Ibrahim Nindi afanye kazi sana Simba
Muktasari:
- Wachezaji wa kati waandamizi ni Rushine de Reuck na Ismael Toure na ukiondoa hao ndio kuna Ibrahim Nindi na Vedastus Masinde.
KUANZA kupewa nafasi ya kucheza kwa Ibrahim Nindi katika kikosi cha Simba kulikuwa ni fursa nzuri kwake.
Ilikuwa ni kama kuokota embe dodo chini ya mti wa mpera maana kipindi anapewa nafasi, ndio ambacho Simba ina uhaba wa wachezaji wengi wa nafasi ya beki wa kati.
Wachezaji wa kati waandamizi ni Rushine de Reuck na Ismael Toure na ukiondoa hao ndio kuna Ibrahim Nindi na Vedastus Masinde.
Lakini yale makosa ambayo Nindi kayafanya katika mechi ile ya Namungo ambayo Simba ilitoka droo kwa mabao 2-2, sidhani kama yatampa tena urahisi wa kupata nafasi ya kucheza kama ambavyo amepata juzi.
Kwa uzoefu wetu hapa kijiweni, hizi timu zetu kubwa za Kariakoo huwa ni vigumu kumvumilia na kumpa tena nafasi mchezaji ambaye ameifanya ipoteze mechi muhimu au kafanya makosa ambayo yanaziweka kwenye wakati mgumu.
Sasa tumeanza kupata wasiwasi juu ya mdogoetu Nindi maana wale Simba hawakufurahia kabisa zile bao mbili za Namungo dhidi yao japo baadaye walishinda 3-2.
Baada ya kilichotokea, anatakiwa kujituma na kuonyesha kiwango bora hasa mazoezini na katika mechi ambazo atapewa nafasi nyingine vinginevyo mambo yanaweza kuww magumu kwake hapo baadaye.
Kile kitendo cha kutolewa baada ya kucheza kwa dakika 45 tu kinapaswa kumshtua na kumfanya aongeze umakini maana hadi kiungo anarudishwa kucheza katika nafasi yake sio ishara nzuri.
Na isitoshe Wilson Nangu na Abdulrazack Hamza wameshaanza mazoezi baada ya kupona na kuna dogo Mbegu ambaye atarudi hivi karibuni kutoka timu ya taifa ya vijana.