Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Sajili’ tano Yanga Princess na rekodi zao

DIR 06

Muktasari:

  • Miongoni mwa sajili hizo tano kuna wachezaji kutoka Ethiopia, Rwanda, Uganda na Nigeria, huku baadhi yao wakiwa na uzoefu wa mashindano ya kimataifa ikiwamo Ligi ya Mabingwa Ulaya.

YANGA Princess imeamua kuvuka mipaka katika kusuka kikosi chake cha msimu wa 2026/27, ikiwaleta nyota kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, huku ikilenga kuongeza ushindani kwenye maeneo muhimu ya timu hiyo.

Miongoni mwa sajili hizo tano kuna wachezaji kutoka Ethiopia, Rwanda, Uganda na Nigeria, huku baadhi yao wakiwa na uzoefu wa mashindano ya kimataifa ikiwamo Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mwanaspoti linakuchambulia baadhi ya sajili tano za timu hiyo na rekodi zao walipotoka.


SAJI 01

1. MESAY TEMESGEN – ETHIOPIA

Huu utakuwa usajili wa pili kutoka Ethiopia kuitumikia  Ligi ya Wanawake msimu huu baada ya awali Simba Queens kumtambulisha Senaf Demise wote kutoka CBE.

Mesay ni kiungo mwenye uwezo wa kucheza pia eneo la mbele. Akiwa CBE, alicheza mashindano mbalimbali makubwa ikiwemo ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ameitumikia timu ya taifa ya Ethiopia.

Msimu uliopita alifunga mabao mawili katika mechi 18. Alicheza mechi tatu na kuanza zote, akifikisha dakika 250, huku akiwa na bao moja katika mashindano hayo

Uzoefu wa kucheza mashindano makubwa kama CECAFA na Ligi ya Mabingwa Afrika, unaweza kuwa msaada kwa Yanga ambayo imeonekana kujijenga upya.


SAJI 02

2. SANDRINE MUTUYIMANA – RWANDA

Huyu ni mshambuliaji wa Rwanda ambaye Yanga Princess ilianza kumfuatilia baada ya kufanya majaribio katika kikosi hicho.

Sandrine alikuwa akiichezea Inyemera WFC na kabla ya kusaini Yanga Princess alikuwa miongoni mwa washambuliaji waliokuwa wakifanya vizuri katika soka la wanawake Rwanda.

Msimu uliopita nyota huyo alikuwa anaongoza kwenye vita ya ufungaji bora akipachika mabao 10 katika mechi nane.

Baada ya kuvutia benchi la ufundi, akasaini mkataba wa miaka mitatu na Yanga Princess.

Ni usajili unaokwenda kuongeza nguvu kwenye nafasi ya ushambuliaji ambayo msimu uliopita ilikuwa inaongozwa na Jeanine Mukandayisenga ambaye alimaliza mfungaji bora akipachika mabao 20.


SAJI 03

3. SUMAYA KOMUNTALE – UGANDA

Usajili mwingine ni wa beki wa kushoto, Komuntale aliyesaini mkataba wa miaka miwili akitokea She Cooperate kutoka Uganda.

Komuntale, ambaye awali alikuwa nahodha wa Tooro Queens, amewahi pia kucheza Kampala Queens na ameiwakilisha Uganda katika ngazi mbalimbali za timu za taifa, kuanzia za vijana hadi Uganda Queens na ya wakubwa, Crested Cranes.

Beki huyo anatajwa kuwa miongoni mwa mabeki bora wa kushoto katika ukanda huo kutokana na uwezo wake wa kupiga mipira iliyokufa, kutoa krosi sahihi na uelewa mzuri wa kiufundi.

Anakuja Yanga wakati ambao nafasi anayocheza walikuwepo nyota kama Wincate Kaari raia wa Kenya na Mtanzania Protasia Mbunda ambaye mwishoni mwa msimu uliopita alikubwa na majeraha ya goti.


SAJI 04

4. JOAN NABIRYE – UGANDA

Yanga imemsajili akitokea WFC Nike Lusso ya Georgia ambayo inacheza michuano mikubwa ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Nabirye ambaye kabla ya kutimkia huko, kiungo huyo mkabaji, alicheza msimu wa 2023 akiwa Minsk FK ya Belarus, alicheza mechi 25 na kufunga mabao sita, mbili za Ligi ya Mabingwa ya Ulaya UEFA.

Machi 2024 alihamia Spartak Moscow kama mchezaji huru, kabla ya kujiunga na Trabzonspor Women Januari 2025. Akiwa Uturuki katika msimu wa 2024/25, alicheza mechi moja ya ligi na kufunga bao moja, hivyo rekodi yake ya ligi katika kipindi hicho ikiwa mechi 26 na mabao saba.

Ni usajili unaoweza kuongeza nguvu eneo la kiungo kutokana na uzoefu wake wa kucheza nafasi ya kiungo mkabaji na uwezo wa kusaidia timu kwenye beki.


SAJI 05

5. BARAKAT OLAIYA – NIGERIA

Hili ni jina ambalo mashabiki wa soka la wanawake Tanzania wanalifahamu. Olaiya, raia wa Nigeria, amewahi kuitumikia Simba Queens msimu wa 2022/23 kabla ya kuhamia Asa Tel Aviv ya Israel.

Akiwa Simba Queens, Barakat alifanya vizuri katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake mwaka 2022 akiisaidia Simba kufika nusu fainali na kufunga mabao mawili.

Rekodi yake ya nyuma inaifanya hii kuwa moja ya sajili zinazoweza kuvutia zaidi, hasa kwa mashabiki wanaomkumbuka kutokana na kiwango alichoonyesha akiwa Simba Queens.


WANAINGIA NA UZOEFU GANI?

Kwa jumla, sajili hizi zinaonyesha Yanga Princess haijaangalia majina pekee, bali imejaribu kuongeza wachezaji wenye uzoefu tofauti.

Mesay ana uzoefu wa Ethiopia na mashindano ya CAF, Sandrine anaingia akiwa na rekodi nzuri ya mabao Rwanda, Sumaya ana uzoefu wa timu ya taifa Uganda, Nabirye ana uzoefu wa ligi za Afrika Mashariki na soka la kimataifa, wakati Barakat tayari ana kumbukumbu ya kucheza na kufanya vizuri kwenye hatua ya CAF.

Mtihani uliopo Yanga kwa sasa si kuwasajili nyota hao bali namna kocha atakavyowachanganya na wachezaji waliokuwepo ili kuunda kikosi chenye uwezo wa kupambana katika Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania.