Mambo 10 shoo ya Christian Bella Dar
Muktasari:
- Hata hivyo, Bella na wasanii wenzake waliweka historia ya burudani ya’live’ iliyotikisa ukumbi, japo kulijitokeza mambo kadhaa yaliyozua mjadala.
SHOO ya Christian Bella iliyofanyika Mlimani City imeacha gumzo kubwa jijini Dar es Salaam, ikiwa ni moja ya maonesho yaliyojaa burudani ya nguvu, mashabiki wakijazana na kucheza muda wote, huku hisia zikiwa mchanganyiko kutokana na baadhi ya changamoto za kiutendaji ndani ya ukumbi.
Hata hivyo, Bella na wasanii wenzake waliweka historia ya burudani ya’live’ iliyotikisa ukumbi, japo kulijitokeza mambo kadhaa yaliyozua mjadala.
1. Ukumbi wafurika mapema, shangwe latawala
Kuanzia saa moja jioni, ukumbi wa Mlimani City ulianza kufurika mashabiki waliofika kumuona Christian Bella akifanya shoo kama yake kama alivyoahidi kabla ya siku hiyo. Ukumbi ulijaa na muda wote watu walikuwa wakicheza, kuimba na kushangilia bila kuchoka.
2. Atawala jukwaa kwa ‘˜live performance’
Christian Bella alionyesha ubora wake wa muda mrefu jukwaani. Uimbaji wake wa hisia na nguvu uliwafanya mashabiki kusimama muda wote, wengine wakiimba naye wimbo kwa wimbo.
3. Kubadili mavazi mara tatu.
Kila baada ya nyimbo kadhaa Bella aliongeza ladha ya shoo kwa kubadilisha mavazi ambapo alifanya hivyo mara tatu. Kila aliporudi jukwaani alionekana akiwa na ‘mpya”, akishuka mara kwa mara kubadilisha nguo baada ya nyimbo kadhaa, huku akiwa na taulo jeupe la kujifutia jasho.
4. Mastaa kibao waibukia jukwaani
Shoo ilianza kwa wasanii mbalimbali kama Ally Choki, Linex, Joh Makini na Barnaba kabla ya Ommy Dimpoz kuibuka jukwaani. Dimpoz alipanda kuimba wimbo wa ‘Mama’ na Bella, jambo lililozua shangwe kubwa, hasa kutokana na tetesi za zamani za kutokuelewana kati yao.
5. Wimbo ‘Mama’ wagusa hisia za wengi
Wakati Christian Bella na Ommy Dimpoz wakiimba ‘Mama’, ukumbi mzima ulibadilika kihisia. Mashabiki walionekana kuguswa, wengine wakiimba kwa hisia kubwa kutokana na ujumbe wa wimbo huo.
6. VVIP, VIP na regular ilikuwa ishu
Baadhi ya mashabiki walilalamikia changamoto ya mpangilio wa viti baada ya maeneo kuchanganyika. VVIP zilikuwa na meza nyeusi, VIP vikiwa na viti vya kawaida maalumu, huku regular zikiwa za kawaida zaidi, lakini utekelezaji haukuonekana kuwa makini sehemu zote.
7. MC na baadhi ya mashabiki
Mshehereshaji wa shoo (MC) ni kama hakuitendea haki shoo hiyo kulingana na ukubwa wake, kwani mara kwa mara alikuwa akirudia kauli kama “mnanisikia?”€ na kuzungumza sana kuhusu VVIP, VIP na regular, jambo lililoonekana kuwachosha baadhi ya mashabiki na kushindwa kuleta msisimko wa shoo.
8. Bei ya vinywaji yazua minong’ono
Baadhi ya mashabiki walilalamikia bei ya vinywaji kuwa juu kupita kiasi, ambapo ‘baketi’ ya kawaida ilifikia hadi Sh40,000 wakati kiingilio cha kawaida kilikuwa Sh25,000, hali iliyozua mjadala mkubwa ukumbini.
9. Ishu ya mabaunsa na viti
Kulitokea malalamiko kuwa baadhi ya mabaunsa na wahudumu walihusika kupanga na kuuza viti ndani ya ukumbi. Wengine walibebea viti kutoka sehemu nyingine, wakati wengine walikuta viti vyao vimeondolewa baada ya kwenda kucheza mbele ya jukwaa, hali iliyosababisha zogo la hapa na pale.
10. Waitikiaji wa Bella waonekana wa kawaida
Tofauti na Bella aliyebadilisha mavazi, baadhi ya waitikiaji wake walionekana na mavazi ya kawaida zaidi, kama ya aina ya kanisani. Waliongozwa na ‘choir master’ akiwa jukwaani, jambo lililoibua mjadala mdogo kuhusu maandalizi ya timu nzima.
Kwa ujumla, shoo ya Christian Bella katika Mlimani City imeacha alama kubwa kwa upande wa burudani, mahudhurio na ‘collabo’ za wasanii wakubwa. Hata hivyo, changamoto za mpangilio na huduma zimeibua mjadala, jambo linaloacha funzo kwa waandaaji wa matamasha makubwa nchini. Bella ameendelea kuthibitisha kuwa bado ni miongoni mwa wakali wa ‘live stage’ Tanzania.