Fei Toto: Sishindani na mtu, nashindana na rekodi zangu
Muktasari:
- Feitoto ambaye kabla ya kwenda Azam alikuwa akiitumikia timu Yanga amefichua siri ya ushindani anaouonyesha dhidi ya wanajangwani akisema ni jududi zake mwenyewe, na huwa haangalii mtu mwingine anafanya nini, isipokuwa nguvu yake ni kuhakikisha huduma yake inaifaa timu iliyomuajiri.
Kama ni mfuatiliaji wa soka la bongo utakuwa umekwishabaini namna ambavyo kiundo mshambuliaji wa Azam FC Feisal Salum ‘Feitoto’ anavyowasumbua wachezaji wa timu yake ya zamani.
Feitoto ambaye kabla ya kwenda Azam alikuwa akiitumikia timu Yanga amefichua siri ya ushindani anaouonyesha dhidi ya wanajangwani akisema ni jududi zake mwenyewe, na huwa haangalii mtu mwingine anafanya nini, isipokuwa nguvu yake ni kuhakikisha huduma yake inaifaa timu iliyomuajiri.
Kile alichokifanya ndani ya Yanga kipindi cha misimu mitano kuanzia 2018 hadi 2022, kisha kuhamia Azam, ilionekana kama anakwenda kufeli, lakini haijawa hivyo.
Ndani ya Azam, huu ukiwa msimu wake wa tatu, Fei Toto anafanya vizuri kila kukicha, huku akisema aliamini kujituma na kuweka nidhamu mbele hakuwezi kumtupa.
Fei Toto akiwa Yanga katika misimu mitano, alifunga mabao 22 kwenye Ligi Kuu, wakati Azam FC katika msimu wake wa tatu kafikisha mabao 33, huku akiasisti mabao 28.
Kutokana na takwimu zake, zimemuibua aliyekuwa kiungo wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Haruna Moshi ‘Boban’ aliyesema: “Wakati anasajiliwa Yanga alikuwa mdogo na kadri anavyokuwa kiwango chake kinazidi kuimarika. Pia amekuwa na muendelezo kila msimu anafanya vizuri, ndiyo maana timu zingine zimekuwa zikishawishika kuhitaji huduma yake.”
Ifahamike kwamba, mwaka 2018 wakati Fei Toto anatoka JKU na kutua Yanga, alikuwa na umri wa miaka 20, hivi sasa anayo 28 akiwa tayari amecheza miaka nane ndani ya Ligi Kuu Bara, hivyo inaonesha amekomaa kwa mapambano.
Mwingine ayezungumzia Toto wa Yanga na Azam ni staa wa zamani wa Simba, Singida Black Stars na Namungo FC, Meddie Kagere raia wa Rwanda aliyesema: “Fei Toto ni kati ya wachezaji wenye vipaji vikubwa Tanzania na anaweza akacheza nchi yoyote kulingana na kile anachokionyesha uwanjani.”
Aliyekuwa beki wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ambaye kwa sasa anaichezea Transit Camp ya Ligi ya Championship yeye alisema: “Wakati mwingine mchezaji anapotoka Yanga tena akiwa anahitajika kama ilivyo kwa Toto, nyuma yake huwa anajituma kwa bidii katika mazoezi, anazingatia nidhamu na akili yake imejaa utulivu.”
Vilevile aliyekuwa winga wa Azam, Gibril Sillah ambaye anaichezea Al-Ahly kwa sasa, naye alimzungumzia Toto akisema: “Ni miongoni mwa vipaji na bidii ya kazi nilivyovishuhudia katika soka la Tanzania ni Fei Toto, ndiyo maana niliwahi kubusu kiatu chake, ana uwezo wa kufanya majukumu mengi uwanjani, anawatengenezea wengine wafunge pia anafunga na mabao ya aina yote, mashuti ya mbali, mipira ya kutenga ya chenga, naamini atafika mbali sana.”
KAULI YA FEI
Akizungumzia matamanio yake, Fei Toto anasema anatamani kila msimu kuandika rekodi mpya na ikitokea hajafikia aliyoiweka nyuma yake anachukulia kama kufeli.
“Ndiyo maana msimu wa 2023-2024 nilimaliza na mabao 19, lakini nikawa na asisti saba, wa 2024-2025 nilikuwa kinara wa asisti 13, lakini nikawa na mabao manne na msimu huu bado unaendelea huenda nikafanya vitu vingine zaidi.
“Ndiyo maana wakati naondoka Yanga wengi wao walijua nitafeli nikiwa Azam, lakini niliweka bidii na kuamini katika kipaji changu, sikutaka kujilinganisha na mwingine, kwani kila mchezaji ana kitu chake cha kuifaa timu, nasisitiza nashindana mwenyewe na siyo mtu,” anasema.