Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kumbe rafiki yetu Sure Boy bado yupo yupo!

JICHO Pict


NILISHAMSAHAU rafiki yangu Sure Boy. Kumbe bado yupo. Juzi nilimwona akiingia uwanjani akitabasamu. Duke Abuya akalazimisha kumpa kitambaa cha unahodha. Alistahili? Ndio alistahili. Si ajabu alikuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi uwanjani.


Si ajabu Duke amemsikia Sure Boy zamani. Labda wakati yupo kwao Kenya alikuwa anamsikia akiichezea Azam na timu ya Taifa. Pengine ndiye mchezaji mkongwe zaidi Yanga kwa sasa. Mtoto wa staa wa zamani wa Yanga, Abuubakar Salum ambaye naye alikuwa anajulikana kwa jina la Sure Boy.

JICH 01

Sure Boy ananichanganya kidogo. Na anaweza kuwachanganya watu wengine pia. Ukimpa dakika 10 tu anaweza kukumbusha anastahili kuanza mechi ijayo. Kama siyo kuanza basi kukaa benchi. Lakini hautamuona katika yote haya mawili.

Miaka michache tu iliyopita wakati Yanga wakiwa njiani kwenda katika fainali za Shirikisho Sure Boy alipewa dimba kule Tunisia katika pambano dhidi ya Club Africain. Khalid Aucho hakuwepo. Akamiliki dimba lake vizuri tu na alikuwa mchezaji bora wa mechi kabla Aziz ki hajafunga bao la ushindi la Yanga

JICH 02

Sure Boy ananichanganya. Yanga wanaishi naye kwa masilahi yao. Kwamba ipo siku tu anaweza kuhitajika uwanjani. Lakini mwenyewe alistahili kuishi kwa masilahi yake. kwamba akiwa Namungo anaweza kuwa kiungo wao tegemeo. Akiwa na Pamba ya Mwanza anaweza kuwa kiungo wao anayeanza wiki hadi wiki.

Hapa labda kuna mambo mawili ndiyo maana hajataka kuchukua maamuzi magumu ya kuondoka zake Jangwani. Kwanza kabisa hataki shida ya kwingineko. Shida ya kwenda kuzima Mashujaa ya Kigoma kisha akasafiri na basi kutoka Kigomba hadi Mbeya kucheza na Mbeya City.

Sure Boy katika ligi kuu amecheza timu za raha tu. Timu mbili kubwa za Dar es salaam. Azam na Yanga. Hizi ni timu za ndege. Timu ambazo zinafikia hoteli zenye ‘swimming pool'. Kuhamia katika timu inayofikia katika Guest House mida hii ya jioni anaona haina maana.

Kama angekuwa ana miaka 28 angeweza kuhamia huko lakini nimesoma mahala ana miaka 36 akikimbilia miaka 37. Naona hataki kuanza kujisumbua uzeeni. Labda sasa hivi anawaza akawe kocha kama rafiki yake John Bocco kuliko kujisumbua na timu ndogo.

JICH 03

Hata hivyo, akipangwa mechi mbili tatu tu za Yanga analeta ukorofi. Anaweza kuwapigisha shoti mashabiki na benchi la ufundi. Ni kwa sababu  ni fundi. Fundi wa mpira. Ana uwezo mkubwa wa kupokea, kutunza mpira na kuachia. Ana uwezo mkubwa wa kuwa bosi wa eneo la katikati ya uwanja.

Hata hivyo, sijamuona muda mrefu. Na ambacho kinanisiganisha mawazo ni pale ninapowaza inakuaje makocha mbalimbali wanaopita Jangwani katika siku za karibuni wote wameamua kumweka benchi? Labda kweli kuna kitu kimepungua katika miguu yake.

Hata hivyo, kwa staili ya soka lake naamini bado kuna timu kibao za ligi kuu anaweza kuzisaidia katika nyakati hizi. Unamkumbuka George Kavilla wa Kagera Sugar? Alikuwa akimiliki dimba katika umri kama huu wa Sure Boy. Staili yao ya mchezo haikutofautiana sana.

JICH 04

Kama angekuwa anacheza soka la kutumia mabavu ningemshauri astaafu kwa sababu umri umesogea. Lakini soka analocheza ni la nafasi. Anafika, anapokea anaachia. Anacheza mpira rahisi wa kutogusana sana. Ukiwa unacheza mpira wa namna hii unaweza kucheza muda mrefu kuliko wale wanaocheza soka la kukimbia zaidi au kukurupushana kwa nguvu zaidi uwanjani.

Labda Sure Boy angetupatia msimu mmoja tu pale Coastal Union au Pamba ya Mwanza. Baada ya hapo tungepima wenyewe jua limezama au bado lipo. Tungeamua wenyewe kumstaafisha au kuendelea kuwa naye. Ni tofauti na hali ilivyo sasa. Hatujui kama bado yumo au ameisha kwa sababu muda mrefu anakaa jukwaani kama sisi mashabiki.

Nimemkumbuka rafiki yangu Sure Boy. Juzi nilipomwona uwanjani nilikumbuka mambo mengi. Nilikumbuka pambano la Taifa Stars dhidi ya Ivory Coast pale Abidjan Juni 2012. Wakati tumewasili katika uwanja wa ndege wa Felix Houphouet Boigny Sure alininong’oneza akitania “kaka hawa jamaa wanaweza kudhani sisi ni ball boys”.

JICH 05

Alikuwa akimaanisha namna wachezaji wa Taifa Stars walivyokuwa na maumbo madogo kulinganisha na wachezaji wa Ivory Coast kina Didier Drogba na wengineo. Na kweli, siku ya mechi ndugu zetu Ivory Coast waliingia na maumbo makubwa uwanjani lakini cha kushangaza katikati ya uwanja kuna nyakati ambazo tuliwamiliki ipasavyo.

Kulikuwa na Sure Boy, Amri kiemba, Frank Domayo na Mwinyi Kazimoto. Kuna wakati zilipigwa pasi nyingi kiasi kwamba mashabiki wa Ivory Coast bila ya hiyana wakawashangilia Stars. Walikuwa wakistaajabishwa na maumbo yao huku pasi zikitembea.

Juzi nilipomwona nikakumbuka pia namna ambavyo hata sisi wengine nyakati zinatutupa mkono. Nilimuona baba yake akicheza hadi akistaafu. Na nikamuona mtoto mtu, Sure Boy huyu akikaribia kustaafu.

Nimemwona akiwa kinda pale Azam kisha akaibuka kuwa mchezaji muhimu kikosini. Umri ukasogea pale kisha akaenda Yanga na sasa ana umri wa miaka 36 akiwa anakaribia kustaafu. Huenda na sisi wengine pia ni umri wa kufikiria kustaafu.