Prime
Madridista wameamua kumtoa Mbappe kafara, ni ujinga
WAMEMZOMEA Kylian Mbappe hapa majuzi. Watu wa Madrid wana majivuno hasa. Neno 'Real' maana yake ni Royal. Tangu enzi hizo wanajiona wao ni wafalme. Ndio maana wana ugomvi usioisha na watu wa Catalunya. Watu wa Madrid wanajisikia hasa. Kuanzia katika historia hadi sasa.
Dikteta wa Hispania wakati huo, Francisco Franco Bahamonde alitokea Madrid. Watu wa Madrid huwa wanajiona ni 'babkubwa' kuliko watu wa pande nyingine za Hispania hasa upande ule wa Catalunya. Wakati huohuo watu wa Catalunya ni wapiga kazi hasa. Na kitu kizuri eneo lao lina bahari tofauti na huku Madrid. Kimabavu watu wa Madrid hawataki Wacatalunya wajitangazie uhuru wao.
Ule upande wa Catalunya una watu waaminifu wa daraja la chini au la kati katika maisha. Wakishika jambo lao huwa wanalishika hasa. Wanalipenda eneo lao. Hauwaambii kitu. Ndio akina Pep Guardiola hawa. Yupo Manchester lakini akili yake ipo Catalunya. Mara kadhaa amekuwa katika kampeni za kutaka Catalunywa ipewe uhuru wao.
Nimekumbuka jambo hili juzi baada ya kuona mashabiki wa Real Madrid wakimzomea Mbappe. Kabla ya kumzomea katika pambano hili dhidi ya Real Oviedo tayari walikuwa wamepitisha muswada wa mitandaoni wa kutaka Mbappe aondoke katika klabu yao. Mpaka nilipoishia mashabiki milioni 30 walikuwa wametaka Mbappe aondoke Santiago Bernabeu, maajabu.
Kwanini wanataka Mbappe aondoke Real Madrid? Sijawahi kuelewa. Na sidhani kama nitaelewa. Msimu wake wa kwanza tu akiwa na Madrid alifunga mabao 43. Mtu ambaye aliwahi kufanya hivyo akiwa katika msimu wake wa kwanza ni Cristiano Ronaldo. Alifunga mabao 37. Bado Real Madrid wanamzomea Mbappe.
Msimu wa pili, ambao ni msimu wake wa pili amefunga mabao 41 katika mechi 41. Mbappe ana kosa gani hapo? Hana. Tatizo ni kwamba Real Madrid haijatwaa chochote tangu Mbappe amefika. Hilo ndio wanaona kosa kubwa. Ubingwa huwa sio wa mchezaji mmoja. Wakati mwingine mnaweza kupewa ubingwa na golikipa tu. Wakati mwingine unaweza kupewa ubingwa na safu ya ulinzi.
Msimu huu kama Arsenal wakitwaa taji lolote la ubingwa basi anayehusika zaidi anaweza kuwa kipa David Raya. Akina Bukayo Saka wangeweza kufunga mabao lukuki kule mbele lakini kama wasingekuwa na Raya langoni sidhani kama wangeweza kufika nafasi waliyopo sasa hivi katika michuano yote miwili. Ligi Kuu ya England na Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.
Tatizo jingine ni kwamba wakati Madrid wakiwa katika mbio za ubingwa kabla ya kumkabidhi Barcelona kombe wiki iliyopita, Mbappe alikuwa na majeraha na aliamua kwenda kujipumzisha Italia na mpenzi wake. Kwa mujibu wa Mbappe Madrid walimpa ruhusa hiyo. Mashabiki wa Madrid wanaamini kwamba hakuwa mzalendo. Ni kitu cha kawaida tu kwa wachezaji. Mashabiki waliamua kuwa na nongwa.
Imewahi kumtokea Cristiano Ronaldo. Amewahi kuzomewa Pale Santiago Bernabeu. Maringo tu ya mashabiki. Wanaamini kwamba wao wapo juu ya mashabiki. Fikiria kwamba waliwahi hata kumzomea Zinedine Zidane akiwa kama mchezaji. Mashabiki wao wana maringo tu. Baada ya kutazama takwimu za Mbappe unaweza kuona kosa lake lolote?
