Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mundi: Ngumi zimenifungulia fursa Ujerumani

MUNDI Pict

Muktasari:

  • Katika mahojiano na Mwanaspoti, Kiboko ya Wabishi anasema alikwenda Ujerumani mwaka 2025 kwa mambo mawili; kupigana ngumi na kazi ya kusambaza bidhaa za wateja wa mtandaoni katika kampuni moja ambapo anachokifanya anapewa ramani na kuwapelekea wateja vitu vyao.

BONDIA Said Mundi ‘Kiboko ya Wabishi’ anayepigana uzani wa kilo 69 baada ya kuona Ujerumani kuna fursa ya kumuingizia kipato, hakusita kwenda kupambana ili kuhakikisha anajiweka imara kiuchumi kabla ya nguvu ya kutafuta haijamuisha.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, Kiboko ya Wabishi anasema alikwenda Ujerumani mwaka 2025 kwa mambo mawili; kupigana ngumi na kazi ya kusambaza bidhaa za wateja wa mtandaoni katika kampuni moja ambapo anachokifanya anapewa ramani na kuwapelekea wateja vitu vyao.

“Maisha yanahitaji kujitoa na kuthubutu, kama unavyojua kazi ya ngumi huwezi kupigana muda wote, kuna wakati unaweza ukachoka, ndiyo maana nikiwa bado kijana nikiona fursa ya kunipa pesa lazima nitaifanya, bidii, nidhamu na kujitambua ndivyo vinavyonipa mafanikio na hatua ya kimaisha,” anasema.

MUN 01

SHERIA YA UJERUMANI

Anasema ukifika katika nchi hiyo, lazima mgeni akae miezi sita ndipo anaweza akaruhusiwa kuanza kufanya kazi za kumuingizia kipato cha kujikimu na maisha, lakini kuna masharti ambayo lazima upewe na serikali.

“Jambo la kwanza lazima kazi utafute mwenyewe, ukiipata unapewa mkataba kisha unakwenda serikalini nao ili waukague ndipo wakuruhusu kuendelea na majukumu,” anasema bondia huyo na kuongeza:

“Kabla ya kuruhusiwa kufanya kazi, wanafanya ukaguzi wa mchakato wa njia gani ulitumia kuingia nchini kwao, jambo lingine lazima wakupime afya yako kwa kina, wakiona kila kitu kipo sawa basi unakuwa huru kuendelea na majukumu yaliyopo kwenye mkataba wako.”

Anasimulia safari yake ya kwenda Ujerumani, alipata mwaliko kutoka kwa bondia wa nchini humo ambaye ni rafiki yake, hivyo ikawa rahisi kwake kupata viza kirahisi, nje na hapo anakiri ingekuwa ngumu.

MUN 03

“Unapofika katika nchi hiyo sharti la kwanza lazima usome lugha yao ya Kijerumani, ambapo kwa upande wangu hadi sasa nina miezi minne tangu nianze kusoma, kwani Kiingereza kinazungumzwa maeneo machache sana, inayotumika kila sehemu ni lugha yao,” anasema na kuongeza:

“Nina uwezo wa kuzungumza hilo linanisaidia zaidi kwenye majukumu yangu, hasa katika kuwasiliana na wateja, vinginevyo ingekuwa changamoto.”

Ili aanze kucheza ngumi anasema, lazima akae miaka miwili awe na bima ya afya na vipimo vinavyomuonyesha hana changamoto yoyote.

“Nimevuka mitihani hiyo nimepimwa nipo salama kiafya, nimeishapata bima hivyo naweza nikaendelea na majukumu yangu kama kawaida, huku wenzetu ngumu kuruhusiwa kupanda ulingoni bila kujua utimamu wako wa mwili, wanahakikisha kila kitu kipo sawa.” anasema.

Kuhusu maisha, anasema: “Kupanga chumba kwa mwezi gharama yake ni Sh2.4 milioni kwa pesa za Kitanzania, wakati chakula matumizi ya kujibana kwa siku ni Sh90,000. Ndiyo maana wenzetu huku wanajali sana muda na kufanya kazi nyingi kwa siku.”


