Prime
Kadi tatu nyekundu Simba, FVS yazua jambo!
KUNA tatizo kubwa la nidhamu ya wachezaji ndani ya uwanja. Yale matukio waliyozoea kuyafanya kimyakimya misimu ya nyuma katika Ligi Kuu Bara kisha yakapita kama hakijafanyika kitu, sasa yanafichukuliwa na matumizi ya teknolojia ya Football Video Support (FVS), huku adhabu zikiwemo kadi nyekundu zikionyeshwa hapohapo.
Katika Ligi Kuu Bara msimu wa 2026-2027, matukio hayo yameanza kufichuka haraka jambo ambalo kwa muda mrefu lilikuwa likipita bila kuonekana moja kwa moja na waamuzi.
Si hayo tu, FVS imetumika katika matukio mbalimbali ikiwemo kuamua adhabu ya penalti na mabao ambayo awali yalionekana kama kuna viashiria vya kuotea, lakini mapitio yalisahihisha.
Msimu uliopita na ile ya nyuma yake, matukio kama hayo mwisho wa siku tuliyachukulia kama matatizo ya kibinadamu kwa waamuzi kupitiwa, lakini sasa hakuna kisingizo. Anayefanya madudu, anafichuliwa papo hapo, haki inatendeka bila ya kusubiri Kamati ya Saa 72 ikutane.
Tukiwa katika raundi tatu za mwanzo ndani ya Ligi Kuu Bara, matumizi ya FVS yameonyesha si tu uwezo wa teknolojia kusaidia waamuzi kufanya uamuzi sahihi, bali pia namna baadhi ya wachezaji wanavyocheza kwa kutumia nguvu kupita kiasi, kucheza rafu hatarishi na kufanya vitendo ambavyo msimu uliopita vingepita bila adhabu ya papo kwa papo.
Simba ndiyo imekuwa mfano mkubwa wa hali hiyo, ikiwa na wachezaji watatu waliotolewa kwa kadi nyekundu katika mechi zake tatu za kwanza, huku matukio yote yakibainika baada ya matumizi ya FVS.
David Kameta ‘Duchu’ alikuwa wa kwanza kuonyeshwa kadi nyekundu katika ushindi wa Simba wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar, Agosti 16, 2026, baada ya kumchezea madhambi nahodha wa wapinzani, David Luhende.
Siku tatu baadaye, kiungo raia wa Nigeria, Ibraheem Jabaar naye alitolewa kwa kadi nyekundu katika ushindi wa Simba wa mabao 2-1 dhidi ya Pamba Jiji, Agosti 19, 2026, baada ya kumchezea madhambi Abdulkarim Yunus.
Hali hiyo ikaendelea Agosti 22, 2026, Anthony Mligo akionyeshwa kadi nyekundu katika ushindi wa Simba wa mabao 2-1 dhidi ya Singida Black Stars baada ya kumkanyaga kwa nyuma Yusuph Khamis.
Matukio hayo matatu yalifanyiwa mapitio kwa kutumia FVS, jambo linaloibua swali kwamba msimu huu wachezaji wamekuwa na nidhamu mbaya zaidi au teknolojia imeanza kuyaweka wazi makosa yaliyokuwa yakipita bila kuonekana?
Katika kadi tano nyekundu zilizotolewa hadi sasa msimu huu, nne zimehusisha matumizi ya FVS. Mbali na tatu za Simba, nyingine ni ya nahodha na kiungo wa Coastal Union, Jofrey Manyasi, aliyeonyeshwa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Yanga.
Manyasi alionyeshwa kadi hiyo baada ya mwamuzi wa kati, Raphael Ikambi wa Morogoro, kujiridhisha kupitia FVS kuwa mchezaji huyo alimkanyaga vibaya kiungo wa Yanga, Mkenya Duke Abuya, katika mchezo uliochezwa Agosti 20, 2026 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Hali hiyo inaonyesha sura mpya ya soka la Tanzania, ambapo vitendo vya wachezaji ambavyo huenda vilikuwa vikifichika katika kasi ya mchezo sasa vinaweza kufuatiliwa na kuamuliwa kupitia teknolojia.
ILIVYOKUWA MSIMU ULIOPITA
Msimu wa 2025-2026 kulikuwa na matukio kadhaa ambayo waamuzi hawakuyaona kwa wakati, lakini baadaye yaliamuliwa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).
