MetLife ilivyothibitisha uhusiano wa Cubarsi na Martina Riera
Muktasari:
- Cubarsi na Martina walisherehekea pamoja baada ya Hispania kutwaa taji la michuano hiyo kwa mara ya pili kwa kuifunga Argentina goli 1-0 huko New York, Marekani.
Katikati mwa dimba la MetLife ilipopigwa fainali ya Kombe la Dunia 2026, ndipo mchezaji wa Hispania, Pau Cubarsi, 19, alithibitisha uhusiano wake na Martina Riera baada ya tetesi za muda mrefu.
Cubarsi na Martina walisherehekea pamoja baada ya Hispania kutwaa taji la michuano hiyo kwa mara ya pili kwa kuifunga Argentina goli 1-0 huko New York, Marekani.
Beki huyo wa kati anayeitumikia klabu ya FC Barcelona, alikuwa na msaada mkubwa kikosi cha Hispania ambacho kilimaliza michuano hiyo kikiwa kimeruhusu goli moja pekee katika mechi nane walizocheza.
Kwa ujumla Cubarsi alionyesha kiwango kizuri katika fainali hizo hadi kuja kushinda tuzo ya Mchezaji Bora Kijana mbele ya Lamine Yamal aliyekuwa akitajwa na wengi.
Baada ya Hispania kutwaa taji hilo, Cubarsi alisherehekea akiwa na familia yake huku pembeni yake akiwepo Martina, msichana ambaye amekuwa akivikwepa vyombo vya habari ili kujiepusha na presha inayowakumba wapenzi wa wanasoka maarufu.
Furaha ya ushindi huo iliwafanya wawili hao kuweka kando usiri wa uhusiano wao walioutunza kwa muda mrefu, na hatimaye kamera zikawanasa wakibusiana juu ya nyasi za uwanja wa MetLife unaochukua mashabiki 82,500.
Tukio hilo ambalo liliteka mazungumzo katika mitandao ya kijamii, ndio uthibitisho rasmi na wa wazi zaidi kwamba wawili hao ni wapenzi. Tetesi za kuwa pamoja zilianza mwaka uliopita walipoonekana pamoja wakifurahia maisha nchini Ugiriki.
Ilipofika Mei 2026, baada ya Barcelona kutwaa ubingwa wa La Liga, Cubarsi aliposti picha kwa mara ya kwanza akiwa na Martina kwenye uwanja wa Camp Nou. Picha hiyo iliyokuwa katikati ya nyingi iliwaonyesha wawili hao wakiwa wameshikilia kombe.
“Sisi ni mabingwa wa Ligi!. Sasa ni wakati wa kusherehekea juhudi na kazi kubwa tuliyoifanya katika msimu mzima,” aliandika Cubarsi katika posti hiyo.
Siku chache baadaye walionekana tena pamoja katika hafla ya chakula cha jioni ya kuwapongeza wachezaji wa Barcelona kwa kumaliza msimu wa mashindano vizuri.
Ikumbukwe katika hafla hiyo ndipo pia na mchezaji mwenzake, Lamine Yamal alionekana hadharani kwa mara ya kwanza akiwa na mpenzi wake mpya, Ines Garcia ambaye ni mwanamitindo wa Hispania.
Hata hivyo, matukio hayo hayakutosha kutoa uthibitisho wa moja kwa moja kama Cubarsi na Martina ni wapenzi au marafiki, lakini tukio lao la MetLife limejibu maswali yote muhimu ambayo mashabiki walikuwa wakijiuliza kwa muda mrefu.
Inaelezwa kuwa Cubarsi na Martina wanafahamiana tangu utotoni, urafiki wao wa muda mrefu umeendelea kukua hadi kuwa uhusiano wa kimapenzi. Katika Kombe la Dunia 2026, wawili hao ni miongoni mwa ‘kapo’ ambazo zimewavutia mashabiki wengi.
Wote wawili walizaliwa Estanyol, mtaa mdogo uliopo Girona, ambao una wakazi wasiozidi 200. Katikati ya maisha ya kawaida, Cubarsi akawa mtu mwingine kabisa baada ya kujiunga na akademi ya Barcelona (La Masia), hatua iliyomfungulia njia ya kuwa mchezaji maarufu duniani.
Kuhusu Martina Riera, bado haijafahamika iwapo bado anasoma au anaishi wapi, kwani amekuwa akilinda maisha yake binafsi.
Hata hivyo, baada ya kuonekana hadharani akisherehekea ushindi pamoja na Cubarsi, matarajio ya mashabiki wengi duniani ni kwamba yombo vya habari na mitandao mikubwa itaanza kufuatilia kwa karibu zaidi maisha yake.
Na licha ya umaarufu wa Cubarsi kuzidi kuongezeka kwa kasi, ameendelea kuishi maisha ya kawaida, inaelezwa kuwa anaishi katika nyumba moja jijini Barcelona pamoja na dada yake mkubwa aitwaye Irene, kitu kinachomfanya kuzidi kuwa na nidhamu ya kazi.
Anapopata muda wa kupumziko hupenda kupika, kutazama mechi za Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) na Ligi Kuu ya England, kucheza michezo ya video au kufuatilia vipindi vya televisheni.
Pia anaendelea na masomo ya Shahada ya Usimamizi wa Biashara (Business Administration and Management), hivyo maisha yake ni uwanjani na darasani.
Ikumbukwe Cubarsi alicheza mechi yake ya kwanza rasmi akiwa na kikosi cha kwanza cha Barcelona Januari 18, 2024, katika mchezo wa Kombe la Mfalme dhidi ya Unionistas de Salamanca. Aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Andreas Christensen, ikiwa ni siku chache kabla ya kutimiza miaka 17.
Siku tatu baadaye alicheza mechi yake ya kwanza ya La Liga dhidi ya Real Betis kwenye Uwanja wa Benito Villamarin.
Kuanzia hapo, maendeleo yake yalikuwa makubwa na chini ya kocha Xavi Hernandez, alijijengea nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza akimaliza msimu wa 2023/24 akiwa amecheza mechi rasmi 24.
Alijitangaza zaidi barani Ulaya katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Napoli, ambapo alianza kikosi cha kwanza, akawa beki mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kuichezea Barcelona katika mashindano hayo na kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi.