ambalo nalichukia sana. Nadhani hiyo pia ni sababu iliyofanya nichukue muda kumaliza kazi hii."
Ikumbukwe albamu zake mbili za mwanzo zote zilikuwa za Bongo Fleva ila ile ya tatu (A Boy From Tandale), ililenga soko la kimataifa na ndio sababu ya kushirikisha wasanii wengi wa huko. Ilifanya vizuri licha ya kujumuisha nyimbo nyingi zilizotoka miaka mingi nyuma kama Number One Remix (2014) ft. Davido, Nana (2015) ft. Mr. Flavour na Kadogo (2016) ft. P Square.
Hata hivyo, ukweli utabaki kuwa ni albamu iliyosheheni majina makubwa kama Ne-Yo, Tiwa Savage, Vanessa Mdee, Rick Ross, Jah Prayzah, Rayvanny, Omarion, Young Killer na Morgan Herritage, kundi la muziki wa reggae kutokea Jamaica.