Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ABUYA: Injini ya Yanga iliyoiacha miguu izingumze

Muktasari:

  • Kuondoka kwake mwanzoni mwa msimu huu wa 2025-2026 kwenda kujiunga Singida Black Stars kuliacha maswali mengi.

HAKUNA ubishi kwa misimu kama minne hivi, jina la Khalid Aucho lilikuwa kama alama ya uimara na utulivu katika safu ya kiungo ya klabu ya Yanga.

Kuondoka kwake mwanzoni mwa msimu huu wa 2025-2026 kwenda kujiunga Singida Black Stars kuliacha maswali mengi.

Miongoni mwa maswali ni ‘Yanga inaweza kumpata mbadala wa kiwango chake?’...’Nani wa kuziba nafasi yake?’ Hata hivyo, ndani ya muda mfupi tu, majibu ya maswali hayo yameanza kujitokeza uwanjani na jibu hilo ni Duke Abuya.

Yanga waliachana na Aucho baada ya mkataba aliokuwa nao kumalizika mwishoni mwa msimu uliopita na kutokukaa naye mezani kuzungumza ili kumuongezea mkataba mpya na badala yake mabosi wa Yanga waliamua kuongeza nyota wapya wakimnasa Moussa Balla Conte aliyejiunga na Yanga akitokea CS Sfaxien ya Tunisia ambaye waliamini atakuwa mbadala sahihi wa Aucho lakini mambo yamekuwa tofauti. Pia Yanga ilimbeba dogo kutoka Zenji, Abdulnassir Abdallah ‘Casemiro’ ambaye bado hajaaminiwa.

Hata hivyo, kumbuka Yanga ilikuwa na jembe moja kikosini nalo si jingine Duke Abuya ambaye amedhihirisha kuwa ameshateka rasmi ufalme wa Aucho Jangwani. Ndivyo ukweli ulivyo kutokana na Mkenya huyo kufanya kazi kwa utulivu, akiacha miguu yake izungumze zaidi. Anacheza kwa ukomavu, akili na nidhamu ya kiufundi inayokaribia falsafa ya Aucho.

Abuya sasa anazidi kuteka mioyo ya mashabiki wa Yanga.

Yanga eneo la kiungo sasa lina Abuya na Mudathir Yahya ukimuondoa Aziz Andabwile, ambaye chini ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Romain Folz  aliaminiwa na kutumika mechi kadhaa kabla ya jamaa kuondoka naye kurudishwa benchi, pia kuna Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ ambaye amepoteza namba kabisa kikosini hadi benchi.

Jina linaloimbwa kwa sasa ni Abuya, si kwa bahati mbaya, ni kiungo  aliyefanikiwa kuliteka benchi la ufundi la Yanga na anadhihirisha kwa uwezo alionao katika mechi zote alizocheza msimu huu.

Utabisha nini? Katika mechi mbili zilizopita za Ligi Kuu dhidi ya Fountain Gate na Coastal Union ametoa asisti za upendo kwa Pacome Zouzouana Prince Dube na jamaa kuifungia Yanga mabao muhimu yaliyoiwezesha timu kupanda hadi nafasi ya pili ya msimamo, licha ya kucheza mechi sita tu.

Ameonyesha uimara eneo hilo na kufuta utawala wa jina la Aucho.

Dirisha kubwa la usajili jina la Conte lilifunika sajili nyingi Ligi Kuu Bara hii ni kutokana na kutajwa timu zote mbili Simba na Yanga, na baadaye wana Jangwani walifanikiwa kunasa saini yake. Lakini sasa hana anachokifanya, anaishia kukaa benchi huku Abuya na Mudathir Yahya ndio wenye uhakika wa namba.


PASI SAHIHI

Kiungo mkabaji anahitaji kuwa na nidhamu ya kucheza katika nafasi yake ili kujenga safu ya ulinzi bora ya ziada na kuzuia timu kushambuliwa kiurahisi, hicho ndicho kinafanywa na nyota huyo. Nidhamu hii inampa nafasi ya kuwa mchezaji muhimu, si tu kwa klabu bali pia kwa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars ambayo amekuwa akiitwa mara kwa mara.

Abuya ana nidhamu nzuri ya kucheza katika nafasi akihakikisha kuwa kila wakati anasimama maeneo yanayoweza kutoa ulinzi wa ziada kwa mabeki wa kati.

Ana uwezo wa kupunguza presha kwa mabeki kwa kuhakikisha mpira haupenyi kiurahisi kuelekea eneo lao, yaani ni Mkata Umeme wa ukweli.

Ukiondoa ubora huo, Abuya ni kiungo mwenye uwezo wa kupanda kutengeneza mashambulizi na wakati mwingine anakaa eneo lake, lakini anahakikisha anatoa pasi sahihi kwa uelekeo wa kutengeneza mashambulizi kwa timu. Sio rahisi pasi yake kupotea njiani.

Ukitaka kuamini hilo mfuatilie awapo na mpira na hata akipoteza pasi ni mwepesi wa kupambana kuitafuta, tofauti na wachezaji wengine wanaocheza eneo hilo.

Pia ana uwezo wa kumiliki mpira na kuuficha.

Tukio zuri ambalo amelifanya kwa usahihi ni mechi ya hivi karibuni Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fountain Gate, naye kuibuka nyota wa mchezo. Alihusika kwa usahihi katika bao lililofungwa na Pacome kwa kutoa pasi safi iliyozaa bao hilo la pili.

