Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sugu: Hizi ndo sababu Chameleone kukiwasha Honors

Muktasari:

  • Maswali hayo yameongezeka baada ya Chameleone kuwasili nchini Julai 27, 2026, akiwa ameambatana na mama yake mzazi pamoja na bendi yake nzima kwa ajili ya tamasha hilo litakalofanyika Julai 31, 2026, katika Ukumbi wa SuperDome, Masaki, Dar es Salaam.

UAMUZI wa kumuingiza mwanamuziki mkongwe wa Uganda, Jose Chameleone, katika orodha ya wasanii watakaotumbuiza kwenye tamasha la Bongo Fleva Honors Season 4 umeibua mjadala miongoni mwa wadau na mashabiki wa muziki, wengi wakijiuliza kwa nini msanii wa nje apewe nafasi katika jukwaa ambalo tangu kuanzishwa kwake limejulikana kwa kuenzi waanzilishi wa Bongo Fleva nchini Tanzania.

Maswali hayo yameongezeka baada ya Chameleone kuwasili nchini Julai 27, 2026, akiwa ameambatana na mama yake mzazi pamoja na bendi yake nzima kwa ajili ya tamasha hilo litakalofanyika Julai 31, 2026, katika Ukumbi wa SuperDome, Masaki, Dar es Salaam.

Hata hivyo, mwanzilishi wa tamasha hilo, mwanamuziki na Mbunge wa zamani, Joseph Mbilinyi 'Sugu', amesema uamuzi wa kumwalika Chameleone haukutokana na umaarufu wake pekee, bali na mchango mkubwa alioutoa katika ukuaji wa muziki wa Bongo Fleva ndani na nje ya Tanzania.


SUGU AFAFANUA

Akizungumza kuhusu ushiriki wa Chameleone, Sugu amesema msanii huyo ni miongoni mwa wanamuziki wa Afrika Mashariki walioupa heshima muziki wa Tanzania kwa miaka mingi.

"Mchango wa Jose Chameleone katika muziki wa Bongo Fleva ni mkubwa sana. Ni mmoja wa wasanii wa nje walioweza kufanya ziara nyingi za muziki katika mikoa mbalimbali ya Tanzania kuliko hata baadhi ya wasanii wa hapa nyumbani. Amechangia kwa kiasi kikubwa kuukuza muziki wa Afrika Mashariki, ndiyo maana tumeona anastahili kuwa sehemu ya Bongo Fleva Honors."

Aliongeza kuwa Chameleone ameandika historia kwa kuwa msanii wa kwanza kutoka nje ya Tanzania kushiriki tamasha hilo, akisisitiza kuwa hatua hiyo haibadilishi dhima ya tamasha, bali inaonyesha namna muziki wa Bongo Fleva ulivyovuka mipaka na kushirikiana na wasanii wa ukanda wa Afrika Mashariki.

"Huyu ndiye msanii wa kwanza wa kimataifa kushiriki Bongo Fleva Honors, lakini naamini hatakuwa wa mwisho."


BONGO FLEVA HONORS ILIANZAJE?

Bongo Fleva Honors ni jukwaa maalumu lililoanzishwa na Sugu kupitia kampuni ya Deiwaka World kwa lengo la kuwatambua, kuwaheshimu na kuwashukuru wasanii walioanzisha na kuijenga Bongo Fleva hadi kufikia hadhi iliyonayo leo.

Tofauti na tuzo nyingi zinazotolewa kwa mafanikio ya mwaka husika, Bongo Fleva Honors hulenga kuenzi historia ya muziki huo kwa kuwapa heshima wasanii walioweka msingi wake, huku wakipata nafasi ya kutumbuiza mbele ya mashabiki wao.

Tangu kuanzishwa kwake, tamasha hilo limeendelea kukua na kuwa moja ya matukio makubwa yanayowakutanisha wakongwe wa muziki wa Tanzania pamoja na kizazi kipya.


SAFARI YA MISIMU MINNE

Msimu wa kwanza wa Bongo Fleva Honors ulifanyika mwaka 2023 na ulianza kwa kuwaenzi baadhi ya magwiji walioweka msingi wa muziki wa Bongo Fleva.

Mwaka 2024, msimu wa pili uliendelea kuwapa heshima wasanii wengine waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya muziki huo.

