Hapatoshi safari ya kufuzu AFCON 2027
Muktasari:
- Miongoni mwa timu zilizofanya vizuri katika michezo miwili ya mwanzo na kukusanya pointi sita ni Morocco, Ivory Coast, Gambia, Afrika Kusini, DR Congo, Rwanda, Mali na Guinea-Bissau.
CAIRO, MISRI: MBIO za kuwania nafasi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 zinazotarajiwa kufanyika Tanzania, Kenya na Uganda, zinatarajiwa kupamba moto kuanzia wiki hii, huku timu za taifa za Afrika zikirejea uwanjani kwa michezo ya raundi ya tatu na nne ya kufuzu mashindano hayo.
Michezo hiyo itakayochezwa kati ya Novemba 12 na 17, inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, hasa kwa timu ambazo zimeanza vizuri kampeni hizo na sasa zinakutana na wapinzani wao wa moja kwa moja katika michezo miwili ya nyumbani na ugenini.
Miongoni mwa timu zilizofanya vizuri katika michezo miwili ya mwanzo na kukusanya pointi sita ni Morocco, Ivory Coast, Gambia, Afrika Kusini, DR Congo, Rwanda, Mali na Guinea-Bissau.
Mojawapo ya michezo inayosubiriwa kwa hamu ni ya Kundi C, ambako Ivory Coast na Gambia, ambazo kila moja ina pointi sita, zitakutana mjini Bouake kabla ya kurudiana nchini Gambia, katika mji wa Bakau.
Ghana nayo inakabiliwa na mtihani mgumu itakapocheza michezo miwili dhidi ya Somalia, ikiwa na jukumu la kufufua matumaini yake ya kufuzu baada ya kupoteza mechi zake mbili za mwanzo.
Michezo hiyo miwili inaweza kuamua hatma ya Ghana katika kampeni hizo, ikizingatiwa kuwa timu hiyo inashika mkia katika kundi hilo bila pointi.
Kundi K pia litakuwa na pambano la timu mbili zilizoanza kwa ushindi, Mali na Rwanda, ambazo zote zina pointi sita. Timu hizo zitakutana mjini Bamako kabla ya kurudiana Kigali, Rwanda.
Katika Kundi J, Senegal na Msumbiji zina pointi nne kila moja, huku Sudan ikiwa nyuma kwa pointi moja. Michezo ya Senegal dhidi ya Sudan na ile ya Msumbiji dhidi ya Ethiopia inaweza kuwa na athari kubwa katika msimamo wa kundi hilo.
Morocco itakuwa na jukumu la kuendeleza rekodi yake nzuri katika Kundi A itakapokutana mara mbili na Niger, wakati Misri na Angola, ambazo kila moja ina pointi nne katika Kundi B, zikisaka matokeo yatakayozidi kuimarisha nafasi zao. Malawi ipo nyuma yao kwa pointi moja pekee.
Afrika Kusini, ambayo imeshinda michezo yake miwili ya mwanzo katika Kundi D, itakutana na Kenya, moja ya nchi zitakazoandaa fainali hizo. Kikosi cha Kenya kinaongozwa na kocha Benni McCarthy, aliyewahi kuwa mshambuliaji wa timu ya taifa ya Afrika Kusini.
DR Congo nayo itakuwa na jukumu la kulinda rekodi yake ya kutopoteza mchezo katika Kundi E itakapokutana mara mbili mfululizo na Sierra Leone.
Katika makundi mengine, F, G, H na I, ushindani bado ni mkubwa kutokana na tofauti ndogo ya pointi kati ya timu zinazowania nafasi za juu. Cameroon, Uganda na Algeria zinaongoza makundi yao, huku Benin na Burkina Faso zikilingana kileleni mwa Kundi F.
Kundi L linaongozwa na Guinea-Bissau yenye pointi sita, wakati Nigeria inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi tatu kabla ya kukutana mara mbili na Tanzania, ambayo ni mwenyeji mwenza wa mashindano hayo.
Tanzania, Kenya na Uganda tayari zimefuzu moja kwa moja kucheza fainali hizo kutokana na kuwa wenyeji wenza, bila kujali nafasi zitakazomaliza nazo katika makundi ya kufuzu.
Kwa mujibu wa mfumo wa kufuzu, katika makundi yenye nchi mwenyeji, timu itakayomaliza katika nafasi ya juu zaidi baada ya mwenyeji ndiyo itakayopata tiketi ya fainali. Katika makundi mengine, timu mbili zitakazomaliza katika nafasi mbili za juu zitafuzu.
Fainali za AFCON 2027, zitakazotambulika kwa jina la PAMOJA, zimepangwa kufanyika kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027, zikishirikisha mataifa matatu ya Afrika Mashariki, Tanzania, Kenya na Uganda.