Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mamlaka ziko wapi changamoto za waamuzi?


Mara kwa mara mtendaji mkuu wa Kampuni ya Waamuzi wa Mechi za Soka la Kulipwa (PGMOL), Howard Webb hujitokeza kuzungumzia utata unaojitokeza kwenye uamuzi wa mechi za Ligi Kuu England na kuelezea kasoro au kufafanua uamuzi.


Mara nyingine hujitokeza kuzungumzia jinsi kampuni hiyo inavyoandaa mkakati wa kuwezesha waamuzi kufanya vizuri zaidi, vizuri kwamba wao wana teknolojia ya hali ya juu na kazi yao ni kueleza changamoto halafu wataalamu wa teknolojia ya mawasiliano wanaingia kazini kutafuta suluhisho.

Hii husaidia kupunguza lawama dhidi ya waamuzi, pia marefa hujibidiisha kufanya vizuri ili isitokee Webb anaita waandishi kila baada ya raundi fulani kuzungumzia matatizo ya uamuzi au kuzungumzia kasoro za mwamuzi mmoja.

 PGMOL, ambacho ni chombo kilichoundwa kwa ajili ya kusimamia na kuratibu waamuzi wa ligi hiyoa, imekuwa ahueni kwa matatizo ya waamuzi na uamuzi na mara zote kuna watu wanakuna vichwa kufikiria jinsi ya kuboresha uamuzi na kupunguza malalamiko na shutuma zinazoharibu raha ya mchezo huo mzuri.

Tangu msimu uliopita watu wameacha kuzungumzia uzuri wa mpira wa miguu, wameacha kuzungumzia ubora wa wachezaji, wala hawazungumzii mbinu za kocha bali midomo imejaa lawama dhidi ya waamuzi.

Ni kweli lawama hizo hutokana na unazi wa klabu mbili za Dar es salaam, Yanga na Simba, lakini si kitu cha kunyamazia wakati raha ya mchezo wenyewe inapotea taratibu kutokana na baadhi kudhani mamlaka zinachagua timu ya kutwaa ubingwa.

Pamoja na lawama hizo kujaa unazi, zinazalishwa na kasoro nyingi za waamuzi ambao wanaonekana wameshindwa kuwa makini katika tafsiri ya sheria za kuotea, kunawa mpira na matukio mengine yanayohusu adhabu za kadi.

Kibaya zaidi ni kwa sasa kuna teknolojia zaidi ya miaka hiyo ya nyuma. Picha za marudio za video ni rahisi kwa mtu yeyote kuzipata mitandaoni baada ya mechi na kuzitengeneza kuonyesha kasoro ya mwamuzi katika tafsiri ya tukio fulani na hivyo kujenga hali ambayo hoja yake inaweza kuaminika.

Na zaidi ya hayo, ile Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi, maarufu kwa jina la Kamati ya Saa 72, inaibuka na kuadhibu waamuzi waliotuhumiwa kufanya kosa hilo na sentensi yao huwa moja tu; kushindwa kutafsiri vizuri sheria bila ya kusema tafsiri sahihi ni ipi.

Hata hao waamuzi wa zamani wanaojaribu kujadili matukio tata ya uamuzi kwenye televisheni, bado hawatoi maoni yanayoweza kuaminika kuna tafsiri sahihi au potofu ya matukio, hasa kwa nchi kama hii ambayo ina wendawazimu wa mapenzi kwa klabu hizo mbili kongwe.

Katika mazingira haya ni muhimu sana kwa mamlaka, hasa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kufikiria mbinu za kupunguza lawama hizi au tuhuma dhidi ya chombo hicho kuwa kinataka timu fulani itwae ubingwa na hivyo haioni shida kunapokuwa na lawama dhidi ya uamuzi mbovu.

Si busara hata kidogo kwa kiongozi mkuu wa soka kujitokeza kuzungumzia uamuzi na hatua ambazo TFF inaweza kuchukua kukitokea matatizo katika mechi moja tu, yaani ya Simba na Yanga.

Ni kauli iliyotakiwa itolewe kuzungumzia tatizo la uamuzi kwa ujumla baada ya utafiti wa kina na hivyo kuzungumzia kasoro hizo zinasababishwa na changamoto gani na wameamua kuzishughulikia vipi.

Adhabu dhidi ya waamuzi za kuwafungia miezi miwili au sita hazitoshi kushughulikia tatizo hili linalozidi kuwa kubwa. Vitisho vya kuwapeleka mahakamani haviwezi kuondoa tatizo hili, hasa kama hakuna utafiti wowote unaoonyesha matatizo ya uamuzi yanatokana na wengi wao kuhongwa.

Ni lazima mamlaka zichunguze tatizo ni nini. Je, kuna mfumo au mchakato mzuri wa kupata waamuzi wa kuchezesha ligi za juu? Ili mwamuzi afikie daraja hilo anatakiwa apitie hatua gani, maana ni ajabu kuona waamuzi wapya wengi na wengine inawezekana hata ligi za wilaya hawajachezesha.

Kama kuna mpango wa makusudi wa ukondowishaji (mainstreaming gender issues) wa masuala ya jinsia, nini kinafanyika ili kupata waamuzi bora wa kike au ni kutafuta kuacha lawama kuwa uongozi fulani ulipandisha wanawake wengi kuwa waamuzi wa kati.

Wenzetu Ulaya walianza ukondowishaji muda mrefu, lakini ni nadra sana kuona mwamuzi wa kike akiwa refa wa kati hata Chama cha Soka Ulaya (UEFA) kilianza kuwatumia waamuzi wa kike miaka minne iliyopita katika mashindano ya Conference League. Sisi tunakimbilia wapi, maana matatizo mengi huhusishwa na waamuzi wasaidizi wa kike.

Kuna haja kwa TFF na Kamati ya Waamuzi, kwanza kuchunguza changamoto hizo na kutafuta mkakati wa kuzishughulikia, lakini zaidi kuja na mfumo wa kuwasiliana na umma wakati matatizo ya uamuzi yanapokithiri.

Inawezekana kabisa marefa wakawa wanafanya tafsiri nzuri ya sheria, lakini upotoshaji unakuwa mwingi mitandaoni na kwenye vyombo vya habari na hivyo raha ya mchezo kuondolewa. Bila ya ufafanuzi kutokana kwa mwamuzi mbobevu aliyeaminiwa na TFF na Kamati ya Waamuzi, ladha ya soka itaendelea kuharibiwa na upotoshaji.

Raha ya mchezo huu uliopewa sifa ya beautifull game, itapotezwa iwapo mamlaka zitakalia kimya kero za kasoro za uamuzi zinazozungumzwa kila wiki. Watu watapotea viwanjani kwa kuona hawawezi kupata burudani inayotoa mshindi wa kweli bali anayetakiwa na mamlaka.