Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Achana na CAF tuishangae kamati ya Masaa 72


DUNIA nzima imepigwa na butwaa baada ya Kamati ya Rufaa ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), kuivua Senegal ubingwa wa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) na kuipa Morocco ambayo ilikata rufaa kudai kuwa inastahili kuvishwa ubingwa huo kutokana na kitendo cha wapinzani wao hao kutoka Afrika Magharibi.


Katika mechi hiyo, awali wachezaji wa Senegal walipinga uamuzi wa refa kuipa Morocco penalti katika dakika ya mwisho jijini Rabat, Morocco katika fainali kwa kuamua kutoka uwanjani wakishawishiwa na kocha wao.

Lakini, nyota na nahodha wa Senegal, Sadio Mane alionyesha uanamichezo kwa kutoungana na wachezaji wengine kutoka uwanjani kugomea uamuzi huo wa refa na badala yake akajitahidi kufanya ushawishi ili wenzake warejee uwanjani, jambo ambalo alilifanikisha baada ya takriban kati ya dakika 15 hadi 17.

Refa akaamuru mchezo uendelee kwa mshambuliaji wa Real Madrid, Brahim Diaz kupiga penalti. Hata hivyo, Diaz hakufanikiwa kuipatia Morocco bao baada ya mbwembwe za upigaji wake kwa stahili ya panenka, kuupeleka mpira alipokuwa amesimama kipa wa Senegal na hivyo kumrahisishia kuudaka.

Hatimaye mechi iliisha kwa sare ya bila kufungana na Senegal ikapata bao pekee katika muda wa nyongeza na hivyo kutwaa ubingwa wa AFCON 2025, hivyo kukabidhiwa taji hilo kubwa katika mashindano ya soka ya Bara la Afrika.

Hata hivyo, Morocco ilikata rufaa ikidai kuwa kitendo cha wachezaji wa Senegal kutoka uwanjani na kukaa nje kwa takriban dakika 15 hadi 17 kilikiuka kanuni ya 82 ya sheria za soka kwamba timu inayotoka uwanjani bila ridhaa ya mwamuzi inakiuka kanuni na hivyo inastahili adhabu inayotolewa katika sheria ya 84 kwamba iondolewe mashindanoni, ipokwe pointi na matokeo kutambuliwa kuwa ni ushindi wa mabao 3-0 kwa timu iliyosalia uwanjani.

Kamati ya Rufaa ya CAF, ilikubaliana na hoja za Morocco na hivyo kutangaza kuivua ubingwa Senegal, jambo ambalo limekuwa kituko cha mwaka katika ulimwengu wa soka ambao unahoji inakuwaje kanuni kuu ya mpira wa miguu ya kwamba refa ndio mwamuzi wa mwisho ikiukwe?

Yaani refa wa fainali hiyo hakuvunja mchezo baada ya wachezaji wa Senegal kutoka uwanjani na waliporudi aliruhusu mchezo kuendelea. Hao waliotoka uwanjani bila ya kurudi na pasipo ridhaa ya refa ni wachezaji wa timu gani?

Kama refa alisubiri hadi wachezaji wa Senegal waliporejea uwanjani na kuendelea na mchezo hadi kumaliza dakika 90 na baadaye 120, huyo aliyetafsiri kuwa mchezo ulivunjika kabla alichezesha mechi gani iliyokuwa na kombe uwanjani?

Kwamba mamlaka ya mwisho kwenye dakika tisini yanaweza kuamuliwa na watu wengine mezani na si mwamuzi wa kati?

Pamoja na kwamba suala hili bado halijafikia mwisho baada ya Senegal kusema itakata rufaa Mahakama ya Kimataifa ya Michezo (CAS), ukweli kwamba uamuzi huo unapingwa kila kona si tu ya Afrika, bali na dunia kwa ujumla, hauna budi kutuzindua sisi tunaosimamia na kuratibu mpira wa miguu katika ngazi mbalimbali kuanzia kimataifa, kitaifa, kimkoa na wilaya.

Sheria kuu ya mpira wa miguu ni kumpa mamlaka ya mwisho mwamuzi wa kati. Kwamba ndiye atakayewabika na lolote linalotokea uwanjani. Tafsiri yake ya sheria katika tukio lolote ndiyo inayotamalaki. Na ikitokea kwamba ameshindwa kutekeleza wajibu wake kadri ilivyotakiwa, refa ndiye anayetakiwa kuwajibika ama kwa kuadhibiwa au kwa yeye mwenyewe kutambua kosa lake na kujiwajibisha ama kwa kukiri kosa na kuomba radhi au kujiengua kwenye kazi hiyo (ingawaje hili ni gumu kwa jamii zetu).

