Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

FUNGA MWAKA: Mastaa waliosepa katika lebo zao 2025

LEBO Pict

Muktasari:

  • Baadhi ya wasanii hao wa Bongofleva waliteka mazungumzo hasa mtandaoni kwa jinsi walivyotaka kuachana na lebo hizo kuanzia mwanzoni mwa 2025 kama ifuatavyo.

PENGINE huu ndio mwaka tulioshuhudia wasanii wengi wenye majina makubwa wakiachana na rekodi lebo zao ambazo ziliwatambulisha katika soko la muziki kwa mara ya kwanza au kukuza chapa zao.

Baadhi ya wasanii hao wa Bongofleva waliteka mazungumzo hasa mtandaoni kwa jinsi walivyotaka kuachana na lebo hizo kuanzia mwanzoni mwa 2025 kama ifuatavyo.

LEB 01

1. Ibraah - Konde Music Worldwide

Baada ya uvutano wa muda mrefu, hatimaye Ibraah na lebo yake ya zamani, Konde Music Worlwide walifikia makubaliano ya kuachana rasmi mbele ya Baraza la Sanaa Taifa (Basata) mwezi Mei.

Lebo hiyo inayomilikiwa na Harmonize, katika kikao chake na Basata iliwakilishwa na meneja wake Sandra, huku Ibraah akifuatana na mshauri wake wa biashara, Msigwa.

Kupitia makubaliano hayo, Ibraah aliruhusiwa kuendelea na kazi zake za muziki bila masharti yoyote kutoka kwa lebo hiyo, hatua inayotoa nafasi kwa msanii huyo kujiendeleza zaidi kisanaa kwa uhuru na ubunifu.

Akiwa Konde Music, Ibraah alitoa EP tatu, Steps (2020), Karata 3 (2021), Air Piano (2024) pamoja na albamu moja, The King of New School (2022) yenye nyimbo 17 ambazo hakushirikisha msanii yeyote wa lebo hiyo.

Na hadi anaondoka Konde Music, Ibraah alikuwa ameshirikiana na Harmonize katika nyimbo tano ambazo ni One Night Stand (2020), Addiction (2021), Mdomo (2022), Tunapendeza (2023) na Dharura (2024).

LEB 02

2. Mbosso - WCB Wasafi

Mwishoni mwa Januari ndipo zilianza tetesi kuwa Mbosso ameomba kuondoka WCB Wasafi, lebo aliyojiunga nayo mwaka 2017 baada ya kusambaratika kwa kundi la Yamoto Band.

Kwa sasa akiwa msanii huru, Mbosso anaendesha lebo yake, Khan Music, ambapo anasimamia mwelekeo wake wa kisanii ili kuleta ushawishi na mabadiliko makubwa katika muziki kwa njia ya ubunifu.

Khan Music ndio imesimamia EP yake ya pili, Room Number 3 (2025) ambayo imekuja na nyimbo kali kama Pawa, Aviola, Nusa Saa, Merijaah n.k.

Akiwa na WCB Wasafi, Mbosso alitoa albamu moja, Definition of Love (2021), na EP moja, Khan (2022) ambayo kufanya kwake vizuri kulipelekea kushinda tuzo ya TMA 2022 kama Msanii Bora wa Kiume.

Na alipokuwa Yamoto Band alifanya vizuri na nyimbo zao kali hadi kushinda tuzo ya TMA 2015 kama Kundi Bora la Mwaka Bongofleva wakiwabwaga Weusi, B.O.B, Navy Kenzo na Makomando.

LEB 03

3. Yammi - The African Princess

Usiku wa Mei 5, katika taarifa yake umma lebo ya The Africa Princess yake Nandy ilitangaza usitishwaji wa mkataba na msanii wake Yammi kwa kile kilichotajwa kama makubaliano ya pande zote mbili.

Yammi alitambulishwa na The African Princess hapo Januari 2023 na kutoa EP yake ‘Three Hearts’ iliyofanya vizuri hadi kuchaguliwa kuwania Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Msanii Bora Chipukizi.

“Tunaamini lebo imetoa mazingira bora yaliyomwezesha kukua kisanaa, na tunafurahi kuona amepata wawekezaji waliovutiwa kuendeleza na kusimamia kipaji chake ili kufikia hatua kubwa zaidi kimataifa.”

“Kuondoka kwake pia kunatoa nafasi kwa The African Princess kuendelea na dhamira yake ya kuwainua wasanii wapya, kuwekeza kwao, na kuendelea kuchangia katika maendeleo ya muziki wa Tanzania na Afrika,” taarifa ilieleza.

Yammi aliyevuma na nyimbo zake kama Tiririka (2023), Nitadumu Naye (2024) na Kukupenda (2024), baada ya kuondoka katika lebo hiyo akaja na EP yake, After All (2025) yenye nyimbo sita huku akimshirikisha Mdogo Sajenti.

LEB 04

4. Platform - Abbah Music

Mnamo Juni, Platform alitangaza kuachana na lebo ya Abbah Music akisema kuwa uamuzi huo umefikiwa kwa maelewano ya amani na kwa nia ya kuendeleza malengo mapya ya kisanaa na ukuaji wa kazi zake.

Abbah Music ni lebo yake mtayarishaji Abbah, na imehusika kuibua vipaji kadhaa vikali akiwamo Hanstone ambaye alifanya vizuri katika wimbo wa Maua Sama, Iokote (2018).

“Ninabaki na heshima kubwa kwa timu nzima ya Abbah Music kwa moyo wa kujituma waliouonesha katika kila hatua. Ushirikiano wetu umekuwa wa thamani kubwa, na naamini mafanikio yaliyopatikana yatabaki kuwa kumbukumbu muhimu katika historia yangu ya muziki.

“Nawatakia kila la heri katika mipango yenu ya sasa na ya baadaye. Shukrani nyingi kwa ushirikiano wenu, na kwa mashabiki wangu, asanteni kwa sapoti yenu,” sehemu taarifa ya Platform ilieleza.

Chini ya Abbah Music, Platform amefanya vizuri na nyimbo zake kama Ananipenda (2023) na Wivu (2023) ambazo zote video zake zimetazamwa zaidi ya mara milioni 10 katika mtandao wa YouTube.

LEB 05

5. Lava Lava - WCB Wasafi

Baada ya miaka takribani saba ya kufanya kazi pamoja, Lava Lava aliamua kuachana na WCB Wasafi na kwenda kuanzisha lebo yake, Bite Gang ambayo ndio inasimamia kazi zake kwa wakati huu.

Taarifa za kuondoka kwake kwa mara ya kwanza zilitolewa mwezi Mei na Baba Levo ambaye ana ukaribu mkubwa na Diamond, mwanzilishi na mmiliki wa WCB Wasafi.

“Safari njema, mdogo wangu (Lava Lava) una kipaji kikubwa sana. Watanzania watakuwa mashahidi wa namna ambavyo Diamond alipigania kipaji chako hadi kikabadilika kuwa fedha.

“Alifanya kila namna, ikiwamo kushirikiana na wewe kwenye nyimbo nyingi sana. Sasa umekua, na ni vyema kujitegemea ili kuwapa nafasi wadogo zako wengine,” alieleza Baba Levo.

Utakumbuka Lava Lava alitambulishwa na WCB Wasafi hapo Mei 2017 akiwa ni msanii wa tano baada ya Harmonize (2015), Rayvanny (2016), Rich Mavoko (2016) na Queen Darleen (2016).