Nyuma ya pazia ya kugombana kwa 'A Listi'
Muktasari:
- Akifichua yanayojiri ndani ya kundi lao, Uwoya ameliambia Mwanaspoti kuwa, wao huwa wanagombana mara nyingi, kiasi kwamba wakati mwingine wote hujikuta wamenuniana, lakini baadaye hurudi kuzungumza kama kawaida. Na hii tabia hawajaianza sasa ni toka kipindi cha miaka ya nyuma.
URAFIKI wa mastaa wanne wa Bongo Movie, Aunt Ezekiel, Irene Uwoya, Jacqueline Wolper na Kajala Masanja, unaonekana kuwa na upande ambao mashabiki wengi hawaushuhudii, hasa wanapokutana na tofauti, kugombana na kununiana kabla ya kurejea katika maelewano.
Akifichua yanayojiri ndani ya kundi lao, Uwoya ameliambia Mwanaspoti kuwa, wao huwa wanagombana mara nyingi, kiasi kwamba wakati mwingine wote hujikuta wamenuniana, lakini baadaye hurudi kuzungumza kama kawaida. Na hii tabia hawajaianza sasa ni toka kipindi cha miaka ya nyuma.
“Nyinyi mtuone tu hivi sisi, huwa tunaishi maisha ya kugombana sana, hata hizo habari zinazosemwa kuwa tumegomba huwa ni za kweli na wala sio kiki, sema tu hatuziweki mbele ya jamii, kwenye kundi letu unaweza kukutana tumegombana na tumenuniana wote, halafu ghafla tukajikuta tunaongea tu,” amesema Uwoya.
Kauli hiyo inaonyesha kuwa kugombana si jambo geni katika urafiki wao. Hata hivyo, Uwoya amesema tofauti hizo hazimaanishi mwisho wa urafiki wao, kwani wakati mwingine mmoja hulazimika kujishusha ili maelewano yarudi.
Akieleza zaidi kuhusu tabia zao wanapokuwa na tofauti, Uwoya amesema yeye ni mtu anayependa kusema ukweli bila kuzunguka, huku akimtaja Aunt na Wolper kuwa miongoni mwa wanaoweza kujishusha ili mambo yaendelee vizuri.
“Mimi ni mtu ambaye nimenyooka, sipendi kona kona. Kitu kama ni bluu nitasema bluu, siwezi kusema nyeupe,” amesema.
Pia amegusia suala la kubembelezwa ndani ya kundi hilo, akisema yeye hajioni kama mtu anayependa kuombewa sana, bali anaamini nafasi yake kama mtoto wa kwanza inamtaka kuwa imara. Aidha Uwoya amesema haya maisha ndio ambayo wamekuwa wakiishi toka wameanza kufahamiana kwenye kazi ya Sanaa, na ndio maana kipindi cha nyuma hawakuwa watu wa kuonekana sana karibu tofauti na sasahivi ukaribu wao upo haswa kwenye kipindi chao cash A Listi.
“Kwasasa kila mmoja amejifunza namna ya kuishi na tabia za mwenzake ,hivyo hata tukigombana utakuta huwa tunayamaliza mapema, ila kipindi cha nyuma ilikuwa kugombana yaani tunaweza Kaa hata miezi au mwaka hakuna kutafuta au kuongea,lakini ikitokea basi huwa hivyo tunakuwa sawa,” amesema Uwoya.