Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Masai: Niligomea mkwanja wa vigogo nikachagua heshima

MASAI Pict (1)
MASAI Pict (1)

Muktasari:

  • Anaelezea ofa hizo alizipata baada ya Mtibwa kushuka daraja msimu wa 2023/24, lakini hakuona sababu ya kuweka mbele tamaa ya pesa, badala yake aliunganisha nguvu na wenzake ili kuhakikisha wanairudisha timu hiyo katika Ligi Kuu.

BEKI na nahodha wa Mtibwa Sugar, Oscar Masai amesimulia alivyokataa ofa nono kutoka baadhi ya timu za Ligi Kuu Bara ili kujijengea heshima itakayokuwa inasimuliwa na wachezaji watakaofuata nyuma yake.

Anaelezea ofa hizo alizipata baada ya Mtibwa kushuka daraja msimu wa 2023/24, lakini hakuona sababu ya kuweka mbele tamaa ya pesa, badala yake aliunganisha nguvu na wenzake ili kuhakikisha wanairudisha timu hiyo katika Ligi Kuu.

“Nilijisikia vibaya kushuka na timu nikiwa kama nahodha kwani nyuma yangu walikuwepo wenzangu kama Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ licha ya kupitia changamoto hawakushuka, kitu hicho kiliniumiza, kama unavyojua maisha ya mchezaji  anapopata timu ya kumsajili anapata pesa ya kufanya kitu cha maana” anasema Masai na kuongeza;

“Kwa sasa najiona sina deni ikitokea timu inanihitaji naweza nikafanya maamuzi ya kwenda kujiunga nayo, kwani tayari timu imerejea Ligi Kuu.

“Jambo linalotakiwa kufanyika kwa msimu huu kama wachezaji wa Mtibwa ile nguvu tuliyoitumia kuipambania timu isishuke na ikashuka tuizidishe mara mbili, naamini itatusaidia katika msimamo wa ligi tuwe nafasi za juu.”

MASA 04

NAHODHA MTUNZA SIRI

Masai anazungumzia majukumu ya unahodha hayaishii katika kuvaa beji pekee, bali anapaswa kutunza siri za wachezaji na kujenga daraja la umoja baina yao na uongozi.

“Kuna wakati mchezaji mwenzako anaweza akafanya tukio unaloliona anaweza akafukuzwa na ukiangalia ana familia nyuma inayomtegemea, utalazimika kuongea na uongozi ili kumpa nafasi nyingine na kupewa adhabu ndogo,” anasema Masai na kuongeza;

“Imewahi kutokea tukio gumu siwezi kulifafanua nikiwa Mtibwa, timu ilisafiri kwenda Mbeya, baadhi ya wachezaji walibakia kambini na watatu walikuwa wa kikosi B, walifanya vitu vya hovyo ambavyo walitakiwa wafukuzwe moja kwa moja, kocha alikuwa Salum Mayanga nikamuomba nizungumze naye kama mzazi ili awasamehe na alinielewa.

MASA 05

“Nikamwambia kocha ukiwafukuza angalia familia zao zinazowategemea, naomba wapewe adhabu nyingine, akaniruhusu nikaongee na uongozi nao ukanielewa, hivyo adhabu yao wakakatwa mshahara, ukiondoa suala la wanawake yapo matukio mengine ya hovyo walifanya.”

Mbali na hilo, anasema timu inapotokea kufanya vibaya, uongozi unaanza kumuuliza nahodha, hivyo kama ni mtu ambaye hawezi kubeba madhaifu ya wengine ni ngumu kufanikiwa.

“Nyakati nyingine ngumu nikiwa nahodha timu iliposhuka, iliniumiza wakati huo huo nilipata ofa nyingi za timu za Ligi Kuu na niliahidiwa kibunda cha maana, ila nilijua kuna maisha baada ya hilo, nilijifunza unapoondoka katika timu uache amani itakayokusaidia wakati mwingine kurejea tena,” anasema.

MASA 03

MTIBWA INAINGIA MOYONI

Anasema asilimia kubwa ya wachezaji walioichezea Mtibwa kwa muda mrefu, imewaingia moyoni na alilishuhudia hilo wakati wanapambania isishuke daraja 2023/24 na kwa bahati mbaya ikashuka, alipata ushirikiano kwa wachezaji waliowahi kuichezea.