Mwaka 2025, msimu wa tatu ulimheshimu mkongwe wa Hip Hop, Afande Sele, ambaye alitoa onyesho lililowakumbusha mashabiki enzi za nyimbo zake zilizotikisa Tanzania.

Safari hiyo sasa imefikia msimu wa nne mwaka 2026, ambao umeandika historia kwa kumleta Jose Chameleone kutoka Uganda kuwa msanii wa kwanza wa Afrika Mashariki, nje ya Tanzania, kushiriki jukwaa hilo.


AHADI KWA MASHABIKI

Baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Chameleone amesema anafurahia mwaliko huo na amejiandaa kutoa burudani ya kiwango cha juu.

"Ninafurahi kuwa Tanzania tena. Nawashukuru waandaaji kwa kunipa heshima hii. Watu wengi wamekuwa wakinisikiliza kwa miaka mingi, lakini sasa wataniona jukwaani nikiwa na bendi yangu kamili. Ninaamini itakuwa shoo ambayo mashabiki wataikumbuka kwa muda mrefu."

Msanii huyo amesema Tanzania ni moja ya nchi zilizochangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya muziki wake. Ndiyo maana aliona ni muhimu kuja akiwa na bendi yake yote ili kuwapa mashabiki burudani ya kiwango cha kimataifa.


MCHANGO WA CHAMELEONE BONGO

Kwa zaidi ya miaka 20, Jose Chameleone amekuwa mmoja wa wanamuziki wa Afrika Mashariki waliokuwa na uhusiano wa karibu na tasnia ya muziki ya Tanzania. Mbali na kufanya maonyesho mengi katika mikoa mbalimbali ya nchi, msanii huyo amewahi kushirikiana na wasanii kadhaa wa Tanzania, hatua iliyochangia kuimarisha uhusiano wa kimuziki kati ya Tanzania na Uganda.

Katika kipindi cha ukuaji wa Bongo Fleva mwanzoni mwa miaka ya 2000, Chameleone alikuwa miongoni mwa wasanii wa kwanza wa Afrika Mashariki waliokuwa wakishiriki mara kwa mara katika matamasha makubwa nchini Tanzania, akipanda jukwaa pamoja na majina makubwa kama Profesa Jay, AY, Mr Blue, TID, MwanaFA, Q Chief na wengine waliokuwa wakitawala soko la muziki wakati huo.

Kupitia nyimbo zake za Kiswahili na maonyesho yake ya moja kwa moja, Chameleone alijijengea mashabiki wengi nchini Tanzania kiasi cha kuifanya nchi hiyo kuwa moja ya masoko yake makubwa nje ya Uganda. Umaarufu wake ulisaidia pia kuimarisha ushirikiano wa kimuziki kati ya wasanii wa Tanzania na Uganda, huku ukifungua milango kwa kizazi kilichofuata kufanya kazi kwa pamoja bila mipaka.

Ni historia hiyo ambayo waandaaji wa Bongo Fleva Honors wanaamini inampa Chameleone sifa za kuwa sehemu ya tamasha hilo, wakisisitiza kuwa lengo lake si kuenzi wasanii wa Tanzania pekee, bali pia watu wote waliotoa mchango mkubwa katika safari ya ukuaji na mafanikio ya muziki wa Bongo Fleva ndani na nje ya mipaka ya nchi.

USIKU WA HISTORIA

Mbali na Chameleone, tamasha la mwaka huu linatarajiwa kuwakutanisha mashabiki wa muziki wa vizazi tofauti katika usiku mmoja wa kuenzi historia ya Bongo Fleva.

Kwa mujibu wa waandaaji, lengo si kutoa burudani pekee, bali pia kuwakumbusha Watanzania mchango wa wasanii waliofungua njia kwa kizazi cha sasa.

Kwa ujio wa Chameleone na maelezo ya Sugu kuhusu sababu za kumchagua, mjadala uliokuwepo sasa umepata majibu. Badala ya kuwa tamasha la Tanzania pekee, Bongo Fleva Honors limeonyesha kuwa linatambua mchango wa kila msanii aliyeisaidia Bongo Fleva kuvuka mipaka na kuwa sauti ya Afrika Mashariki.