Prime
Mamelodi, Yanga sawa na hadithi ya walevi wawili
Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini imetinga fainali yake ya pili mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuitoa Esperance de Tunis ya Tunisia kwa jumla ya mabao 2-0 kutokana na matokeo ya ushindi wa bao 1-0 nyumbani na ugenini.
Msimu uliopita, Mamelodi pia ilitinga fainali ya Ligi ya Mabingwa na kufungwa na Pyramids ya Fiston Mayele wa moto.
Kabla ya fainali hizo mbili, Mamelodi ilikutana na Yanga kwenye robo fainali ya mashindano hayo mwaka 2024. Mechi zote mbili ziliisha kwa suluhu (0-0) na Yanga kutolewa kwa mikwaju ya penalti.
Hata hivyo, mechi ya marudiano kule Pretoria Afrika Kusini, ilizua utata mkubwa kwa Yanga kuamini ilistahili bao halali. Yanga ilipiga kelele nyingi sana ilistahili kushinda mchezo ule na kutinga nusu fainali. Lakini tangu pale Yanga haijawahi kuvuka hatua ya makundi na Mamelodi inacheza fainali ya pili.
Hapa ndipo ninapoukumbuka mkasa wa walevi wawili marafiki waliokuwa pamoja tangu watoto, wakasoma pamoja, wakajifunza kunywa pombe pamoja na kuendelea kuishi pamoja kama ndugu.
Wake zao hawakupenda tabia zao za ulevi wa kupitiliza. Wakawashauri waache pombe, ikashandikana, wakaanza kukata tamaa.
Siku moja, mke mmoja alikutana na watu waliomshauri cha kufanya ili waume zao waache pombe. Wakawashauri wawakodi vijana wa kijiweni ili waende kulewa kwenye baa ambazo waume wao hupendelea kunywa.
Wajisogeze kwenye meza yao na wanywe pamoja huku wakilipa ‘bili’ zote. Wahakikishe wanalewa chakari hadi wapoteze fahamu. Ikishakuwa hivyo wawavue nguo halafu wawavunjie mayai ‘sehemu za nyuma’ halafu wawarudishe nyumbani.
Wale vijana wahuni wa mitaani wakafanya kama walivyoagizwa na ‘wateja wao’. Na wale walevi bila kujua ulikuwa mtego, wakafakamia pombe za ofa za ‘marafiki zao’ wa siku moja hadi wakapoteza fahamu. Wale vijana wahuni wakawachukua wale walevi na kuwavunjia mayai ya kutosha kisha wakawabeba hadi kwa wake zao, wakawakabidhi.
Wakalala fofofo na kuzinduka alfajiri huku wakijisikia utelezi kwa nyuma. Mmoja akakimbilia bafuni kujikagua. La haula, kweli kunateleza. Akashtuka, Akajigusa tena, akainama chini na kuanza kulia akadhani ameingiliwa kinyume na maumbile. Mke akataka kucheka kwa sababu alijua mchezo mzima. Lakini akajikausha na kuuliza, “mume wangu, kuna nini bafuni hadi unalia?”
Mume akapotezea, “ah, hamna kitu”, kisha akauliza, “hivi mke wangu, jana nililewa sana ehe! Nilirudi vipi nyumbani?” Mke akajibu, kuna marafiki zako fulani wahuni wahuni hivi walikurudisha. Jamaa akashtuka, kisha akasema “pombe sinywi tena.” Mke akauliza, “kwani mume wangu leo una nini, mbona sikuelewi maneno unayosema?” Mume akajibu, “sasa hunielewi nini wakati nasema pombe sinywi tena?”
Akachukua ‘boxer’ yake na kuanza kuifua. Mke akasema, “mume wangu, tangu lini ‘boxer’ zako unafua mwenyewe, mbona leo unakuwa hivyo lakini?” Jamaa akasema, “sitaki maneno mengi, pombe sinywi tena, basi.” Mke akajisemea moyoni ‘dawa imemuingia huyu, kakoma’.Akaenda kumkumbatia mumewe na kusema, “ahsante Mungu kwa kumuokoa mume wangu kutoka kwa adui pombe.”
Yule mlevi mwingine naye hali ilikuwa vilevile kwa mkewe, tofauti ni moyoni aliweka nadhiri kukicha atarudi baa akawakamate wale jamaa ili alipize kisasi, kisha aache pombe. Basi kulipokucha na akaenda baa kama alivyodhamiria kuwasubiri wale jamaa. Wakati anawasubiri, akaagiza moja ya moto na moja ya baridi.
Akaagiza na zingine na zingine, lakini hakuwaona. Akasema atarudi kesho na kesho ilipofika, hakuwaona.
Basi stori ikawa hivyo na jamaa akaendelea kuwa mlevi kupindukia huku mwenzake akiwa ameacha kabisa pombe.
Stori ya walevi hawa ndiyo sawa na mkasa wa Yanga na Mamelodi Sundowns.
Yanga sawa na yule mlevi aliyerudi baa akitaka kuwakamata wale vijana wahuni na matokeo yake akaendelea kuwa mlevi.
Mamelodi ni sawa na yule mlevi aliyeamua kuacha pombe kabisa na sasa mambo yake ni safi.
Baada ya muda kidogo tu, tofauti baina yao imekuwa kubwa sana.
Mamelodi wako fainali ya pili, huku Yanga wakishindwa kuvuka hatua ya makundi.