Kitu cha kushangaza ni kwamba hata Mbappe mwenyewe ana hasira ya kutopata taji lolote la Ulaya mpaka sasa. Ana bahati mbaya. Alipoamua kuondoka tu PSG wao wakachukua ubingwa wa Ulaya na yeye mpaka leo hajapata kitu. Lakini pia unapoangalia aina ya mchezo wa Mbappe hakuna mahala unaweza kudhani kwamba anacheza chini ya kiwango kwa makusudi. Namba zake zinathibitisha hilo.
Madrid ndivyo walivyo. Hauwezi kusikia mashabiki wa Barcelona wakimzomea mchezaji wao staa. Barcelona wakikuweka moyoni huwa wanakuweka kisha wanakuhifadhi moyoni. Haishangazi iliwauma sana wakati Luis Figo alipoamua kuvuka mipaka na kuondoka zake Catalunya kwenda Madrid. Wale watu wakikuweka moyoni huwa hautoki kirahisi.
Umewaza kwamba siku moja mashabiki wa Barcelona wangeweza kumzomea Lionel Messi au Andres Iniesta au Xavi Fernandes? Kwa sababu yoyote ile ya kukosa kombe wasingeweza kufanya kile ambacho Madrid wamewahi kufanya kwa Zinedine Zidane, kisha Cristiano Ronaldo halafu sasa kwaMbappe. Ni basi wataamua kuonyesha jeuri kwa mchezaji bila ya sababu za msingi.
Nini kitaendelea kati ya Mbappe na Madrid. Historia inaonyesha kwamba kuna wachezaji wengi waliwahi kuzomewa kama hivi lakini wakaishia kuwa mashujaa katika klabu. Hata Ronaldo mwenyewe baada ya kuzomewa aliishia kuwa shujaa wao kwa kutwaa mataji mengi tu. Aliacha alama klabuni na alifunga midomo yao.
Sijui kama Mbappe ataamua kufuata njia hii. Kila mtu ameumbwa tofauti. Kuna ambao wanavumilia na kujaribu kuwathibitishia mashabiki kuhusu ubora wao. Wachezaji wengine hawana muda huo. Sijui Mbappe yupo upande gani lakini ninachojua ni kwamba Wafaransa wana maringo sana. Mbappe ni Mfaransa. Anaweza akaamua kuondoka zake Santiago Bernabeu mwishoni mwa msimu. Baada ya kuvunjika kwa mahusiano yake na mashabiki mpaka sasa anaweza kuchukua hatua tofauti.
Na kama akichukua hatua hiyo? Lolote linaweza kutokea. Kuna watu wana vibunda vyao na wanamtazama kwa jicho la kumtamani. Nani hataki kuwa na Mbappe? Anacheza katika klabu yoyote kubwa duniani kwa sasa. Anaingia katika kikosi cha kwanza. Tatizo ni ada yake ya uhamisho na mshahara wake. Hata hivyo Manchester City na Manchester United wanaweza kulipa mshahara wake moja kwa moja.
Kwa Manchester United kuna anguko wamepitia na Mbappe anaweza asiwe na tamaa ya kwenda huko. Manchester City wana kila kitu ambacho kinaweza kumvutia mchezaji wa daraja la Mbappe. Wana hela na wanatwaa mataji. Hakuna mchezaji ambaye hawezi kuvutika na mradi wao. Hakuna.
Tinu yangu Arsenal? Huwa haisajili wachezaji wa aina ya Mbappe. Huwa inaweza kuwatengeneza wachezaji wa aina ya Mbappe lakini haiwezi kuwanunua wachezaji wa aina hiyo. Arsenal ilichowahi kuweza ni kuvunja rekodi ya uhamisho ya ndani tu kwa Declan Rice lakini haijawahi kuingia hata kumi bora ya rekodi za uhamisho wa dunia.
Tusubiri kuona sinema ya Mbappe na Madrid itaishia wapi. Binafsi imenishangaza. Madrid wana mastaa wengi. Kuna Vinicius Junior, kuna Jude Bellingham, kuna akina Rodrigo. Kuna wengi. Tatizo wameliona kwa Mbappe tu mwenye namba nzuri. Ni ubaguzi fulani tu wa kawaida. Ni azimio fulani hivi lisilo la lazima ila ni kupeleka presha kwa wachezaji mastaa zaidi klabuni.