Kauli 3 za Ruby zafichua safari yake
Muktasari:
- Huu siyo ukimya wa kawaida wa msanii anayepumzika muziki, bali sehemu ya safari ambayo amekuwa akiifafanua hatua kwa hatua tangu aanze kuzungumza wazi kuhusu wokovu na mwelekeo mpya wa maisha yake.
LEO Mwanaspoti inamwaangazia Hellen George maarufu kama Ruby, msanii ambaye ukimya wake kwenye Bongofleva kwa muda sasa unaonekana kuwa na jibu lake.
Huu siyo ukimya wa kawaida wa msanii anayepumzika muziki, bali sehemu ya safari ambayo amekuwa akiifafanua hatua kwa hatua tangu aanze kuzungumza wazi kuhusu wokovu na mwelekeo mpya wa maisha yake.
Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Ruby ametoa kauli ambazo zikifuatiliwa kwa mpangilio zinaonyesha namna mtazamo wake ulivyokuwa ukibadilika. Agosti 2025 alizungumza kuhusu kutaka kuitwa ‘mtumishi’, Januari 2026 akaeleza namna wokovu ulivyombadilisha, huku Septemba 2026 akisisitiza kwamba hayupo duniani kuwafurahisha watu.
Hizo ndizo kauli tatu zinazofuatilia safari hiyo, kuanzia alipoanza kuzungumza na Mwanaspoti kuhusu wokovu, hatua aliyofikia baadaye hadi msimamo aliouweka sasa.
AGOSTI 2025: “NATAKA KUITWA MTUMISHI”
Agosti 2025, Ruby alizungumza na Mwanaspoti kuhusu hatua yake ya wokovu na namna alivyokuwa akiitazama safari yake mpya.
Katika mazungumzo hayo alisema angependa zaidi kuitwa mtumishi akitofautisha maisha ya msanii anayelenga kuwafurahisha watu na yale ya mtu anayechagua kufanya kile anachoamini Mungu anataka.
Wakati huo, Ruby hakuwa akisema moja kwa moja kwamba amefunga milango ya Bongo Fleva. Badala yake, alieleza kuwa muziki bado ulikuwa sehemu ya maisha yake na alikuwa akipokea shoo za aina ya muziki wa Bongofleva, lakini ndani yake kulikuwa na hamu kubwa ya kuimba nyimbo za Gospel na kumtumikia Mungu kwa namna tofauti. Kauli hiyo ikawa moja ya hatua za mwanzo zilizosaidia kueleza mwelekeo mpya wa maisha yake.
JANUARI 2026: “WOKOVU UMENIBADILISHA”
Januari 2026, Mwanaspoti ilimfuatilia Ruby tena baada ya kufikisha miaka miwili tangu kuokoka.
Katika hatua hiyo, Ruby alisema wokovu ulikuwa umebadilisha maisha yake. Wakati huohuo, bado hakutaka kusema kwamba ameacha kabisa Bongofleva, lakini alieleza kuwa tayari alikuwa ameanza kuimba kanisani na kuingia studio kwa ajili ya kurekodi nyimbo za injili.
Hapo ndipo mabadiliko yake yalipoanza kuonekana kwa sura pana zaidi.
Haikuwa tena hamu ya kuitwa mtumishi pekee, bali kulikuwa na hatua ambazo alikuwa tayari anazichukua katika maisha yake na kwenye muziki.
Kutoka kwenye Bongo Fleva iliyomjengea jina, Ruby akaanza kuelekea zaidi kwenye muziki wa Injili, huku akiendelea na safari yake ya wokovu ambapo alikuwa akionekna sehemu mbalimbali za neno la injili na hata posti zake katika akaunti yake ya Instagram,zilikuwa zikionyesha mambo ya kiutumishi wa Mungu.
SEPTEMBA 2026: “SIPO DUNIANI KUPENDEZA WATU”
Sasa, Septemba 2026 ya hivi karibuni, Ruby ameweka msisitizo mkubwa zaidi na kuliambia Mwanaspoti kuwa sasa rasmi ameachana na muziki wa bongo fleva na kuwa bize na injili.
Miongoni mwa kauli zake ni kwamba hayuko duniani kuwafurahisha watu, akisisitiza kuwa alichagua kumfuata Yesu si kwa sababu ya watu wala kwa lengo la kuwapendeza.
Ruby ameliambia Mwanaspoti haya: “Nawapenda mashabiki zangu ila nampenda Yesu zaidi.”€
Kauli hiyo inaweka wazi kwamba maamuzi yake ya sasa hayaongozwi na matarajio ya watu kuhusu kile wanachotaka kumuona akikifanya.
Msanii huyo amesisitiza kuwa watu wanapaswa kumfuata Yesu na si Ruby, akieleza kuwa yeye si mtu wa kuwapeleka watu mbinguni na kwamba jukumu lake ni kufanya kile anachoamini Mungu anataka.
“Watu wabebe misalaba yao, huku kwa Ruby, wokovu ni safari ya mtu binafsi yenye changamoto, imani na wajibu wa kila mmoja katika maisha yake.”
Anasema: “Watu wanatakiwa waelewe wamfuate Yesu na sio Ruby, mimi ni binadamu mwenye historia na mapungufu yangu, hivyo sitaki mtu afanye maisha yake kuwa msingi wa imani. Nataka anayemuona Ruby wa sasa aone kwanza kile anachokiamini kuhusu Mungu.”
Pamoja na mwelekeo wake wa sasa wa kiimani, Ruby bado anatambuliwa kwa kazi alizofanya kwenye muziki wa Bongo Fleva. Hilo limeonekana pia kwenye Zikomo Africa & Caribbean Awards 2026, ambako ametajwa kuwa ‘Official Nominee’ wa Tanzania katika kipengele cha Best Zikomo Female Artist of the Year 2026. Uteuzi huo unakuja wakati ambapo Ruby amekuwa akizungumza wazi zaidi kuhusu mabadiliko ya maisha yake na namna imani ilivyobadili mtazamo wake kuhusu muziki na maisha kwa ujumla. Katika mtazamo huo, Ruby ameweka pia wazi kuwa maisha yake ya nyuma kwake ni ushahidi kwamba Mungu anaweza kubadilisha maisha ya mtu wakati wowote. Pia maisha hayo hayo yake ya zamani ndiyo ushahidi kwamba Mungu anaweza kufanya chochote na wakati wowote.
Na hapo ndipo safari yake inapoonekana kuchukua sura mpya kutoka kwa msanii aliyekuwa akitambulika zaidi kupitia Bongo Fleva, hadi mtu anayesisitiza zaidi kuhusu imani yake, wokovu na kile anachoamini Mungu anataka afanye.