Kane asingeshinda tuzo Tanzania
Muktasari:
- Kane, ambaye ameichezea Tottenham Hotspurs kwa muda mrefu bila kutwaa taji lolote, anakuwa Mwingereza wa kwanza kutwaa tuzo hiyo ya Mpira wa Dhahabu katika kipindi cha miaka 25.
MSHAMBULIAJI Mwingereza wa Bayern Munich, Harry Kane ameibuka kuwa Mwanasoka Bora wa Dunia baada ya kutangazwa usiku wa kuamkia Jumanne kuwa mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or.
Kane, ambaye ameichezea Tottenham Hotspurs kwa muda mrefu bila kutwaa taji lolote, anakuwa Mwingereza wa kwanza kutwaa tuzo hiyo ya Mpira wa Dhahabu katika kipindi cha miaka 25. Nahodha huyo wa England ameibuka mshindi wa tuzo hiyo baada ya msimu ambao ameifungia klabu yake mabao 61 katika mechi 51 alizoichezea Bayern Munich, ambao ni mabingwa wa Ujerumani.
Kwa ujumla, Kane amefunga mabao 73, kutoa pasi nane za mabao katika mechi alizoichezea Bayern na England. Aliwashinda Kylian Mbappe wa Real Madrid na Ufaransa ambaye alishika nafasi ya pili na Lamine Yamal wa Barcelona na Hispania, aliyeshika nafasi ya tatu.
Kihistoria, Kane anakuwa mchezaji wa tano wa England kushinda taji hilo baada ya Stanley Matthews aliyeshinda tuzo hiyo mwaka 1956), Bobby Charlton (1966), Kevin Keegan (1978 na 1979 na Michael Owen (2001).
Kwa Bayern, Kane anakuwa mchezaji wa kwanza kushinda tuzo hiyo tanguKarl-Hein Rummenigge aitwae mwaka 1981. Mtikisa nyabvu huyo hatari pia alishinda tuzo ya Gerd Muller kwa upande wa wanaume. Muller alikuwa mtikisaji mabao hodari wa Ujerumani.
Katika orodha inayoonyesha kuhusika kwa washambuliaji katika mabao, Kane anaonekana kuwa kileleni. Alicheza dakika 4,048, akifunga mabao 61 na kutoa pasi saba za mabao, wakati Mbappe alicheza dakika 3,620, kufunga mabao 42 na kutoa pasi sita za mwisho.
Lakini chini ya wawili hao kuna takwimu tofauti hadi kumfikia Yamal ambaye alikuwa mshindi wa tatu wa Ballon d’Or. Michel Olise alicheza dakika 4,009, kufunga mabao 22 na kutoa pasi 26 za mwisho, huku Erling Haaland akicheza dakika 4,143, kufunga mabao 38 na kutoa pasi tisa za mwisho.
Pia yupo Luis Dias aliyecheza dakika 4,058, kufunga mabao 26 na kutoa pasi 19 za mwisho, ndipo anakuja Yamal ambaye alicheza dakika 3,699, kufunga mabao 24 na kutoa pasi 17 za mwisho.
Katika orodha hiyo ya wachezaji waliohusika katika mabao mengi, hayumo kiungo wa Barcelona na Hispania, Rodri, ambaye alitwaa tuzo hiyo mwaka juzi, wakati Ousmane Dembele aliyetwaa mwaka jana ana idadi ndogo ya mabao na pasi za mwisho.
Katika vinara hao watatu wa Ballon d’Or, ni Yamal pekee ambaye ana taji la dunia baada ya kuiongoza Hispania kutwaa Kombe la Dunia na pia alikuwemo katika kikosi kilichotwaa ubingwa wa Ulaya.
Kane ana taji moja la ubingwa wa soka wa Ujerumani, kitu ambacho alikuwa akikikosa miaka yote akiichezea Spurs na England.
Nimejaribu kuweka takwimu hizo ili kuzungumzia suala la mijadala ambayo hutawala hapa Tanzania kila linapoibuka suala la mchezaji anayestahili kutwaa tuzo, maarufu hapa kwetu kama MVP.
Mara nyingi hoja hujikita kwenye takwimu pekee, kitu ambacho kisingemuwezesha Kane kutwaa tuzo hiyo na pengine uzito mkubwa ungewekwa kwa Yamal mwenye mataji matatu yaani ubingwa wa dunia, ubingwa wa Ulaya na Ligi ya Kuu Hispania.
Lakini, kwa mujibu wa vigezo vya Ballon d’Or, mshindi hupatikana kutokana na kuangalia kiwango chake yaani kujikita katika ufungaji, kutoa pasi za mwisho na kutengeneza nafasi. Kigezo cha pili ni mafanikio ya timu, ambacho huangalia mataji ambayo timu imetwaa katika mashindano makubwa ambayo mchezaji alipata akiwa na klabu na taifa lake.
Na kigezo cha mwisho ni fair play au mchezo wa kiungwana ambao mchezaji huuonyesha na tabia yake nje na ndani ya uwanja.
Hivyo vyote ndivyo huchangia mchezaji kushinda tuzo ya Ballon d’Or na waendeshaji wa tuzo hiyo huangalia takwimu hizo kwa uangalifu na kutoa orodha ya mwisho ambayo huamuliwa na wapigakura, yaani yeyote anayeshinda anakuwa anastahili tuzo hiyo.
Kwa hiyo, ubishi wetu kuhusu mchezaji anayestahili tuzo ya mchezaji bora usijikite katika takwimu pekee, bali sifa nyingine zinazoendana na utamaduni wa mpira wa miguu.
Harry Kane ni mchezaji ambaye amekumbatia sifa kubwa mbili katika hizo, yaani upachikaji mabao na uungwana kwa kuwa ni vigumu kumuona akionyeshwa kadi nyekundu au njano. Lakini tuzo ya kutwaa mataji makubwa inampita pembeni kwa kuwa siyo Bayern Munich wala England iliyoweza kutwaa ubingwa katika miaka ya karibuni au msimu uliopita.