Prime
Bao safi la Chama lilivyoficha uchafu wa watani
Muktasari:
- Hiki ndicho kilichotokea kwa mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga, Mei 3, mwaka huu pale dimbani Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.
WASWAHILI husema umaridadi huficha umasikini. Ukiwa nadhifu yaani unavaa vizuri watu hawatajua dhiki uliyoibeba nafsini mwako.
Hiki ndicho kilichotokea kwa mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga, Mei 3, mwaka huu pale dimbani Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.
Nyota wa Simba, Clatous Chota Chama alifunga moja ya mabao mazuri zaidi katika historia ya mpira, sio tu wa Tanzania, bali duniani kote.
Mabao kama yale ni nadra sana kufungwa, na inapotokea likafungwa, basi lazima lizungumzwe sana. Bao la Chama limezungumzwa dunia nzima na kuufanya mpira wa Tanzania utajwe kwa uzuri na kuficha mambo yote mabaya yaliyogubika mechi hiyo.
Bao la lile linafanana na la Wendell Lira wa Klabu ya Goianesia ya Brazil alilofunga dhidi ya Atletico Goianiense kwenye ligi ya kanda nchini humo. Bao hilo lilishinda tuzo ya bao bora la Fifa 2015. Pia lililishinda bao la juhudi binafsi la Lionel Messi wa Barcelona dhidi ya Athletic Bilbao kwenye fainali ya Copa del Rey.
Na pia lililishinda bao la umbali wa mita 50 la Alessandro Florenzi wa AS Roma ya Italia alilofunga dhidi ya Barcelona kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Bao la Chama na la Lira yanafanana kila kitu. Aina ya pasi aliyopewa mfungaji na jinsi mfungaji alivyopiga mkasi. Mtangazaji wa Kiingereza wa mechi ya watani, Peter Otai kutoka Uganda alisema, "Chama, scooping deep... Elie Mpanzu with a ball... it's Chama! Oh ho ho! What a goal! Beauty at its best, beauty at its best! Bow down to greatness, bow down to football!. You will never see that again! What a goal! Clatous Chama! Delicious, that's a delicious goal!"
Kwa Kiswahili. "Chama, anaubetulia kwa ndani...Elie Mpanzu na mpira...ni Chaamaa! Oh! Oh! Oh! Bao la aina yake! Ubora katika ubora wake, ubora katika ubora wake! Chutama kwa kilicho bora, chutama kwa mpira. Hutaliona tena. Bao la aina yake. Clatous Chama. Tamu sana. Hilo ni bao tamu sana." Ama kwa hakika bao lile lilikuwa tamu...tamu sana! Bao bora katika wakati bora kwenye mechi bora. Dunia ikaliona na kulisherehekea. Kituo kikubwa cha runinga cha CNN kikalionyesha bao hilo duniani. Dunia ikafurahi. Mechi ya watani wa jadi Tanzania ikatawala dunia. Mpira wa Tanzania ukawa gumzo duniani.
Lakini, nyuma ya bao hilo safi kulikuwa na uchafu mwingi ambao dunia haikuuona kwa sababu ya bao la Chama. Picha ilianzia Aprili 24 pale taarifa rasmi ilipotoka kwamba mechi ya watani wa jadi, Mei 3, itachezwa dimbani Meja Jenerali Isamuhyo Isamuhyo pale Mbweni. Tanzania ikaitikia kwa sauti tofauti, wengi wakipinga mchezo huo mkubwa kufanyika kwenye uwanja wa aina ya Meja Jenerali Isamuhyo.
Hoja ilikuwa uwanja huo hauna hadhi ya kubeba tukio kubwa zaidi la soka nchini Tanzania. Mechi ya watani wa jadi ndilo tukio kubwa zaidi la soka nchini. Ni sikukuu ya soka. Kitendo cha kulipeleka tukio hilo kwenye uwanja kama ule hakikupokewa vizuri na wengi kasoro Simba wenyewe ambao walikuwa wenyeji wa mchezo. Mjadala wa uwanja ukaendelea na ilipofika Mei 2 ukapata sura mpya.
Wageni Yanga wakaenda kufanya mazoezi ya mwisho na kurekodi video nyingi zikionyesha upungufu katika uwanja. Mjadala ukaibuka upya kwamba uwanja ule sio rafiki kwa mchezo wa ukubwa wa watani wa jadi. Lakini siku ya mchezo ndio ilikuwa balaa. Yanga walipofika eneo la tukio hawakwenda vyumba vya kuvalia uwanjani. Wakaingia nyumba binafsi iliyopo pembeni ya uwanja.
Hiki ni kitendo cha aibu kuliko hata mechi kuchezwa kwenye uwanja ule. Yanga walionyesha kwamba wanaishi karne ya 19 katika wakati huu wa karne ya 21. Bila aibu, bila kusita wameingia nyumba ya jirani. Maana yake walikaa kikao na kupanga iwe hivyo, aibu kubwa. Ukafika muda wa timu kupasha misuli joto kabla ya kuanza kwa mtanange.
Kisha alionekana mtu mmoja akiingia uwanjani akimwaga maji kuelekea golini. Imani za ushirikina. Ukafika wakati wa mchezo wenyewe.
Kweli, uwanja ulijaa tope na kufanya boli lisitembee vizuri kwenye nyasi. Wachezaji walipoanguka uwanjani au kulala yombo kucheza mpira waliishia 'kuogelea' kwenye tope na kuchafuka. Bahati nzuri ni kwamba Chama alifunga bao lile mapema kabisa kabla uwanja haujaharibika sana. Kabla jezi hazijachafuka sana. Bila hivyo, kwa namna alivyoruka sarakasi na kufunga angeinuka akiwa amejaa tope na kuonekana akishangilia akiwa mchafu.
ISITOKEE TENA
Mechi ya watani wa jadi ndio kubwa zaidi nchini na inatakiwa kuchezwa kwenye uwanja bora. Hii ndio alama ya mpira wetu na ndio kioo cha mpira. Haipaswi kuchezwa tu ilimradi ichezwe, hapana. Isitokee tena mechi hiyo kuchezwa kwenye uwanja wa hadhi chini ya ukubwa wa mchezo.
Lakini, zaidi ya hapo, isitokee tena mambo ya aibu kama yaliyofanywa na Yanga. Kitendo cha kufikia moja kwa moja nyumba ya jirani ni makosa makubwa. Ni aibu kubwa. Kitendo cha yule mtu kupita katikati ya uwanja akimwaga maji ni aibu kubwa.
Leo Chama katufichia aibu. Tunashangilia CNN kuonyesha bao la Chama. Vipi siku CNN wakimuonyesha kiongozi mkubwa wa klabu akiiongoza timu yake kuingia nyumba ya jirani badala ya vyumba vya kuvalia pale uwanjani? Vipi CNN wakimuonyesha mtu anamwaga maji katikati ya uwanja? Hali hii idhibitiwe, isitokee tena!