Manchester United, Liverpool kuwasha moto Old Trafford leo
Muktasari:
- Katika msimamo wa ligi hiyo ya Malkia, United wanaonekana kuwa hatua moja mbele, wakishika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 61 huku Liverpool wakiwafuatia katika nafasi ya nne wakiwa na pointi 58.
MANCHESTER, ENGLAND: PATAKUWA hapatoshi Old Trafford pale ambapo vigogo wawili wa soka la England, Manchester United na Liverpool, watakutana leo, Jumapili katika Dabi ya Kaskazini-Magharibi kwenye Ligi Kuu ya England huku kila mmoja akisaka heshima na nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa.
Katika msimamo wa ligi hiyo ya Malkia, United wanaonekana kuwa hatua moja mbele, wakishika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 61 huku Liverpool wakiwafuatia katika nafasi ya nne wakiwa na pointi 58.
Tofauti hiyo ndogo ya pointi (tatu) kati yao inaifanya mechi hii kuwa na uzito zaidi, kwani ushindi unaweza kubadili kila kitu katika hatua za mwisho za msimu. United wanaingia uwanjani wakiwa na morali kubwa baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Brentford, matokeo yaliyowaweka karibu zaidi na ndoto yao ya kurejea kataika michuano hiyo. Kikosi hicho kinahitaji pointi tatu za mechi ya leo kuhakikisha kinamaliza ndani ya tano bora, jambo linalowapa presha chanya ya kumaliza kazi mbele ya mashabiki wao.
Chini ya kocha Michael Carrick, Manchester United wamekuwa timu nyingine kabisa, wakionyesha ubora na ufanisi mkubwa katika mechi zao za hivi karibuni. Wamekusanya pointi 29 katika kipindi hicho, rekodi bora kuliko timu yoyote, jambo linaloonyesha namna walivyobadilika na kuwa tishio. Faida nyingine kubwa kwa United ni ubora wao wakiwa nyumbani ambapo wamepoteza mchezo mmoja pekee dhidi ya timu za juu msimu huu. Rekodi hiyo inaifanya Old Trafford kuwa ngome imara na kuwapa mashabiki wao matumaini makubwa ya ushindi katika dabi hii.
Kwa upande wa Liverpool, nao hawako nyuma katika mbio hizi. Wanaingia wakiwa na kasi ya ushindi wa mechi tatu mfululizo, kitu ambacho hakikutokea tangu mwanzo wa msimu. Ushindi wao wa mabao 3-1 dhidi ya Crystal Palace umeongeza uhai na kuimarisha imani ndani ya kikosi.
Matokeo hayo pia yamepunguza presha kwa benchi lao la ufundi huku kocha wao, Arne Slot akianza kurejesha imani ya mashabiki. Hata hivyo, changamoto kubwa kwa Liverpool imekuwa ni rekodi yao dhidi ya timu kubwa msimu huu.
Katika mechi 12 walizokutana na timu za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo, Liverpool wameshinda mara moja, wakitoa sare saba na kupoteza nne. Takwimu hiyo inaweka doa kabla ya kukutana na United wanaoonekana kuwa katika ubora wao.
Zaidi ya hapo, Liverpool hawajapata ushindi wowote ugenini dhidi ya timu za juu msimu huu, hali inayoongeza presha kabla ya kushuka Old Trafford, uwanja ambao tayari una historia ya kuwatesa.
Katika mechi 19 zilizopita za ligi kati ya timu hizi, United wameshinda mara tatu huku Liverpool wakionekana kuwa na makali zaidi.
Hata hivyo, ushindi wa mabao 2-1 walioupata United katika mchezo wa kwanza msimu huu unawapa nguvu wakiamini wanaweza kufanya kile ambacho hawajafanya kwa muda mrefu kuwafunga Liverpool mara mbili ndani ya msimu mmoja.
Kwa upande wa takwimu, mechi za United zimekuwa na burudani ya mabao, ambapo michezo 25 imekuwa na mabao kutoka pande zote mbili. Hii inaonyesha wazi kuwa timu hii ina nguvu ya kushambulia lakini pia inaacha mianya ya kuruhusu mabao.
United pia wamekuwa hatari wanapoongoza kipindi cha kwanza, wakishinda mechi nane kati ya tisa walizoongoza nyumbani kabla ya mapumziko. Hii ina maana Liverpool watapaswa kuwa makini tangu dakika za mwanzo.
Kwa upande wa Liverpool, mabao yao mengi ya ugenini yamekuwa yakifungwa kipindi cha pili huku wakifunga mabao matano kabla ya mapumziko kati ya mabao 25 waliyofunga ugenini.
Miongoni mwa nyota wa kuangaliwa ni pamoja mshambuliaji Benjamin Sesko ambaye ameendelea kung’ara kwa upande wa United, akiwa tayari amefunga mabao 10 ya ligi, mengi yakiwa baada ya dakika 30 za mchezo.
Kwa upande wa Liverpool, matumaini yao yanabebwa na Alexander Isak ambaye anatarajiwa kucheza mechi yake ya 100, akiwa na hamu ya kuweka alama muhimu katika dabi hii. Hata hivyo, pigo kubwa kwa Liverpool ni kukosekana kwa nyota wao Mohamed Salah ambaye amejiunga na orodha ya majeruhi, hali inayopunguza nguvu ya ushambuliaji ya timu hiyo. Habari njema kwao ni kurejea kwa kipa Alisson Becker ambaye anaweza kuongeza uimara katika safu ya ulinzi.
CHIMBUKO LA DABI
Uhasama kati ya Manchester United na Liverpool una mizizi yake tangu mwishoni mwa karne ya 19, ukichochewa zaidi na ushindani wa kiuchumi kati ya miji ya Manchester na Liverpool.
Ipo hivi, Ujenzi wa Manchester Ship Canal mwaka 1894 uliifanya Manchester kuwa na njia ya moja kwa moja ya usafirishaji wa bidhaa kupitia bahari, hivyo kupunguza utegemezi wake kwa bandari ya Liverpool.
Hatua hiyo iliathiri uchumi wa Liverpool na kuongeza uhasama kati ya miji hiyo miwili.
MAFANIKIO YAO
Manchester United wanatajwa kama wafalme wa soka la ndani nchini England kutokana na rekodi yao ya kushinda ubingwa wa ligi mara 20, idadi ambayo ni kubwa kuliko klabu nyingine yoyote nchini humo.
United pia imeshinda Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu, pia wametwaa FA Cup mara 12, League Cup mara sita, Europa League mara moja, UEFA Super Cup mara moja pamoja na Kombe la Dunia la Klabu mara moja.
Mafanikio haya yanaifanya United kuwa moja ya klabu zenye historia tajiri zaidi duniani, jambo linalochochea zaidi ushindani wao mkali na Liverpool kila wanapokutana.
Kwa upande wa Liverpool, yenyewe imetwaa Ligi Kuu England mara 19, huku ikiwa na mafanikio makubwa zaidi barani Ulaya kwa kushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya mara sita, zaidi ya klabu yoyote ya England.
Mafanikio hayo yameifanya Liverpool kuwa nembo ya ubora katika soka la Ulaya kwa miongo kadhaa.
Mbali na hayo, Liverpool pia imetwaa FA Cup mara nane, League Cup mara 10, Europa League mara tatu, UEFA Super Cup mara nne pamoja na Kombe la Dunia la Klabu mara moja.