Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Clatous Chama kwa nini amerudi nyumbani

JICHO Pict


WASWAHILI na uswahili wao waliwahi kusema 'mwenda tezi na omo marejeo ngamani'. Inawezekana imemkuta Clatous Chotta Chama. Kama utaniuliza maana ya msemo huo, nitakwambia tu inamaanisha 'zunguka unavyoweza, lakini utarudi nyumbani'.


Imemkuta Chama. Hatimaye amerudi nyumbani. Simba. Timu ambayo ilimleta nchini. Ikampaisha. Tusisahau naye aliipaisha vile vile. Simba ya Chama na Chama wa Simba vyote vilikuwa juu. Walipelekana hewani. Wakapata mafanikio ndani na nje ya nchi. Baadae uhusiano wao ukawa wa mashaka kwa kiasi kikubwa. Kuna 'kidudu mtu' aliingilia kati penzi lao. Yanga.


Chama akashutumiwa sana alikuwa anatumika na upande wa pili. Na katika moja kati ya ndoto kubwa ya upande wa pili, licha ya kuwa na kikosi kabambe katika miaka ya karibuni, ilikuwa ni kumpata Chama. Kusudio la kwanza ilikuwa ni kuwaumiza watani. Kusudio la pili ilikuwa ni kuimarisha kikosi katika ubunifu wa eneo la mbele.

Picha ya kwanza ya Chama pale Kigamboni ilitushtua sana. Chama akiwa na Pacome pamoja na Aziz Ki. Ndoto inayotisha. Hata hivyo, baada ya hapo maisha hayakwenda kama yalivyofikiriwa. Wakati ikidhaniwa Chama alikuwa anaenda kupumzisha ufalme wa mmoja wao kati ya Aziz na Pacome ni yeye ndiye ambaye alijikuta akipumzishwa benchi kwa muda mrefu.

CHAM 01

Ilisemwa Chama hakuendana na kasi ya Yanga. Hakuendana na ujana wa Aziz na Pacome pamoja na yule Mcongo, Maxi Nzingeli ambaye huwa anaichezea Yanga kama vile aliweka jiwe la ufunguzi wa jengo la Yanga. Makocha wawili walipita Yanga, huku Chama akiwa mchezaji anayetumia muda mwingi katika benchi kuliko katika nyasi.

Mashabiki wa Yanga walijitahidi kwa kadri walivyoweza kumrudisha uwanjani kiakili. Mashabiki wa Simba wakiongozwa na msemaji wao walitumia muda huo kuwaonyesha watani wao Chama alikuwa amekwenda Yanga kufuata pensheni. Haukuwa muda mzuri katika maisha ya soka ya Chama.

Baadae ilionekana kama vile Yanga walikuwa wamemvuta Chama katika klabu yao kwa ajili ya kumdhalilisha. Kwamba alikuwa mfalme sana Simba, lakini katika timu yao alikuwa mchezaji wa kawaida tu. Chama hakuwa na nyakati nzuri Yanga. Hakuwahi kuacha alama. Ni tofauti na maisha yake Msimbazi.

CHAM 02

Kushindilia msumari wa mwisho wa kipindi kibaya cha Chama Yanga, Injinia Hersi Said na watu wake waliamua kutomwongezea mkataba mpya. Awali walikuwa wamempa mkataba wa mwaka mmoja tu. Usingeweza kumlaumu Injinia kwa sababu Chama hakuacha alama Yanga, lakini tayari alikuwa na wachezaji wake ambao walikuwa msingi wa timu. Kina Pacome na Maxi.

Chama akaishia zake Singida Black Stars. Haikufikirika siku moja Chama yule ambaye aliiteka Tanzania angeweza kucheza katika timu iliyokuwa mbele kidogo ya Wilaya ya Manyoni. Haikufikirika lakini ilitokea. Ilionekana kuwa mwanzo wa mwisho wake. Kwa nini Simba hawakumchukua moja kwa moja wakati Yanga walipoamua kutomuongezea mkataba dirisha kubwa lililopita? Nitakupa jibu.

Simba walihisi kuchekwa na watani. Kwamba ingeonekana mchezaji ambaye alikuwa staa mkubwa kwao alikwenda kwa mtani na ameonekana mchezaji wa kawaida tu. Kwamba ingeonekana viwango (standards) za mtani zipo juu kuliko wao. Lakini hapo hapo kuna jambo moja ambalo Simba walilikumbuka zaidi.