“Ukiachana na wachezaji wa zamani kama Kocha Mecky Maxime wa Mbeya City, Zuberi Katwila kocha wa Geita Gold, Abdallah Juma mchezaji wa zamani na wengine wengi walikuwa wanafika uwanjani na kuangalia tunavyocheza na kutuuliza kuna shida gani ili tusaidiwe timu irejeshe heshima yake,” anasema Masai na kuongeza;

“Kwa wachezaji wa sasa kuna Baba Ubaya, Salum Kanoni, Salum Kihimbwa, kwa kifupi ni wengi walikuwa wanaumizwa na mwenendo wa timu.”

MASA 02

MATUKIO YA HUZUNI

Anasimulia matukio yaliyowahi kumuachia alama ya maumivu ni kifo cha babu yake aliyemtaja kwa jina la Masai na cha mchezaji mwenzake Idd Mobby.

“Wakati napokea taarifa za kifo cha babu tulikuwa tunajiandaa kwenda kucheza na Yanga Juni 6, 2022 kocha Mayanga aliniambia nategemewa katika mechi hiyo, mimi ni mwanamume napaswa kujikaza na kumwombea dua, hiyo mechi tulifungwa bao 1-0 la Denis Nkane.

“Miaka miwili iliyopita alifariki rafiki yangu Mobby, nakumbuka alikuwa anafanya mazoezi ya kukimbia barabarani ili kujiandaa na mechi inayofuata kwani mechi ya siku hiyo hakupangwa, hivyo alijipanga baada ya mazoezi hayo aje uwanjani ila kwa bahati mbaya hilo halikutimia tukaambiwa yupo hospitali, kikafuata kifo cha ghafla.”

Mbali na hilo, anawataja wachezaji aliyokuwa anawatazama kama mfano katika nafasi yake ni beki wa zamani wa Azam FC, Agrey Morris na Salum Mbonde aliyewahi kuzichezea Mtibwa na Simba.

“Mbonde alikuwa anatumia akili kubwa na siyo nguvu, lakini Agrey hata washambuliaji hawakuwa wanapiti hovyo mbele yake ilikuwa kazi kazi, wakati nipo Azam B walikuwa wanasema mimi ni Agrey mpya,” anasema.

Masai anasema kwa washambuliaji, kabla ya kuondoka kwa aliyekuwa staa wa Yanga Fiston Mayele anayekipiga Pyramids, ndiye alikuwa hatari kwa mabeki kwa upande wake.

“Kipindi hicho Mayele akiwa uwanjani asipofunga ni bahati mbaya, lakini alikuwa mtu anayeumiza akili za mabeki, kwa sasa ninayemkubali ni Prince Dube hatumii nguvu ila uwanjani anapatikana maeneo mengi ili umzuie inatakiwa ufiti na pumzi,” anasema Masai aliyeitaja mechi ambayo hataisahau akiwa Geita Gold walifungwa mabao 5-0 na Simba.

Masai aliyeanza kucheza Ligi Kuu msimu wa 2019/20 alipopandishwa Azam FC akitokea kikosi B, anasema soka limempa hatua lakini hawezi kuyaweka wazi mambo aliyoyafanya kupitia kazi hiyo.

“Azam itasalia katika kumbukumbu za maisha yangu, kwani ndiko nilikoanzia kucheza Ligi Kuu pia ina miundombinu ambayo mchezaji anapata kila kitu kinachotakiwa, hivyo akifanya kosa ni yeye na wala si viongozi,” anasema Masai anayeamini bado ana nafasi ya kuichezea Taifa Stars.

MASA 01

KUHUSU MAVAZI

Anasema ingawa hajaweka nguvu katika nguo za fasheni, mara moja moja akiamua anatafuta mikato ya kushitua.

“Kuna kipindi niliwahi kupata maoni mengi ya wachezaji wenzangu katika mtandao wa Instagram niliposti picha niliyovaa pensi la jinzi lilikuwa bwanga na mikato fulani hivi ya kiatu cha kinyamwezi,” anasema mchezaji huyo.