Kuvia damu kwa wanamichezo, Sababu, dalili na matibabu
Muktasari:
- Katika maisha ya mwanamichezo ni kawaida katika siku za maisha yake kuwa na historia ya kupata jeraha lisilovujisha damu lakini likawa na ishara ya kuvimba na kubadilika rangi.
LIGI mbalimbali za kimataifa Ikiwamo EPL, La Liga na Bundesliga zilirudi mwishoni mwa wiki iiliyopita. Vile ligi kuu ya Tanzania bara NBC 2026 nayo imeendelea kwa mechi kadhaa za katikati ya wiki.
Katika maisha ya mwanamichezo ni kawaida katika siku za maisha yake kuwa na historia ya kupata jeraha lisilovujisha damu lakini likawa na ishara ya kuvimba na kubadilika rangi.
Kwa mwanamichezo ambaye rangi ya ngozi ya mwili ni maji ya kunde au mweupe ni rahisi kuona pale alipojeruhiwa au kujijeruhi pengine kwa kujigonga au kugongana na kitu, kubadilika rangi na kuwa pekundu au penye giza. Hii ni hali ya kawaida kuwapata wanamichezo ambao wanacheza michezo inayohusisha kukumbana kimwili ikiwamo mchezo wa soka, kikapu, ngumi, raga na miereka.
Mara nyingi mwanamichezo anaweza kuiona hali hiyo kabla ya kutoka mchezoni au baadaye baada ya kutoka mchezoni. Maeneo ambayo mara kwa mara yanaweza kupatwa na hali hii huwa ni pamoja na ya miguuni, mgongoni, kichwani, usoni au mikononi. Mwanamichezo hapaswi kuwa na hofu kwani kiashiria cha kubadilika rangi eneo la mwili alilojeruhiwa ni kuvia kwa damu ndani.
Hili ndilo tatizo la kawaida la kitabibu linaloweza kutokea pale mchezaji anapopata jeraha butu, yaani lisilomwaga damu nje ya mwili. Mfano mzuri ni pale mwanamichezo anayejeruhiwa na kupata jeraha bapa lisilovujisha damu nje ya mwili. Tishu za mwili zinaweza kujeruhiwa kwa njia kama ya kugongwa na mwili wa mchezaji mwingine. Aina hii yajeraha ndilo hujulikana kitabibu kama ‘blunt injury’.
Aina hii ya jeraha huwa halichani au halitengenezi kukata, bali huwa ni butu. Vilevile kubadilika kwa rangi huwa ni kawaida kutokea katika hatua za awali kama kiashiria mojawapo cha mlipuko wa kinga ya mwili au kuwajibika kwa kinga ya mwili pale mwili unapojeruhiwa.
Mwili hufanya hivyo kutokana na athari inayotokea katika mishipa ya damu inayopeleka damu katika eneo hilo. Katika makala ya leo italitazama zaidi tatizo la kuvilia damu ndani kwa ndani katika eneo lililojeruhiwa bila kuvujisha damu nje ya mwili.
KUVIA DAMU KUNAKUWA HIVI
Kuvilia damu ni kiashiria cha kujeruhiwa kwa mishipa ya damu na kuvujisha damu pasipo kutoka nje ya mwili, hivyo damu hiyo hurundikana na kuganda katika eneo hilo. Wakati wa kufanya mazoezi au kucheza mechi mbalimbali wanamichezo wanaweza kupigwa au kugongwa na kupata majeraha ya misuli ya miguuni, mgongoni, mikononi, kichwani au usoni na damu ikavuja kwa ndani na kuvilia.
Damu hiyo huvuja na kurundikana ndani kwa ndani kutokana na ngozi ya nje kuwa haijapasuka, lakini baadaye inaweza kutengeza uvimbe.
Tatizo hili hutokea katikati ya tando zinazofunika misuli na mishipa ya damu ya eneo hilo au ile ya jirani palipojeruhiwa na kupasuka.