Pamoja na maneno kusambaa kuwa refa alikuwa akipata maelekezo kutoka kwa baadhi ya viongozi wa CAF kuwa asivunje mchezo na kuwasubiri wachezaji wa Senegal warejee uwanjani wakijua kuwa Diaz angeipa ushindi Morocco kwa mkwaju wa penati, kitaalamu inawezekana kabisa kuwa mwamuzi alijua angesimamia tafsiri gani ya sheria.

Hoja zote za wachezaji wa zamani, wa sasa kama Hakim Ziyech, makocha na wanahabari zimejikita katika mamlaka ya refa kuwa ya mwisho kwa jambo lolote linalotokea ndani ya dakika tisini na ndio maana Kamati ya Nidhamu ya CAF ilikutana na kuhangaikia zaidi masuala ya nidhamu yaliyojitokeza na kuadhibu, huku matokeo yakibakia yaleyale ya uwanjani.

Bila ya hata kujua hatima ya ubingwa wa AFCON 2025, kelele zinazopigwa kupinga uamuzi wa Kamati ya Rufaa ya CAF zinatosha kutustua huku Tanzania katika mienendo yetu ya maamuzi yanayofanywa na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi (Kamati ya Saa 72), ambayo hivi sasa imefikia hatua ya kufanya maamuzi kwa matukio ambayo refa hakuyaadhibu.

Kamati imefikia hatua ya kuadhibu hata rafu ambazo refa aliziona na kuziachia ama hakuziona kabisa, jambo ambalo kimsingi halitakiwi liamuliwe na mtu mwingine zaidi ya refa wa kati. Kamati imefikia hatua ya kuadhibu hata mchezaji ambaye inadhani vitendo vyake ni vya kupoteza muda wakati refa hakutafsiri hivyo na hakuadhibu.

Maamuzi hayo ni sawa nay a Kamati ya Rufaa ya CAF ambayo yanapingwa dunia nzima. Timu inaweza kupokwa ushindi kama tu itabainika kuwa ilimchezesha mchezaji ambaye kisheria hakustahili (ineligible player) au ikabainika kuwa rushwa ilitumika kushawishi ushindi, lakini si tafsiri au makosa ya mwamuzi.

Ndio maana dunia inahangaika kubuni teknolojia zitakazomrahisishia refa kufanya uamuzi sahihi kwa kuwa uamuzi wake ndio wa mwisho na kosa moja laweza kuathiri mwenendo mzima wa timu kagtika msimu mmoja.

Kwa hiyo tusiishangae Kamati ya Rufaa ya CAF kwa kuamua kuivua ubingwa Senegal, uamuzi ambao utapinduliwa wakati wowote, bali tujishangae kwa jinsi mwenendo wa Kamati ya Saa 72 unavyopora mamlaka ya refa.

Kadri inavyofanya uamuzi ndivyo watu wanavyozidi kulinganisha matukio na kutuhumu kuwa kuna njama za kuibeba klabu moja. Hii ikizidi ndipo mpira unafikia hatua ya timu moja kugomea mchezo muhimu uliokusanyisha wazito kutoka pande mbalimbali za nchi na kufedhehesha mchezo mzima.

Ni muhimu sana Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB) wakajifunza kitu kutokana na kituko hicho cha CAF kwa kuwa kinaweza kuwa na athari katika mashindano yajayo ya Afrika, kiasi cha kuwepo na uwezekano wa kupoteza msisimko.

Kama tuhuma zilivyokuwa dhidi ya Morocco tangu hatua za awali za AFCON 2025, tayari kelele kama hizo zipo hapa Tanzania ambako kuna madai kuwa mamlaka zinataka kuibeba timu moja kuwa bingwa na tayari tunaona mechi zinavyokuwa za kukaniana kiasi cha kutokuwa za ushindani wa kiufundi.

Zaidi ya hayo, tuhuma zimekuwa zikitolewa waziwazi dhidi ya mamlaka na waamuzi, lakini kinachofanyika ni kuadhibu waamuzi, wachezaji na viongozi na si kushughulika na tatizo kabla ya kuathiri ligi nzima. Hii haifai iachwe iendelee.

Lililo kuu ni kwamba “maoni ya refa” ndani ya dakika 90 ndiyo ya mwisho na ndiyo yanaamua matokeo ya mchezo. Sasa kabla ya kufika hatua hiyo ya kupindua matokeo, ni vizuri tuanze sasa kujidhibiti kutoingilia mamlaka ya refa. Kama refa hajaona faulo na kasoro yake kubwa ni hiyo, basi aadhibiwe ka njia ambayo itamfanya awe bora zaidi na si kumpumzisha kwa muda kisha kurejea akiwa yuleyule.

Kwa hiyo, badala ya kuishangaa Kamati ya Rufaa ya CAF, tutafakari maamuzi ya vyombo vyetu yanayoingiliana na mamlaka ya mwisho ya refa uwanjani. Tujihadhari!