CHAM 03

Walikumbuka Chama alikuwa msaliti. Kuanzia maisha yake Msimbazi. Kwamba alikuwa hachezi vema mechi dhidi ya mtani. Lakini akaamua kuhamia kwa mtani kabisa. Ni kitu ambacho kilivunja mioyo ya mashabiki na mabosi wa Msimbazi. Kwamba walichokuwa wanakifikiria kuwa Chama alikuwa 'anatumika' lilikuwa jambo la kweli kwa sababu aliamua kuhamia rasmi mitaa ya Twiga na Jangwani.

Hata hivyo, pamoja na yote haya mwishowe Simba wameamua kunyoosha mikono juu kwa mwamba wa Lusaka. Licha ya kila kitu ambacho kimetokea baina yao na Chama wameamua ni bora ambaye umri umeenda kuliko Joshua Mutale aliye kijana. Bora ya Chama ambaye atacheza kwa asilimia hamsini tu ya uwezo wake kuliko Neo Maema atakayecheza kwa asilimia mia moja ya uwezo wake.

Kumekuwa na mgawanyiko wa hisia (mixed feelings) kwa mashabiki kuhusu kurudi kwa Chama Msimbazi, lakini nadhani asilimia ya waliotaka bora Chama imekuwa kubwa kwa sababu Simba walishindwa kupata mbadala wake halisi baada ya kuondoka kwake. Imetokea mara mbili. Wakati ule alipokwenda Morocco kucheza RS Berkane, kisha alipokwenda kwa mtani.

Kina Jean Charles Ahoua wameonekana kuwa na namba nzuri uwanjani, lakini hawajawahi kuwa Chama. Hawajawahi kukaa katika mioyo. Simba ina watu wake ambao waliwahi kukaa katika mioyo ya mashabiki katika miaka ya karibuni. Emmanuel Okwi na Clatous Chama. Hauwaambii kitu watu wa Simba. Inabidi ufanye kazi hasa kuwasahaulisha Simba kuhusu watu hawa.

Ndiyo maana Chama amerudi zake Msimbazi akiwa na umri wa miaka 34. Juni mwaka huu atatimiza miaka 35. Simba wanafahamu Chama huyu sio yule, lakini bora uwe na huyu kuliko kuwa na Mutale ambaye hajui afanye nini akiwa ndani ya boksi la adui. Kuna kundi kubwa la wanachama na mabosi ambao wamesamehe yote yaliyopita kuhusu Chama kuliko kumuona Mutale akikokota mpira kuelekea kwa adui.

CHAM 04

Na sasa Simba na Chama wataheshimiana kwa kiasi kikubwa. Chama amegundua hakuna malisho mema zaidi na heshima kubwa nje ya Simba. Atarudi akiwa na adabu. Naona na Simba nao wametanua misuli yao kwake kiasi kwamba wamemnyima hata jezi yake pendwa namba 17 na sasa atavaa jezi namba 24. Labda kuna sababu za kikanuni zaidi kwa watu wa CAF ndiyo maana juzi alivaa alivaa jezi namba 24 pale Tunisia. Hata hivyo Simba kwa sasa wameshika mpini zaidi.

Haishangazi pia kuona hata wao wamempa Chama mkataba wa mwaka mmoja tu. Zamani ingekuwa miaka mingi zaidi. Ni suala la kusubiri na kuona nini kitafuata. Umri umesogea, lakini anaweza kuvuta muda zaidi kama. Atarudisha asilimia hamsini tu ya uwezo wake ambao kina Kibu Dennis inaonekana walishindwa kuufikia na kuwasahaulisha Wanasimba kuhusu yeye.

Kitu kingine ambacho sipaswi kusahau kuhusu Chama kurudi Simba ni namna alivyorudi Simba katika siku yake ya mwisho. Kumbe alikuwa na tiketi ya kwenda Tunisia mkononi baada ya mechi yake ya mwisho katika jezi ya Singida Black Stars. Alikwenda uwanjani akacheza vema pambano hilo ingawa Singida walipoteza ugenini. Simba wakamtambulisha baadae usiku na alfajiri yake akaenda zake Tunisia.

Shukrani kwa Chama mwenyewe kuiheshimu timu yake ya zamani. Shukrani kwa Simba kwa kufuata matakwa ya Singida ambayo ilimhitaji mchezaji hadi sekunde ya mwisho. Shukrani kwa kila aliyehusika katika kila dili, ingawa mjadala utaendelea baadae namna ambavyo Singida Black Stars inavyoweza kuwaachia mastaa wake kirahisi kwenda Simba na Yanga ingawa na wao wapo vitani.