Muda umetujibu kwa Doumbia, Boyeli
Muktasari:
- Wasifu wao wa kile walichokifanya siku nyingi nyuma uliimbwa sana kuliko kile ambacho walikifanya muda mfupi kabla ya kujiunga na Yanga ambayo iliwaona ni wachezaji ambao wataongeza kitu kikubwa katika kikosi chao.
SAJILI mbili ziliimbwa sana wakati wa kipindi cha dirisha kubwa la usajili ambazo ni za wachezaji Andy Boyeli na Mohamed Doumbia.
Wasifu wao wa kile walichokifanya siku nyingi nyuma uliimbwa sana kuliko kile ambacho walikifanya muda mfupi kabla ya kujiunga na Yanga ambayo iliwaona ni wachezaji ambao wataongeza kitu kikubwa katika kikosi chao.
Doumbia alisajiliwa baada ya kufanya majaribio Yanga kwa miezi kadhaa. Kukawa na wasiwasi kwamba huyu mchezaji kama ana uwezo kwa nini hana timu hadi amekuja kusaka fursa kwa kutegemea majaribio hapa Bongo.
Kijiwe kikajibiwa kwamba jamaa ana kipaji kikubwa sana na ameamua tu kusaka changamoto mpya Tanzania. Maana alikuwa anacheza soka la kulipwa Ulaya.
Mwingine ni Boyeli aliyetokea Sekhukhune FC ya Afrika Kusini. Wote tunajua namna wachezaji wa nafasi ya mshambuliaji wa kati walivyo adimu kwa miaka ya hivi karibuni, ikatupa tafakari mbona ametolewa kwa mkopo.
Maana yake kama angekuwa mshambuliaji hatari, wale Sekhukhune wasingemtoa tena kwa mkopo. Sio jambo jepesi kwa timu kumtoa kwa mkopo straika wake tegemeo.
Lakini tukatulizwa na takwimu za kile alichokifanya wakati alipokuwa katika Ligi Kuu ya Zambia ili kuaminishwa ni straika tishio badala ya tathmini ya kile alichokifanya Afrika Kusini.
Mwisho wa siku, muda umekuwa hakimu wa haki katika kutupa ukweli kama Doumbia na Boyeli walikuwa usajili mzuri ama hakuwa mzuri kwa Yanga kwani wakiwa hata hawajafikisha mwaka tangu wasajiliwe, klabu hiyo inataka kuachana nao. Boyeli mkataba wake wa mkopo Yanga utakatishwa na anarejea Sekhukhune na Doumbia inasemekana atatolewa kwa mkopo kupelekwa Singida Black Stars. Muda umeshatoa majibu.