Miongoni mwa matukio hayo ni ya aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Seleman Mwalimu ‘Gomez’, ambaye alifungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya Sh1 milioni kwa kumpiga kiwiko beki wa Dodoma Jiji, Andy Bikoko, katika mchezo uliomalizika kwa matokeo ya 0-0, Februari 25, 2026.
Beki wa Yanga, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, naye alifungiwa mechi tano baada ya kubainika kumkanyaga kwa makusudi beki wa Mbeya City, Ibrahim Ame, katika mchezo uliochezwa Septemba 30, 2025, Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Katika tukio hilo, mwamuzi wa kati, Omary Mdoe wa Tanga, naye alifungiwa mechi tano kwa kushindwa kuchukua hatua zinazostahili dhidi ya kitendo hicho.
Kiungo wa Yanga, Mudathir Yahya, pia alifungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya Sh1 milioni baada ya kumpiga kiwiko beki wa Pamba Jiji, Ibrahim Abraham, katika mchezo wa Aprili 8, 2026, Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Yanga ilishinda mchezo huo kwa mabao 3-0, huku Mudathir akifunga mawili, lakini baada ya mchezo huo kamati husika ilimchukulia hatua kutokana na tukio ambalo mwamuzi hakuliona wakati mchezo ukiendelea.
Msimu uliopita hadi unamalizika, kulikuwa na kadi nyekundu 19 zilizoonyeshwa kwa timu tisa kati ya 16 zilizoshiriki Ligi Kuu Bara.
Timu zilizokumbwa na adhabu hiyo ni JKT Tanzania (4), TRA United (3), Namungo (2), Mashujaa (2), Azam (2), Mbeya City (2), KMC (2), Mtibwa Sugar (1), Coastal Union (1).
Ambazo hazikuonyeshwa kadi nyekundu ilikuwepo Simba, Yanga, Singida Black Stars, Dodoma Jiji, Fountain Gate, Pamba Jiji na Tanzania Prisons.
Hadi zinamalizika raundi tatu za kwanza kama ilivyo sasa, kulikuwa na kadi moja tu nyekundu iliyokwenda kwa Lucas Kikoti wa Namungo ambayo alionyeshwa katika mechi dhidi ya Tanzania Prisons iliyochezwa Septemba 21, 2025.
Wachezaji walioonyeshwa kadi nyekundu msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara ni Lucas Kikoti (Namungo), Ramadhan Chalamanda (JKT Tanzania), Mohamed Mussa (Mashujaa), Hamis Mgunya (Namungo), Yeison Fuentes (Azam), Vitalis Mayanga (Mbeya City), Salum Khamis (JKT Tanzania), Omary Yusuph (TRA United), Karimu Mfaume (JKT Tanzania), Castor Mwangabo (KMC), Haroun Lyawatwa (Mtibwa Sugar), Feisal Salum (Azam), Mzamiru Yassin (TRA United), Valentin Nouma (TRA United), Nickson Mosha (KMC), Wilbol Maseke (Coastal Union), Hashim Mussa (Mbeya City), Abdul Bakari (Mashujaa) na Hassan Wahabi (JKT Tanzania).
FVS SULUHISHO
Kwa mtazamo mpana, matukio hayo yanaonyesha kuwa FVS yenyewe si tatizo. Badala yake, teknolojia hiyo inaweza kuwa kioo kinachoonyesha tatizo lililokuwepo ndani ya mchezo lakini ambalo halikuwa rahisi kuonekana kwa macho ya mwamuzi.
Tofauti kubwa ni kwamba msimu uliopita mchezaji angeweza kufanya kitendo cha hatari na kuendelea na mchezo endapo mwamuzi hakukiona. Hatua dhidi yake zingeweza kuchukuliwa baadaye, baada ya kamati kukagua tukio na kutoa adhabu.
Sasa kupitia FVS, baadhi ya matukio hayo yanaweza kubainika ndani ya mchezo na mchezaji kupewa adhabu papo hapo.
Hivyo, ongezeko la kadi nyekundu halipaswi kutazamwa pekee kama tatizo la waamuzi au teknolojia, bali pia kama ishara inayopaswa kuyataka mabenchi ya ufundi, viongozi na wachezaji kutazama upya suala la nidhamu uwanjani.