Mbali na sifa ya kutoa pasi sahihi, Abuya pia ana uwezo wa kupenya mistari ya ulinzi kwa pasi ndefu au za kati zinazovunja mpangilio wa wapinzani, jambo ambalo lilikuwa pia sifa muhimu ya Aucho.


NIDHAMU UWANJANI

Aucho tangu amejiunga na Yanga, licha ya kucheza kwa misimu minne kwa ubora akiwa muhimili wa kikosi hicho eneo la kiungo hakuwahi kupata tuzo hata moja hadi alipohama kwenda Singida Black Stars, ambapo ameshanyakua tuzo moja.

Kwa upande wa Abuya, ambaye msimu huu ndio amekuwa na uhakika wa kikosi cha kwanza tofauti na msimu uliopita alikokuwa akipokezana na Mudathir kucheza sambamba na Aucho, ameonyesha utofauti na huenda akatwaa tuzo nyingi kwani ana nidhamu uwanjani.

Aucho ubora wake uwanjani na kukosa kwake tuzo ilikuwa inatajwa kuwa nidhamu alikuwa ni mtu wa kucheza rafu mara kwa mara. Hiki ni tofauti kwa Abuya anayetajwa kwa ubora na nidhamu nje na ndani ya uwanja.


HANA PRESHA

Moja ya sifa zinazompa thamani kubwa Abuya kikosini Yanga ni uwezo wa kutulia na kucheza mpira akiwa chini ya presha kubwa kutoka kwa wapinzani. Ni kiungo asiyepoteza mpira kirahisi hata anapobanwa na wachezaji wawili au watatu, badala yake hutumia ujanja wa mwili na maamuzi ya haraka kukwepa presha na kutafuta njia salama ya kupitisha mpira.

Utulivu huu humfanya kuwa mhimili wa kupitisha mashambulizi, kwani mara nyingi hugeuza hali ngumu kuwa shambulio la faida kwa Yanga. Zaidi ya hapo, ujasiri wake wa kupokea mpira maeneo hatari bila woga unawasaidia mabeki na viungo wenzake, kwani wanajua mpira ukifika kwake hautapotea.

Uchezaji wake chini ya presha ndio moja ya sababu zinazomfanya aonekane kama kiungo aliyekomaa na anayefaa mifumo mbalimbali ya kisasa ya soka. Abuya anajulikana kwa uwezo wa kusukuma mpira kutoka kiungo kwenda mbele bila kupoteza utulivu.

Hii umsaidia kuvunja presha ya wapinzani na kuanzisha mashambulizi ya Yanga. Ni mchezaji anayefanya kazi kubwa kwa ufanisi; anakimbia bila kuchoka, anarudi kusaidia ulinzi na pia anasukuma timu kupiga mashambulizi.


KUCHEZA NAFASI NYINGI

Yanga ilimsajili Abuya akitokea Ihefu (sasa Singida Black Stars) na uongozi haukuwa na uhakika kama ataweza kuisaidia timu hiyo na walikuwa wanamnasa akatumike eneo la winga na inaelezwa endapo asingetua Jangwani basi angeenda kuitumikia Coastal Union ya Tanga.

Licha ya kumnasa wakiamini ni chaguo sahihi kucheza winga, mambo yamebadilika na moja ya sifa zinazomtofautisha Abuya ndani ya kikosi cha Yanga ni uwezo mkubwa wa kucheza nafasi mbalimbali katika eneo la kiungo.

Ni mchezaji anayebadilika kulingana na mahitaji ya mchezo, jambo linalomfanya awe hazina kwa mfumo wa timu. Abuya anaweza kucheza kama kiungo wa kati akitawala mchezo kwa kasi na utulivu, anaweza pia kucheza kama kiungo mshambuliaji pale Yanga wanapohitaji ubunifu na pasi za mwisho na mara nyingi hutumika kama kiungo wa box-to-box akifanya kazi mbili: kusukuma mashambulizi na kurudi kuzuia.

Kadri mchezo unavyobadilika ndivyo naye anavyobadilika, akitoa ufanisi sawa bila kupoteza muunganiko wa timu. Uwezo huu wa kubadilika ndio unaomfanya kuwa tofauti na Aucho na kuongeza kuwa nguzo imara akisaidiana na Mudathir Yahya katika kiungo cha Yanga.


HACHOKI KIRAHISI

Abuya ni miongoni mwa wachezaji wachache wanaocheza eneo la kiungo wanaojulikana kwa kufanya kazi kubwa uwanjani bila kupunguza kasi hata dakika moja.

Ana injini ya kipekee inayomwezesha kukimbia maeneo makubwa, kufunga mianya, kushambulia na kurudi kujilinda kwa ufanisi. Mara nyingi ndiye mchezaji wa kwanza kuanza presha kwa wapinzani na wa mwisho kuacha kukimbia wakati timu inahitaji kupunguza hatari.

Tofauti na Aucho, ambaye ubora wake ulikuwa ni wa maeneo machache kutuliza timu na kutoa pasi za uhakika, hakuwa anakimbia eneo kubwa uwanjani. Kwa upande wa Abuya, juu unamuona na chini anaonekana na kufanya kazi kwa usahihi.

Kazi yake hii isiyokoma ndiyo inawasaidia Yanga kudhibiti mpira, kuongoza kasi ya mchezo na kuweka uwiano kati ya ulinzi na mashambulizi. Ni mchezaji ambaye hata kama hatengenezi goli au pasi ya moja kwa moja, mchango wake katika kugombea mpira, kupokonya, kufunga njia za wapinzani na kuongoza ulinzi huifanya timu ibaki imara kwa dakika zote 90.