Dira ya taifa 2050 itakavyokuza michezo kama sekta ya uchumi
Muktasari:
- Katika mwelekeo huo, michezo ina nafasi kubwa ya zaidi ya burudani na sekta muhimu ya uchumi, jambo ambalo kupitia Dira 2050, inatambua uwezo wa kutoa ajira, kukuza vipaji, kuongeza kipato cha vijana na kuimarisha pia utambulisho wa Taifa.
DIRA ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kujenga Tanzania yenye uchumi jumuishi, shindani, unaotegemea maarifa, ubunifu na teknolojia na kuongeza fursa za ajira na ustawi wa wananchi, huku michezo ikiwa na nafasi kubwa zaidi ya burudani.
Katika mwelekeo huo, michezo ina nafasi kubwa ya zaidi ya burudani na sekta muhimu ya uchumi, jambo ambalo kupitia Dira 2050, inatambua uwezo wa kutoa ajira, kukuza vipaji, kuongeza kipato cha vijana na kuimarisha pia utambulisho wa Taifa.
Aidha mpango wa muda mrefu umeweka lengo la kuongeza ushindani wa sekta ya michezo na sanaa bunifu ndani na nje ya nchi, japo ili kwa pamoja tuone tunafikia malengo hayo na kupiga hatua zaidi ni lazima tuzingatia mbinu mbalimbali zifuatazo.
SERA YA UCHUMI WA MICHEZO
Serikali inapaswa kuweka mfumo madhubuti wenye sera inayotambua michezo kama shughuli ya kiuchumi, kwa kuzingatia sekta binafsi, vyama vya michezo, wanamichezo na wawekezaji watakavyoshirikiana, ili kuweka mazingira rahisi pia ya uwekezaji.
Usajili wa biashara za michezo, kodi, udhamini na uendeshaji wa mashindano utasaidia michezo kuondokana na mtazamo wa kutegemea ruzuku pekee na kujikita katika mfumo maalumu utakaozalisha mapato ya kujitegemea na kuchochea uchumi kukua.
MIUNDOMBINU YA KISASA
Miundombinu bora ni msingi wa kujenga sekta ya michezo yenye ushindani na kutokana na Serikali na sekta binafsi, zinaweza kujenga zaidi na kuboresha viwanja, kumbi, mabwawa ya kuogelea, vituo vya mazoezi, akademi na vituo vya tiba na sayansi.
Miundombinu hiyo isitumike kwa mashindano pekee, bali iwe ni vitega uchumi vinavyoweza kuzalisha mapato kutokana na tiketi, matangazo, upangishaji, mikutano na matukio mengine, kwani Dira 2050 inasisitiza kuiwezesha Tanzania kitovu cha michezo.
AKADEMI ZA MICHEZO
Tanzania inapaswa kuwekeza katika akademi zinazogundua na kuendeleza vipaji kuanzia ngazi za shule hadi kiwango cha juu cha kitaifa na kimataifa, huku ikiwa na wakufunzi wenye sifa, wataalamu wa lishe, tiba, saikolojia na mazoezi ya viungo.
Mfumo huu utasaidia kuzalisha wanamichezo bora ambao wanaweza kucheza katika ligi kubwa duniani na hivyo kuingiza fedha nchini kutokana na mishahara, uhamisho wa wachezaji, mikataba ya kibiashara, udhamini na kuongeza ajira kwa makocha nchini.
UTALII WA MICHEZO
Utalii wa michezo unapaswa uwe sehemu ya mkakati wa Taifa wa kuongeza mapato ya kigeni, kwa sababu Tanzania ina uwezo wa kuvutia wageni kupitia marathoni, mashindano ya mpira wa miguu, riadha, ndondi, gofu, baiskeli na michezo ya majini.
Wageni wanapokuja kushiriki au kutazama mashindano mbalimbali hutumia fedha katika hoteli, usafiri, migahawa, burudani na vivutio vya utalii na isitoshe mpango huu wa muda mrefu utavutia zaidi ya watalii 500,000 wa michezo kwa kila mwaka.
USHIRIKIANO WA SERIKALI
Sekta binafsi inapaswa iwe mshirika mkuu katika maendeleo ya michezo, huku kwa upande wa Serikali ikijikita kuweka zaidi mazingira rafiki ya kuwavutia wawekezaji kujenga viwanja, kuanzisha akademi, kuendesha timu na kuandaa pia mashindano.
Kampuni pia zinaweza kushiriki kutokana na udhamini, matangazo na uwekezaji wa moja kwa moja na mfumo huo wa ubia kati ya Serikali na sekta binafsi unaweza ukapunguza utegemezi wa fedha za Serikali na kuongeza ubora wa huduma za michezo.
TEKNOLOJIA KIDIJITALI
Teknolojia inaweza kubadilisha michezo iwe biashara yenye soko kubwa kimataifa na kutokana na mfumo huu, Tanzania ina nafasi zaidi ya kutumia majukwaa ya kidijitali kuuza tiketi, kutangaza mashindano, kuuza bidhaa za timu na kusambaza matangazo.
