Madeni yaliishusha Mwenge, sasa imerudi kivingine Zanzibar
Muktasari:
- Mwenge ilikuwa miongoni mwa timu zilizoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Pemba msimu wa 2025-2026, huku ikiwa na azma ya kumaliza katika nafasi mbili za juu na kupata tiketi ya kupanda daraja kurejea Ligi Kuu Zanzibar 2026-2027.
TIMU ya Mwenge imefanikiwa kurejea Ligi Kuu Zanzibar 2026-2027 baada ya msimu wa 2024-2025 kushuka daraja, huku sababu kubwa ya kushuka kwao wakati huo ikitajwa ni madeni yaliyoikabili klabu hiyo.
Mwenge ilikuwa miongoni mwa timu zilizoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Pemba msimu wa 2025-2026, huku ikiwa na azma ya kumaliza katika nafasi mbili za juu na kupata tiketi ya kupanda daraja kurejea Ligi Kuu Zanzibar 2026-2027.
Kocha wa timu hiyo, Mohammed Saidi ‘Shuberi’, anasema kabla ya kufanikisha malengo yao, wakati wakishiriki Ligi Daraja la Kwanza walihitaji kurejea Ligi Kuu, hivyo walikuwa wamejipanga kimwili na kisaikolojia kuhakikisha wanafikia malengo yao.
Katika kufanikisha hilo, Mwenge ilifanya maandalizi ya kuimarisha kikosi baada ya kubaini kuwa kushuka kwao daraja mbali na changamoto za madeni, pia kulichangiwa na kutokuwa na wachezaji waliokidhi mahitaji ya timu.
Safari ya Mwenge kurejea Ligi Kuu haikuwa nyepesi, kwani ililazimika kukabiliana na ushindani mkubwa katika Ligi Daraja la Kwanza Pemba.
ILIYOPITIA MSIMU WA 2024-2025
Baada ya Mwenge kurejea Ligi Kuu Zanzibar, uongozi wa timu hiyo umesema madeni ndicho kitu kikubwa kilichosababisha kushuka daraja msimu wa 2024-2025 baada ya fedha za mfadhili wa ligi hiyo kutumika kulipa madeni hayo.
Mtendaji Mkuu wa Mwenge, Ali Seif Said anasema hatua hiyo ya kulipa madeni, ilifanya washindwe kuwalipa wachezaji wa kikosi hicho, wakashindwa kufanya vizuri uwanjani.
Anasema, awali timu hiyo ilikuwa na malengo ya kufanya vizuri kwani kila mmoja anapotafuta kitu anategemea kufanikiwa lakini kutokana na hali ya kiuchumi na mazingira yalivyokuwa hayakuwezekana.
Kiongozi huyo anasema, msimu wa 2024-2025 waliinunua timu iliyopanda daraja na kuiita Mwenge, huku wakilenga kufanya vizuri, lakini ikawa tofauti.
“Baada ya kununua timu iliyopanda daraja, tulishindwa kuiendesha katika ligi kuu kuhusiana na masuala ya wachezaji na timu kuiweka vizuri kwa sababu tuliingia kwenye mkumbo wa kukabiliwa na madeni mengi, kwahiyo kuna watu walihitaji warejeshewe fedha na usajili ulikuwa haukuwa mzuri kwa upande wetu,” anasema kiongozi huyo.
Said anasema, baada ya kushuka daraja, uongozi wa timu hiyo ulikaa pamoja kutengeneza mikakati ya kukatafakari kwa kina wakiwa na mpango wakurejea Ligi Kuu.
“Kwa kweli tunashukuru baada ya kukaa chini baina ya uongozi na wachezaji, sambamba na baadhi ya mashabiki, tukakubali kwamba timu imeshuka daraja na sasa hivi tunataka kurejea Ligi Kuu na tuhakikishe kila sekta inakaa vizuri,” anasema.
Anasema, wanashukuru timu hiyo imepanda daraja kwa nguvu zake yenyewe bila kutumia njia ya awali kununua timu.
TOFAUTI YA LIGI KUU NA DARAJA LA KWANZA
Kiongozi huyo anasema tofauti kubwa ya Ligi Kuu inakuwa na mdhamini mkuu ambaye anawasaidia lakini Ligi Daraja la Kwanza hakuna mdhamini, ni nguvu za wenyewe viongozi na wapenzi kuihakikisha timu.
“Ligi Kuu faida yake ni kwamba yupo mdhamini anayetoa kiasi fulani kwa timu na mahitaji yanapungua kwa sababu kunakuwa na mambo unapata.
“Lakini Daraja la Kwanza hakuna chochote, ni timu yenyewe kupambana kuhakikisha timu inapata matokeo panapohitajika,” anasema.
ILIVYOREJEA LIGI KUU
Said anasema, timu hiyo ilikuwa na wachezaji walioshuka nao daraja, lakini pia wakaongeza nguvu kwa kuleta wengine ambao wapo nao hadi sasa kwa ajili ya timu kufanikisha inashiriki vyema ligi kuu.
Kiongozi huyo anasema uimara wa kikosi katika ushiriki wao wa Ligi Daraja la Kwanza Pemba ndiyo umeifanya timu hiyo kurejea Ligi Kuu Zanzibar baada ya msimu mmoja pekee.
Mwenge ilimaliza nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Daraja la Kwanza Pemba 2025-2026 ikikusanya pointi 67, nyuma ya vinara Wembe waliokuwa na pointi 72.
Katika michezo 30 iliyocheza Mwenge, ilishinda 19, sare 10 na kupoteza moja, huku ikifunga mabao 43 na kufungwa 15. “Wachezaji tulionao kwasasa tuna imani nao kubwa kuhakikisha kwamba timu inafanya vizuri, kwani wenyewe wapo tayari kupambana uwanjani kutafuta maslahi.
“Wachezaji wana msimamo, wanaipenda timu na wanaitumikia kihaki kuhakikisha tunafikia malengo,” anasema Said.
MKAKATI MPYA
Anasema baada ya kuona madeni na udhaifu wa kikosi chao kuchangia pakubwa kushuka daraja, sasa wamejipanga katika mazingira mawili ikiwemo kuwa na mdhamini wa timu badala ya kutegemea mdhamini mkuu pekee wa Ligi, huku pia wakifanya usajili wa wachezaji bora na watakaoiweka timu sehemu nzuri.
UJUMBE KWA MASHABIKI WA MWENGE
Mtendaji huyo anasema, wanahitaji hamasa iendelee katika Ligi Kuu Zanzibar kwani bado wana uwezo wa kufanya makubwa.
“Tunawapongeza mashabiki kuwa pamoja tangu timu ilivyoshuka daraja hadi kurejea Ligi Kuu Zanzibar, wanedelee na moyo huo kwani bado tunawahitaji,” anasema Said.