Prime
Mayele na Congo wanapokutana na Ronaldo, kama zali
GHAFLA sana Fiston Mayele na rafiki zake Wacongo watakuwa wakizurura hewani kutoka mji mmoja kwenda mwingine kule Canada, Marekani na Mexico kucheza mechi za fainali ya Kombe la Dunia. Ni ukweli usioeleweka.
Congo wapo Kundi moja na Cristiano Ronaldo. Wapo na Ureno na wengineo. Wamejikutaje hapo? Mara ya mwisho walicheza fainali hizo mwaka 1974 pale Ujerumani wakitambulika kama Zaire. Waliambulia aibu. Mechi dhidi ya Yugoslavia walichapwa mabao 9-0.
Hata hivyo, leo wamejikuta tena kombe la dunia. Shukrani kwa Arsene Wenger na genge lake. Wenger kwa sasa yupo Fifa kutengeneza mipango kama hii ya kulifanya kombe la dunia lijalo kuwa na timu 48. Ni Wenger tu, hakuna mwingine. Namfahamu. Alikuwa kocha wangu Arsenal.
Kwa akili zao hatimaye Afrika imepata timu 10 katika michuano ya kombe la dunia. Nyingi kati ya hizi hazistahili. Zinakwenda katika michuano hii kwa sababu Wenger na wenzake wametanua goli. Wametaka timu nyingi zishiriki kombe la dunia. Siyo tu kutoka Afrika bali na kwingineko.
Kina Jordan, Curacao, Panama, New Zealand nao pia watakuwepo katika kombe la dunia. Shukrani kwa mipango ya kina Wenger na genge lake. Hata huku Afrika kuna timu ambazo zimejichokea lakini zitakuwepo kombe la dunia.
Mfano Ghana wamebakia jina tu lakini wamekwenda kombe la dunia. Walikuwa hoi kweli kweli kiasi cha kushindwa kufuzu Kwenda kombe la mataifa ya Afrika lililofanyika Morocco lakini wamekwenda kombe la dunia.
Cape Verde nao walikuwa hoi kweli kweli kiasi cha kushindwa kufuzu kombe la mataifa ya Afrika pale Morocco lakini Mungu Saidia wamefuzu Kwenda kombe la dunia. Mchujo mkali wa timu tano wakati ule ulikuwa hauwezi kuwapitisha kina Cape Verde.
Kuna wababe wa Afrika ambao walikuwa na misuli ya kwenda kombe la dunia kama timu zingekuwa chache. Kwa mfano kama mchujo ungetuleta katika pambano la Morocco na Cape Verde ni wazi Cape Verde isingekwenda. Hata hivyo, mchujo ulikuwa hautuleti katika mechi hizo.
Ni kweli njiani Congo ilimtoa Cameroon kwenda katika pambano la mtoano ambalo lilimkutanisha na mchovu mwingine Jamaica. Kama pambano lingekwenda kati yao na Colombia sidhani kama ingefuzu.
Lakini hata Cameroon ambayo ilitolewa na Congo katika kufuzu nayo imechoka. Leo inamtegemea beki kama Che Malone Fondo katika safu yao ya beki. Wametoka kule kwa kina Rigobert Song, Raymond Kala, Geremi Njitap, leo wapo kwa Che Malone.
Kibiashara ni michuano mizuri. Wengi wanashiriki. Kombe la dunia litakuwa na mechi nyingi. Wasiwasi wangu ni yale matokeo ya Yugoslavia na Zaire yanaweza kujirudia. Inaweza isiwe kwa Congo lakini inaweza kuwa kwa vibonde wengine ambao wamepata fursa ya kushiriki michuano hii kwa sababu kina Wenger wametanua lango.
Baada ya michuano hii kumalizika kina Wenger watakuwa wamepata taswira nyingine. Sijui kama watarudi katika idadi ya timu 32 kama awali au watatuacha hapo hapo. Sijui. Baada ya michuano kumalizika watakuwa wamejifunza kitu.
Kama kuna timu ndogo zitafanya maajabu basi nadhani kina Wenger wanaweza kuendelea na wazo hili la timu 48. Kama kuna aibu nyingi zitatokea basi wanaweza kurudisha wazo lao la muundo wa zamani. Kombe la dunia lina hadhi yake. linahitaji kuchezwa katika viwango vya juu.
Huku Afrika pia kuna timu ambazo zilikuwa zinapata shida kufuzu mpaka CAF walipoamua kubadilisha muundo kutoka timu 16 kwenda timu 24. Hakuna kificho, Taifa Stars ni miongoni mwa timu ambazo zilinufaika na muundo mpya.
Mara ya mwisho walifuzu mwaka 1980. Baada ya muundo kubadilishwa mpaka timu 24 sasa hivi wamekuwa wakifuzu mara kwa mara na juzi tu walikuwepo Morocco. Uzuri ni timu ndogo za Afrika zimeanza kuleta ushindani katika michuano ya mataifa ya Afrika.
Kila la kheri kwa Congo katika michuano hii. Kuna mechi ambayo watacheza dhidi ya Ureno na kukutana na Ronaldo. Kukutana pia na kina Bernardo Silva, Bruno Fernandes, Joao Felix na wengineo. Acha tuone wanavyoikimbilia jezi ya Ronaldo mpira ukiisha.
Kwa Africa nawategemea zaidi Morocco. Wana kitu. Hata kombe la dunia lililopita pale Qatar walionyesha kitu. Najua baada ya kile kilichotokea katika michuano ya Afcon iliyopita watu wengi wa bara hili wameichukia Morocco lakini ukweli unabakia ni miongoni mwa timu chache za Afrika zenye misuli katika kombe la dunia.
Wengine ni Senegal wenye Sadio Mane. Wana watu ambao unaweza kuwatuma kwenda kwenye kombe la dunia na wakafanya jambo. Wana wachezaji wazoefu na wanaocheza katika ligi ngumu Ulaya.
Lakini rafiki zangu kama Tunisia, Afrika Kusini, Algeria wana timu za kawaida tu. Wamepenya kwa sababu tu ya muundo wenyewe. Mpira wa Afrika pia kwa kiasi fulani umeshuka na ndiyo maana hata michuano ya mataifa ya Afrika inakuwa migumu kwa wakubwa.
Tusubiri na kuona. Huenda kuna ambao watatuonyesha maajabu. Acha tusubiri pia pambano la Ronaldo na Mayele. Litaakisi kama kweli hii ni michuano ya kombe la dunia au? Baadaye kina Wenger watapata majibu na watakaa katika kikao kuamua kama kweli maamuzi yao yalikuwa sahihi.