Kwa Simba, kadi nyekundu tatu katika mechi tatu ni ujumbe mzito unaohitaji uchunguzi wa ndani wa klabu. Je, wachezaji wanakosa udhibiti wanapokabiliwa na presha? Je, mfumo wa uchezaji unawasukuma kufanya makosa hayo? Au ni tabia binafsi za wachezaji?
Hivi karibuni, Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker wakati anakiandaa kikosi chake kukabiliana na Singida Black Stars huku akiwa tayari ameshuhudia nyota wake wawili wakionyeshwa kadi nyekundu, amesema hatavumilia kuona hilo likijitokeza katika michezo inayofuatia.
"Tunatakiwa kuonyesha kuwa sisi ni timu kubwa, hivyo tunapaswa kuonyesha nidhamu kubwa ya mchezo, hatua ya kwanza nimeongea nao ili kuona wepesi wa kufanikisha hili, baada ya hapo tutaona hatua nyingine za kufuata.
“Ni wazi kwamba unapokuwa na wachezaji waliosimamishwa inakuwa ngumu, lakini timu hazipati mafanikio kwa kutegemea wachezaji 11 pekee. Ni kikosi kizima ndicho kinachofanikiwa,” amesema Barker. Hata hivyo, Mligo akaja kuonyeshwa kadi nyekundu dhidi ya Singida.
MABAO, PENALTI
FVS mbali na kuamua kadi nyekundu nne, pia teknolojia hiyo imezinufaisha timu kadhaa katika kupatikana mabao na penalti. Matukio mawili katika raundi ya tatu ilishuhudiwa bao la mshambuliaji wa Geita Gold, Richardson Ngodya dhidi ya Kagera Sugar, awali mwamuzi amesema aliotea, lakini teknolojia hiyo ikathibitisha lilikuwa halali.
Pia Simba ilipata penalti iliyozaa bao la pili baada ya mapitio ya FVS kumnasa Ahmed Pipino wa Singida Black Stars alikuwa amemfanyia madhambi Ismael Toure kwenye eneo la hatari.
Kabla ya hapo, Pamba Jiji nayo ilipata penalti baada ya mapitio ya FVS dhidi ya Simba, Idris Diomande akafunga.
Penalti mbili za mchezo wa Polisi Tanzania na Azam, zote zilipatikana kwa msaada wa FVS, mechi ikamalizika kwa sare ya 1-1 kupitia penalti hizo ikiwa ni mechi ya mzunguko wa kwanza.
SIKIA HII
Kocha wa Coastal Union, Fikiri Elias, amesema: "Teknolojia hiyo imekuja kutusaidia na kufanya mpira wa miguu uwe na maendeleo makubwa, ingawa bado ni mapya kwetu hata sisi makocha, ila tutazidi kuwaelekeza wachezaji kuuelewa mfumo mpya.
"Kadi nyekundu aliyopata mchezaji wetu Jeofrey Manyasi nilipozungumza na mchezaji alikiri ni kweli, ila lengo lake lilikuwa kuuwahi mpira lakini akawahiwa na mguu wa Duke Abuya wa Yanga, kikubwa tutazidi kuwaelimisha wachezaji."
Mchezaji wa Mbeya City, Rashid Juma, amesema: "Ni mfumo mzuri, lakini bado tunahitaji elimu kubwa ili tuendane nao, lakini unasaidia sana kutenda haki, dakika 90 zinapomalizika kunakuwa hakuna mtu analalamika."
Mchezaji wa zamani wa Simba na Yanga, Mohamed Banka, amesema: "FVS ni mfumo mzuri kwani unazidi kukuza sola la Tanzania kuwa bora na hiyo itawasaidia sana wachezaji wanapocheza mechi za kimataifa kujua namna ya kuepuka makosa ya kizembe."
Kaimu Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi Kuu Kuu Tanzania (TPLB), Yahya Abushee, amesema: "Tuliwasilisha kanuni zinazoelekeza haruhusiwi mtu yoyote kumlazimisha mwamuzi kufanya jambo, isipokuwa makocha wawasiliane na mwamuzi wa pembeni, mwamuzi wa pembeni atamwambia mwamuzi wa kati kisha changamoto inatatuliwa.
"Endapo kama kuna timu inahitaji ufafanuzi wa jambo lolote, TPLB milango ipo wazi kwa ajili ya kutoa elimu, lengo letu ni kuona mpira wa miguu nchini inafika mbali, tunafanya kazi kwa ajili ya klabu hivyo zipo huru kuwasiliana na bodi."