MUN 02

ALIVYOANZA KUPIGANA NGUMI

Anasema tangu aanze kucheza ngumi za kulipwa 2011, asilimia kubwa maisha yake yaliendeshwa na mchezo huo.

“Nipo Ujerumani kwa sababu ya ngumi, maana aliyenipa mwaliko ni bondia, hivyo kwa asilimia kubwa nimefanya vitu vingi vya maendeleo siwezi kuanza kuvitaja kimoja baada ya kingine,” anasema bondia huyo.

Anasema mchezo wa ngumi kwa sasa ni ajira kamili ya vijana, kubwa ni kujitambua na kuonyesha utofauti kwa jamii inayodhani bondia anaweza akawa mhuni.

MUN 04

“Ngumi zimenikutanisha na watu wengi na kunipa wepesi kufanya baadhi ya vitu, kuna nchi nimefika kama Uingereza kupitia mchezo huo, binafsi kwangu mimi ni mchezo ulionipa heshima kubwa,” anasema bondia huyo na kuongeza:

“Bondia anavyojiweka ndivyo jamii inavyoweza kumtafsiri, lakini ni mchezo wenye heshima zake, kama ambavyo ipo kwenye mpira wa miguu vijana kuonyesha vipaji vyao iwe hivyo kwenye ngumi.” Anasema kabla ya kuchagua ngumi kuwa ajira yake, alijaribu kucheza mpira wa miguu, alipoona itakuwa ngumu kupata mafanikio akaachana nao.

“Nimecheza sana mpira wa miguu ngazi za chini, lakini sikuona kama ni ajira ambayo ingefanya niendeshe maisha yangu, nilikuwa nacheza nafasi zote kasoro kipa,” anasema.


MUN 05

MABONDIA WAKE BONGO

Anasema kwa sasa mabondia anaowakubali kwa sasa nchini Tanzania ni Hassan Mwakinyo ukiachana na ubora wake ulingoni, lakini anaonyesha namna ambavyo amepiga hatua ya maisha na pia ni mtu smati anayepaswa kuigwa na vijana wengi.

“Mabondia wengine ninaowakubali ni Fadhili Majiha, Ibrahim Mafia, Yohana Mchanja,Yusuf Changalawe, Ibrahim Class hawa jamaa ni mafundi, naamini mabondia waliocheza nao wanajua kazi zao, binafasi nawakubari.” anasema.


HIZI HAPA TAKWIMU

Kwa mujibu wa rekodi za BoxRec, amecheza mapambano 40, akishinda 29, akipoteza 10 na kutoka sare moja, Mei, 2025 alipigwa na Adel El Garmaoui  pambano lilifanyika Alte Kongresshallen, Munich, Bayern, Novemba 2024, alishinda dhidi ya Jay Jay Ngotiko (Mkwakwani Tanga), Januari 2024, alishinda dhidi ya Salehe Maafuzu (Mkwakwani, Tanga).

Mengine ni Januari 2023 alishinda mbele ya Bakari Dunda (CCM Mkwakwani, Tanga), Januari 2023 alimpiga Selehe Mahfudh (Mkwakwani, Tanga), Mei 2022 alipigwa  na Mateusz Polski (Gdanski Teatr Szekspirowski, Gdansk), Januari 2022 alishinda mbele ya Bakari Dunda (Tate Plus Hall, Tanga), Aprili 2021, alipigwa na Albano Clement (Ubungo Plaza, Dar es Salaam), Machi 2020 alishinda dhidi ya Bakari Dunda (Mkwakwani, Tanga) na Januari 2020 alimshinda Hassan Mgaya katika Uwanja wa Mkwakwani mjini  Tanga.

Novemba 2019 alipigwa na Yaser Yuksel (EMKA Sportzentrum, Velbert, Nordrhein-Westfalen), Oktoba 2018 alimshinda Mustapha Dotto (Mkwakwani, Tanga) na Oktoba 2018 alimpiga Bakari Dunda kwenye huko Jitegemee mkoani Tanga.