Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shakira, Burna Boy walivyoendeleza rekodi Billboard Hot 100

Muktasari:

  • Dai Dai ni wimbo unaohimiza umoja dunia kote kupitia michuano hiyo ya juu zaidi katika soka inayofanyika katika nchi tatu tofauti ambazo ni Marekani, Mexico na Canada.

Wimbo maalum wa Kombe la Dunia 2026 uitwao ‘Dai Dai’ ulioimbwa na mwanamuziki Shakira kutokea Colombia pamoja na Burna Boy wa Nigeria, unaendelea kufanya vizuri na sasa ukiweka rekodi chati ya Billboard Hot 100.

Dai Dai ni wimbo unaohimiza umoja dunia kote kupitia michuano hiyo ya juu zaidi katika soka inayofanyika katika nchi tatu tofauti ambazo ni Marekani, Mexico na Canada.

Jina la wimbo huo limetokana na lugha ya Kiitaliano na ni msemo wa mitaani unaomaanisha ‘twenzetu’ au ‘chapa mwendo’, ukilenga kuhamasisha watu kujitoa kwa asilimia 100 hasa katika mashindano makubwa kama Kombe la Dunia.

Ni wimbo ulioandikwa kwa lugha tano ambazo ni Kiingereza, Kihispania, Kiitaliano, Kifaransa na Kijapani, huku ukichanganya ladha mbalimbali za muziki kama Afrobeats, Dance Pop, Reggaeton n.k.

Ukiwa umesimamiwa na Ace Entertainment na Sony Music Latin, wimbo huo ndani yake umetaja majina ya wachezaji wakubwa duniani kama Pele, Diego Maradona, Cristiano Ronaldo, Lionel Messi na Mohamed Salah.

Baada ya kuvuma kwa siku zaidi ya 40, hatimaye wimbo wa Dai Dai (2026) umefanikiwa kuingia chati ya Billboard Hot 100 ukishika nafasi ya 75 kutokana na mafanikio yake makubwa nchini Marekani.

Mafanikio hayo yamekuja baada ya Shakira na Burna Boy kuimba wimbo huo mbele mashabiki zaidi ya 80,000 katika sherehe za ufunguzi wa Kombe la Dunia la 2026 zilizofanyika Juni 11 katika Uwanja wa Estadio Azteca, Mexico City.

Kwa ujumla Dai Dai umekuwa wimbo wa nne rasmi wa Kombe la Dunia kuingia kwenye chati ya Billboard Hot 100, huku nyimbo mbili kati ya hizo zikiwa za Shakira, mpenzi wa zamani wa Gerard Pique.

Orodha ya nyimbo rasmi za Kombe la Dunia la FIFA zilizowahi kuingia chati ya Billboard Hot 100, ni kama ifuatavyo; The Cup of Life (1998) wake Ricky Martin - nafasi ya 45 mwaka 1999, Waka Waka (This Time for Africa) (2010) wake Shakira na Freshlyground - nafsi ya 38.

Nyingine ni We Are One (Ole Ola) (2014) wake Pitbull, Jennifer Lopez na Claudia Leitte - nafasi ya 59, na sasa Dai Dai (2026) wake Shakira na Burna Boy - nafasi ya 75.

Ikumbukwe mbali na kuwa na nyimbo za Kombe la Dunia katika Billboard Hot 100, pia Shakira anashikilia rekodi ya kutumbuiza katika fainali nne za michuano hiyo akifanya hivyo 2006 (Ujerumani), 2010 (Afrika Kusini), 2014 (Brazil) na 2026 (Mexico).

Mashindano ya Kombe la Dunia yalianza rasmi mwaka 1930, lakini shirikisho la soka duniani (FIFA) lilianza kutumia nyimbo rasmi za mashindano hayo yanayofanyika kila baada ya miaka minne kuanzia mwaka 1990.

Wakati huo huo, Dai Dai imepanda hadi nafasi ya saba kwenye chati ya Billboard Global Excl. U.S., kutoka nafasi ya 23. Pia umefika nafasi ya kwanza kwenye chati ya Billboard Colombia Hot 100 na kuingia kwenye 10 bora katika chati zaidi ya 12 za Billboard kimataifa.

Juni 18, Shakira aliwashukuru mashabiki wote duniani baada ya video ya wimbo kufikia rekodi ya kutazamwa (views) zaidi ya milioni 100 YouTube, na sasa umefikia milioni 243.

Video hiyo iliyoshutiwa huko Miami, Florida, inaanza kwa kuwaonyesha wachezaji maarufu kama Lionel Messi, Kylian Mbappe na Erling Haaland. Vilevile inaonyesha picha ya uhuishaji ya Shakira akiwa juu ya mnara maarufu wa Angel of Independence uliopo Mexico City.

Ikumbukwe Waka Waka (This Time for Africa) (2010), ndio wimbo wa Shakira wenye mafanikio makubwa zaidi katika mtandao wa YouTube ambapo video yake imetazamwa zaidi ya mara bilioni 4.5 YouTube ikiwa ni kazi yake ya kwanza kufikia namba hizo.

Katika ufunguzi wa Kombe la Dunia 2010 huko Afrika Kusini kwenye uwanja wa Orlando jijini Johannesburg, Shakira alitumbuiza wimbo huo ambao aliishirikisha bendi ya Freshlyground ya nchini humo.

Show hiyo ambayo ilipambwa pia na wasanii wengine kama Pitbull, Jennifer Lopez (J.Lo) na Claudia Leitte, kabla ya Shakira kuimba wimbo huo, aliimba nyimbo zake maarufu kama Hips Don’t Lie (2006) na She Wolf (2009).

Haikuishia hapo, Shakira na Freshlyground Band walitumbuiza tena wimbo huo katika sherehe za kufunga mashindano hayo katika uwanja wa Soccer City, ambapo ilichezwa fainali kati ya Uholanzi na Hispania walioibuka mabingwa.