Mtaalamu wa saikolojia, Charles Nduki, amesema: "Wachezaji wakati mwingine wanapitia changamoto nyingi, inapaswa kuwajenga kiakili ili kurejesha akili mchezoni, ndiyo maana kuna haja ya wanasaikolojia kuzungumza nao mara kwa mara."
NYEKUNDU TATU ZA SIMBA
Kadi tatu nyekundu walizoonyeshwa mastaa wa Simba kwenye mechi tatu mfululizo huku timu hiyo ikiondoka na ushindi, zimechambuliwa na wadau huku wakimpa saluti kocha wa timu hiyo, Steve Barker kutokana na mbinu zake kutiki.
Licha ya kumpa saluti, lakini wadau hao wamemkumbusha Barker aimarishe nidhamu ya wachezaji wa kikosi hicho kwani inaweza kuwagharimu mbele ya safari.
Japokuwa beki wa pembeni wa Simba, David Kameta 'Duchu' alipewa kadi nyekundu dakika ya 54, timu hiyo ililinda ushindi wake hadi dakika ya 90, Simba ikishinda 2-0 dhidi ya Kagera Sugar.
Baada ya hapo, Simba ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Pamba Jiji, licha ya kiungo wake, Ibraheem Jabaar kuonyeshwa kadi nyekundu dakika 42.
Timu hiyo ikashinda tena mabao 2-1 dhidi ya Singida BS, wakati ambapo dakika ya 85, beki wake wa kushoto, Anthony Mligo alionyeshwa kadi nyekundu.
Ingawa wadau walishauri kocha Barker asisitize nidhamu kwa wachezaji wake, lakini walimpongeza kwa utulivu aliyoujenga kwa mastaa wake kutotoka mchezoni hata wanapocheza pungufu.
Staa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella, alianza kwa kumshauri kocha Barker kujenga nidhamu ya wachezaji uwanjani, ingawa kimbinu aliona ameweza kuzijenga saikolojia za wachezaji kutekeleza anachowaambia.
"Faida ya Simba waliyoipata wamekutana na timu ambazo wamezizidi uwezo, ni kitendo kibaya sana kwa kila mechi timu kupata kadi, huko ni kukosa nidhamu kiwanjani, ingawa kimbinu Barker amewajenga wachezaji utulivu hata wanapocheza timu pungufu," amesema Mogella na kuongeza;
"Mbali na kocha viongozi wa Simba wanaona jambo hilo ni la kawaida kwa wachezaji kupata kadi nyekundu kwa mfululizo, kwa ukubwa wa klabu, lazima waepukane na hilo."
Kiungo mkabaji wa zamani wa Simba, Yanga na Stars, Mohamed Banka, amesema kadi mbili dhidi ya Kagera na Singida BS zilitokea kwa makosa ya kawaida ya kimchezo, lakini dhidi ya Pamba ilikuwa ya kinidhamu moja kwa moja, huku akimpa saluti Barker kwamba kimbinu alikuwa vizuri.
"Mbinu za kocha wa Simba anawanyima nafasi wapinzani ya kucheza ndiyo maana wanakuwa wanarudisha mipira nyuma, kuna muda wanajipa utulivu kama wa kupunguza kasi, baada ya muda wanaibuka kwa kasi kubwa kushambulia, hilo linaonyesha wapo fiti, kwani siyo rahisi kumudu majukumu baada ya kupungua kama wachezaji pumzi yao inakata mapema.
"Kadi nyekundu dhidi ya Kagera Sugar, mchezaji alikuwa anakwenda kuokoa mpira, katika harakati za kuwania wote wawili akajikuta anafanya makosa, vivyo hivyo kwa mchezo wa Singida BS hapo huwezi kusema ni ukosefu wa nidhamu, tofauti na ile ya Pamba ambako mchezaji alioonyesha ni kosa la makusudi, hilo unaweza ukaliita kosa la kinidhamu.
"Simba ikicheza pungufu tangu zamani ni ngumu kuwafunga, nakumbuka wakati nacheza Yanga mwaka 2006 mwamuzi alikuwa Othoman Kazi, alimpatia kadi nyekundu mchezaji wa Simba, sikumbuki vizuri alikuwa nani, pamoja na hilo walitushambulia hadi wakashinda mechi."