Takwimu za wanamichezo zinaweza kutumika kuboresha uwezo wao na kuvutia klabu na wawekezaji, huku mitandao ya kijamii ni chanzo cha mapato kutokana na matangazo na maudhui ya michezo, ili kuendana na msisitizo wa Dira 2050, wa kujenga uchumi.
CHAPA YA WANAMICHEZO
Wanamichezo wanapaswa kutazamwa kama chapa zenye thamani ya kibiashara, huku Serikali na taasisi za michezo ziwasaidie kujifunza zaidi kutokana na masoko, mawasiliano, matumizi ya mitandao ya kijamii na kuwasimamia wakati wa kusaini mikataba.
Mwanamichezo anayejulikana kimataifa anaweza akawa balozi wa bidhaa za Tanzania na kuvutia udhamini kutoka kampuni za ndani na nje ya nchi, huku timu pia zinapaswa kujenga chapa zinazoweza kuuza jezi, bidhaa na huduma kwa mashabiki zao.
MASHINDANO KIMATAIFA
Mashindano ya ndani yenye ushindani hujenga soko la michezo kwa sababu ligi mbalimbali zikiwa zinaendeshwa kwa weledi, uwazi na kalenda inayotabirika itasaidia Tanzania kuvutia mashindano ya kikanda na kimataifa na kuongeza zaidi mapato.
Mashindano makubwa huongeza mapato ya tiketi, matangazo, udhamini, utalii na biashara ndogo zinazozunguka matukio hayo na mpango wa muda mrefu utaandaa matukio ya ndani, kikanda na kimataifa kama njia ya kukuza utalii wa michezo nchini.
UWEKEZAJI WA MICHEZO
Changamoto ya upatikanaji wa mitaji inaweza kuzuia ukuaji wa michezo, japo Serikali inapaswa kushirikiana na benki na taasisi za fedha kuanzisha mikopo na mifuko maalumu kwa biashara za michezo na kuhamasisha wawekezaji kupitia vivutio.
Kutokana na vivutio vya kodi na mazingira rafiki ya biashara, itawezesha kuanzishwa kwa kampuni zinazotengeneza vifaa vya michezo, mavazi mbalimbali, programu za kidijitali, huduma za mazoezini na bidhaa nyingine, zitakazochangia uwekezaji.
ELIMU KWA WANAMICHEZO
Elimu ya ujasiriamali, uwekezaji, kodi, mikataba na usimamizi wa fedha inapaswa kuunganishwa katika mafunzo ya michezo, kwa sababu wanamichezo wenye vipaji pekee bila ya uelewa mkubwa wa fedha wanaweza wakashindwa kutumia vizuri mapato yao.
Hatua hii itasaidia kujenga kizazi cha wanamichezo ambao si wazalishaji wa vipaji pekee bali pia wawekezaji, kwa sababu itawasaidia kufundishwa namna nzuri ya kuwekeza mapato ya fedha wanazozipata michezoni na kuanzisha biashara mbalimbali.
UTAWALA BORA
Vyama na taasisi za michezo zinapaswa ziwe na mifumo ya uwajibikaji, uwazi wa fedha, mipango ya muda mrefu na wataalamu wenye sifa na hatua hiyo itasaidia kuona usimamizi mzuri utakaoongeza imani ya serikali, wafadhali na wawekezaji.
Michezo haiwezi ikawa sekta kubwa ya uchumi bila ya uongozi imara na kufikia mwaka 2050 ni lazima kuhakikisha masuala yote yanayohusu utawala bora yanaendana na matakwa ya dira, jambo litakalowezesha kuongezeka kwa mapato ya kimaendeleo.
MAPATO MICHEZONI
Tanzania inapaswa iwe na takwimu sahihi kuhusu mapato ya michezo, ajira, uwekezaji, utalii, kodi, mauzo ya bidhaa na thamani ya sekta, itakayosaidia Serikali kujua ukubwa halisi wa uchumi wa michezo na kupanga uwekezaji mzuri unaofaa.
Pia, Dira 2050 inahitaji mifumo madhubuti ya ufuatiliaji na tathmini ili kuhakikisha malengo ya maendeleo yanatekelezwa ipasavyo, kwa sababu ikiwa itaanzishwa mfumo wa takwimu utasaidia kwa ukaribu kukuza maendeleo na michango ya michezo.
Kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, michezo inapaswa kuonekana injini ya uchumi na sio suala la burudani tu, kwani uwekezaji wa miundombinu, akademi, teknolojia, utalii na chapa za wanamichezo utaongeza ajira na pato la taifa.
Aidha, ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kujenga mfumo wa michezo unaojitegemea na wenye ushindani na sekta zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha zaidi ajira, ubunifu na thamani zinapaswa kupewa kipaumbele.
Dira 2050 imeweka michezo katika mazingira mapana ya mageuzi makubwa na mbinu hizi zikitekelezwa vizuri zitaifanya kwa sasa Tanzania iwe ni kitovu cha kuongeza mapato, kujenga uchumi wa kisasa, jumuishi na wenye ushindani wa kimataifa.