Hali ya damu kuvuja na kurundikana katika misuli hujulikana kitabibu kama ‘muscles contusion’ na hapo baadaye inapoganda na kuvilia hujulikana kama ‘haematoma’. Hali hii huwa na dalili za kubadilika rangi eneo lililojeruhiwa kuwa nyekundu - nyeusi, kuvimba na maumivu. Misuli iliyojeruhiwa huweza kuwa dhaifu na kukakamaa.
Uwepo wa kuvia kwa damu ni vizuri kupewa uzito kwani huenda pia ikawa ni dalili ya kuvunjika mfupa, kuteguka, kuchanika msuli au kukwanyuka kwa ligamenti.
Ndiyo maana wale wanamichezo wa kulipwa ambao michezo ni ajira huwa haraka wanatoa taarifa kwa wataalamu wa afya wa timu au wale binafsi, lengo likiwa ni kuwa na tahadhari ya mapema na hatua zichukuliwe.
Katika hatua za awali mishipa hiyo humwaga damu kwa nguvu na kutawanyika, baadaye taratibu hupungua kisha mrundikano huo wa damu hujazana katika eneo lilipojeruhiwa.
Kutokana na shinikizo la kani ya uvutano (gravity) damu hiyo kama ni miguuni huweza kujaa mbali kidogo na eneo lilipo jeraha kisha huendelea kurundikana ndani ya saa kati ya 24 hadi 48. Kama ni uvimbe wa kuvujia damu huweza kupungua kwa kuwa hakuna shinikizo lolote linaloendelea kuwepo na hivyo hata utendaji kazi wa msuli wa eneo lililojeruhiwa huweza kurudi kawaida.
Ili kuwezesha tatizo hili kupona kwa haraka huduma salama ya matibabu rahisi inaweza kufanyika mapema. Kwa mwanamichezo aliyepata tatizo hilo anatakiwa kuchukua hatua za haraka kulikabili tatizo ikiwamo kupumzika ili kuepusha eneo lililojeruhiwa kupata majeraha zaidi.
Eneo hilo itabidi kulifunga na bandeji na hii unasaidia kuweka mgandamizo, hivyo kusaidia kuzuia damu isiendelee kuvuja. Kwa kuwa eneo hilo lililovimba damu iliyovuja kwa ndani huambatana na maumivu kutokana na shughuli za mlipuko wa kinga ya mwili baada ya tishu kujeruhiwa matumizi ya kuweka barafu yanaweza kutumika.
Barafu inaweza kuwekwa katika mfuko maalumu ili kuepuka barafu yenyewe kugusana moja kwa moja na mwili. Mguu uliojeruhiwa utahitajika kunyanyuliwa juu kuzidi urefu wa kifua cha mjeruhiwa akiwa amelala chali.
Mbinu hii husaidia damu iliyorundikana kuweza kuondolewa kwa haraka na pia kusaidia damu safi kwenda na kutoka eneo hilo kirahisi. Hii ni faida kwa jeraha kwani oksijeni na virutubisho muhimu kwa ajili ya ukarabati na uponaji wa jeraha hufika kwa wingi.
Vifaa tiba saidizi ikiwamo magongo au kiti cha kushikilia vinaweza kutumika ili kujihami na majeraha zaidi wakati wa kutembea kwani jeraha linaweza kuwa kubwa ikiwamo kuvunjika mfupa.
Damu iliyovujia kwa ndani siyo tatizo kubwa linaloweza kumfanya mchezaji kuwa nje muda mrefu, baada ya saa 24-48 tatizo linaweza kuisha.
Endapo tatizo hilo litabainika kuwa kubwa, basi upasuaji mdogo utafanyika ili kuondoa damu iliyovia au kudhibiti isiendekee kuvuja.
Mjuze daktari wa timu au wa kwako binafsi pale unapoona viashiria vya kuvia damu katika maeneo ya mwili uliojeruhiwa au fika katika huduma za afya mapema kwa ajili ya ushauri, uchunguzi na matibabu.