Bingwa wa mdomo mkubwa aenziwa kitaifa
Muktasari:
- Lakini tangu zama za kale wamejitokeza watu waliotumia miili yao, akili zao au juhudi za aina moja au nyingine kujitafutia riziki za maisha na hata kuwa matajiri waliotambulika katika nchi zao na nje.
Siku hizi jamii inashuhudia kila aina ya utapeli, kwa wajanja kutumia mbinu za kila aina za kuhadaa watu na kupata fedha, nyumba, shamba au kitu chochote kile cha thamani.
Lakini tangu zama za kale wamejitokeza watu waliotumia miili yao, akili zao au juhudi za aina moja au nyingine kujitafutia riziki za maisha na hata kuwa matajiri waliotambulika katika nchi zao na nje.
Miongoni mwa njia zilizozoeleka katika michezo ni kuvumbua aina mpya ya mchezo au maonyesho ambayo huvutia watu na anayefanya kujipatia kitita kikubwa cha fedha. Tumeona kila kukicha binadamu akivumbua michezo ya aina mbalimbali ili sio tu kuupa mwili mazoezi kwa ajili ya kuimarisha afya yake au kupata burudani, bali pia kupata pesa.
Tumeona michezo ya hatari kama ya kucheza na papa baharini, wanyama wakali, kuogelea kwenye maji ya baridi kali au ya moto, mbio na mpira kwenye matope, kwenye barafu, msituni na milimani au watu kushindana mbio wakiwa wamebeba wake au waume zao.
Siku hizi watu wasioona wanacheza kandanda, kriketi na hata kurusha mishale.
Mpaka leo upo mchezo uliowashangaza wengi alivyouvumbua raia wa Angola, Francisco Domingo Joaquim, ambaye alifariki mapema mwaka 2023 kutokana na kuugua saratani ya mapafu akiwa na miaka 31.
Ameacha rekodi ya dunia ya aina yake ya kuwa na mdomo mkubwa wenye upana wa sentimita 17 ambao haujavunjwa, lakini kubwa zaidi ni mambo aliyoyafanya kwa kutumia huo mdomo na kuwashangaza watazamaji kila alipofanya maonyesho.
Hivi karibuni palifanyika kumbukumbu maalum katika jiji la Luanda iliyokuwa na maelezo ya maisha ya raia huyu wa Angola ambaye aliitangaza nchi yake kila pembe ya dunia kwa vituko vyake vya kutumia mdomo wake mkubwa.
Mdomo huu mpana aliokuwa nao Francisco ulitokana na matatizo aliyokuwa nayo ya mishipa dhaifu ya eneo linalouzunguka mdomo, mashavu na kidevu chake.
Huyu jamaa aliugeuza ulemavu wake wa mdomo kuwa kitega uchumi ambacho kilimpelekea kuwa na maisha mazuri, ya raha na furaha mpaka pale maradhi ya saratani yaliposababisha kifo chake. Alipotembelea Ulaya alimtoza mtu aliyetaka kupiga naye picha kati ya dola za Kimarekani 30 (shilingi 80,000) hadi dola 100 (shilingi 270,000) na aliyetaka hiyo picha iwe anampiga busu alilazimika kulipa zaidi.
Alishinda mashindano yote ya kutafuta watu wenye midomo mipana na kufanya mambo yasiyo ya kawaida kwa kutumia mdomo.
Ushindi wake wa kwanza ulikuwa mwaka 2010 akiwa na miaka 20, alipoonyesha utaalamu wa kuchezea mdomo wake katika mashindano ya kimataifa ya Domo Kubwa (Big Mouth) yaliyofanyika Rome, Italia.
Francisco aliyejulikana zaidi kama Taya wa Angola alitia mdomoni na kukichezesha kikopo cha soda bila ya matatizo.
Katika mashindano ya Rome, wakati wenzake walichukua vipande viwili au vitatu vya keki kutia mdomoni, yeye alikusanya vipande 10 na kutia mdomoni gilasi na vikombe bila ya matatizo. Vituo vya runinga vya Italia na nchi nyingine za Ulaya vilimualika kwa donge nono kufanya maonyesho na kampuni nyingi zilimwita kufanya maonyesho na kutoza fedha wanaopanda kwenye jukwaa kucheza naye au kupigwa busu. Kila busu moja lilikuwa na ada yake na ukimpiga mabusu matatu basi ulilipa mara tatu na ukiwa na bahati ulipunguziwa kidogo malipo.
Moja ya rekodi zake maarufu ni kutia mdomoni na kutoa mara 14 kopo la soda kwa muda wa dakika moja. Mara nyingi alifanya maonyesho kupitia vituo vya runinga vya Luanda, kumbi mbalimbali na barabarani na kurudi nyumbani na kitita cha fedha. Alikuwa akisema: “Wakati serikali ya Angola inategemea mafuta kujiendesha, mimi nategemea mdomo wangu.”
Katika mahojiano aliyoyafanya wiki chache kabla ya hali yake kuwa mbaya alisema alifurahia maradhi aliyokuwa nayo ambayo yalipelekea mdomo wake kuwa mkubwa sana kwani angekuwa na mdomo mdogo au wa kawaida angekuwa na maisha ya shida kama vijana wengi wanavyotapatapa kutafuta kazi katika jiji la Luanda na kwingine. Aliwataka watu wenye ulemavu wa aina moja au nyingine kutokata tamaa kwa vile ni walemavu, bali wanaweza kutumia hali waliyonayo kujitafutia maisha bora.
“Kila kiungo cha mwili kinaweza kuwa kitega uchumi. Lililo muhimu ni kufikiria unaweza kukitumia vipi,” alisema. Hivi sasa kila mwaka hufanyika maonyesho Angola kumkumbuka Francisco ambaye mpaka sasa ndiye raia pekee wa Angola ambaye jina lake limeingia katika kitabu maarufu cha Guinness kinachoweka rekodi mbalimbali za dunia.
Labda na hapa Tanzania ipo siku tutafanya mashindano ya watu wenye midomo mikubwa au midogo. Sio vibaya kwa wale wanaojiona wanayo midomo mikubwa au midogo sana wakaanza kujipanga ili mashindano ya aina hii yakianza waweze kushiriki vizuri.
Kama ilivyokuwa mwishoni mwa miaka ya tisini ambako lifanyika shindano la mtu mwenye sura mbaya na marehemu Sultan Masoud ‘Masuod Surambaya’ alishindi akifuatiwa na marehemu Dkt. Remmy Ongala na nafasi ya tatu ilikwenda kwa Mzee Jangala.