Prime
Aibu ya Kamati ya Tuzo inaposahau kumchagua nyota bora wa mechi
JUMAMOSI ya Novemba 29 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi ilipigwa mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Mtibwa Sugar na TRA United.
Wenyeji Mtibwa Sugar wakashinda kwa 2-1 wakipindua meza kibabe kutoka nyuma baada ya kutanguliwa kwa bao 1-0.
Kwa utaratibu wa kikanuni, kila mchezo wa Ligi Kuu huwa na tuzo ya Nyota wa Mechi, lakini haikuwa hivyo kwa mechi hii.
Baada ya mwamuzi kumaliza pambano hilo, wadhamini NBC wakaja na tuzo yao, lakini hakukuwa na watu wanaohusika na kusimamia zoezi hilo.
Yaani hakukuwa na jopo la wataalamu wa kuchagua mchezaji bora wala watu wa kuratibu zoezi zima.
Kwa hiyo hakupatikana mchezaji bora wa mechi.
Hii ni kashfa na aibu kubwa sana kwa wasimamizi wa mpira wetu, Bodi ya Ligi na TFF.
Mbaya zaidi tukio hili lilikuja siku ambayo uchaguzi wa kumpata mwenyekiti mpya wa bodi hiyo ulifanyika.
Sasa sijui ni kwamba Watendaji wa Bodi na TFF 'walikuwa bize' na uchaguzi na kuipotezea mechi?
Matatizo haya ya tuzo hayajaanza leo katika mpira wetu.
Mwaka 2018 katika fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (sasa CRDB) kati ya Mtibwa na Singida United, hali ilikuwa hivi hivi pale jijini Arusha.
Msimu wa 2023/24 hadi ligi inaingia duru la pili, Bodi ya Ligi walikuwa hawajatoa hata mara moja zawadi ya mwezi kwa washindi wa tuzo za mwezi.
Washindi wenyewe walikuwa kama ifuatavyo:
Agosti
Kocha Bora: Gamondi - Yanga
Mchezaji Bora: Maxi Nzengeli - Yanga
Septemba
Kocha Bora: Abdihamid Moallin - KMC
Mchezaji Bora: Waziri Junior - KMC
Oktoba
Kocha Bora: Robertinho - Simba
Mchezaji Bora: Aziz Ki - Yanga
Novemba
Kocha Bora: Bruno Ferry - Azam FC
Mchezaji Bora: Feisal Salum - Azam FC
Desemba
Kocha Bora: Bruno Ferry - Azam FC
Mchezaji Bora: Kipre Jr. - Azam FC
Unaposoma makala hii 2025, zawadi hizi hazikuwahi kutolewa tangu wakati ule hadi sasa.
Kwa kifupi ni kwamba washindi wa tuzo ilikula kwao.
Tuzo hizi ambazo husimamiwa na kamati ya tuzo ya TFF, hudhaminiwa na wadhamini wa Ligi Kuu, Benki ya NBC na Azam TV.
Ni aibu kwa TFF, Bodi ya Ligi na wadhamini kushindwa kuzipa heshima tuzo hizi.
Hii inakuja wakati Tanzania ilitoka kutwaa ubingwa wa CECAFA chini ya miaka 17.
Ubingwa wa aina hii unarudisha mjadala wa pesa za zawadi kwa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 15 mwaka 2023.
Desemba mwaka huo iliibuka taarifa ya chini chini ya TFF kuchikichia zawadi ya Sh188 milioni ya timu ya taifa chini ya miaka 15, waliyopata baada ya kushika nafasi ya pili kwenye mashindano ya CECAFA.
Taarifa hii iliyoanza kama tetesi kupitia mitandao ya jamii, ilikuja kuthibitishwa Rais wa TFF, Wallace Karia, aliposema kwamba fedha hizo zitatumika kujengea miundombinu.
Raia Karia alitoa ufafanuzi huo baada ya presha kubwa sana kutoka kila kona ya nchi kufuatia baadhi ya wachezaji kufichua siri.
Bila hivyo TFF isingesema chochote.
TFF hiyo ndiyo hii ambayo kamati yake inasimamia hizi tuzo na kuja na haya mazongi...na ambayo hadi sasa haijatoa tuzo za msimu uliopita.
Ukiacha tuzo za mwezi, tuzo za mwaka ndiyo kizunguzungu zaidi.
Washindi wengine husababisha watu wanaoangalia tuzo waone aibu kama wao ndiyo walichagua.
Msimu 2022/23, walimpa Clement Mzize wa Yanga tuzo ya mchezaji bora wa U20.
Hii ilikuwa ajabu sana kwa sababu Mzize hakushiriki ligi ya vijana chini ya miaka 20 msimu uliopita, yeye alishiriki msimu wa nyuma yake.
Mchezaji bora wa U20 alikuwa Ladack Chasambi wa Mtibwa Sugar na alitangazwa baada ya mashindano pale Chamazi.
Sasa kamati yenye madudu kama haya inapokutana na TFF yenye madudu yale ya juu, lazima kutakuwa na kasoro nyingi.
Na madudu yenyewe ndio kama haya, mechi imechezwa, lakini hakuna watu wa kuchagua mchezaji bora wa mechi.
Mwezi unapita, zawadi za mchezaji bora wa mwezi hakuna.
Na msimu unaisha, tuzo kwa wachezaji bora hakuna.
Hili ni tatizo kubwa sana...ni donda ndugu kabisa...ni tatizo sugu.
Msimu wa 2017/18 Seif Rashid Karihe wa Lipuli alipewa tuzo ya mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports (sasa CRDB), kwa mabao yake manne.
Lakini hata hivyo, hakuwa Karihe peke yake aliyefunga mabao 4.
Heritier Makambo na Amissi Tambwe wa Yanga, pia walifunga mabao 4 kila mmoja.
Lakini hawakupata tuzo...akapewa tuzo mtu mmoja ilhali wapo wengine kama yeye.
Kosa kama hili lilifanyika katika msimu wa kwanza wa mashindano, 2015/16.
Atupele Green wa Ndanda FC aliyekuwa na mabao 5 alipewa tuzo ya mfungaji bora.
Hata hivyo, hakuwa peke yake mwenye idadi hiyo, hata Hamis Kiiza wa Simba naye alifunga mabao 5.
Lakini TFF, kupitia Ofisa Mashindano wake wa wakati ule, Jemedari Said, ilisema rekodi walizokuwa nazo wao ni za Atupele tu, za Kiiza hawana.
Waandaaji wa mashindano hawana rekodi za mashindano yao, ambayo yanaonyeshwa kwenye TV na mabao yanaonekana hata YouTube.
Yawezekana ndiyo sababu ya kushindwa kutoa tuzo kama hiyo msimu uliofuata wa 2016/17.
Msimu 2017/18 tuzo ya kipa bora wa mashindano haikutolewa kwa kigezo kwamba hakukuwa na aliyekidhi sifa.
Inawezekanaje tuzo ikose mchezaji mwenye sifa? Kwani sifa huwa ni zipi? Usikute waliweka sifa ambazo siyo za kimpira.
Labda walitaka kipa ambaye anaokoa michomo akiwa nyumbani kwake amelala kitandani.
Usikute hata mechi ya Mtibwa Sugar na TRA United ilikosa mchezaji bora wa mchezo kwa sababu hakukuwa na aliyekidhi vigezo.