MWIGULU NCHEMBA: Mwanayanga aliyemrithi Majaliwa
Muktasari:
- Mwigulu ambaye ni Mbunge wa Iramba Magharibi Mkoa wa Singida, anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Kassim Majaliwa aliyeitumikia nafasi hiyo kwa miaka 10 mfululizo kuanzia mwaka 2015 hadi 2025.
NI Mwigulu Lameck Nchemba. Ndio, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemteua Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu mpya. Mwigulu anakuwa Waziri Mkuu wa 14 tangu taifa lipate uhuru.
Jina la Mwigulu limewasilishwa bungeni saa 3:06 asubuhi ya leo Alhamisi na mpambe wa Rais kwa Spika wa Bunge, Mussa Zungu, kisha kusomwa kwa wabunge ambao baadaye walimthibitisha kwa kura.
Mwigulu ambaye ni Mbunge wa Iramba Magharibi Mkoa wa Singida, anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Kassim Majaliwa aliyeitumikia nafasi hiyo kwa miaka 10 mfululizo kuanzia mwaka 2015 hadi 2025.
Majaliwa ambaye naye alikuwa mwanamichezo na shabiki wa Simba, akiwa na taaluma ya ukocha wa soka, amemuachia kijiti Mwigulu ambaye naye ni mwanamichezo, akiwa pia ni mwanachama wa Yanga. Mbali na uanachama, Mwigulu pia ni mmoja wa Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa klabu hiyo kongwe nchini.
Pia Mwigulu ni mlezi wa Singida Black Stars, timu inayoshiriki Ligi Kuu Bara ikiwa imefuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kabla ya hapo, Mwigulu amewahi kuwa Rais wa Singida United, timu iliyowahi kushiriki Ligi Kuu Bara msimu wa 2017–2018, 2018-2019 na 2019–20.
Katika kudhihirisha uanamichezo wake, Oktoba 5, 2025 kwenye Viwanja vya Bombadia, Singida Mjini kulikofanyika sherehe za kuipongeza Singida Black Stars kwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame 2025, alisema: “Ninajisikia fahari kusema mimi ni mlezi wa Singida Black Stars.”
Mwigulu aliendelea kwa kusema: “Mambo makubwa zaidi yanakuja, hili ni kombe la kwanza, tunaliangalia la ligi na shirikisho, vikombe vingine vitakuja kwa sababu nimeona benchi la ufundi limejipanga vizuri, wachezaji hali ya kujiamini ipo vizuri sana na mkoa unatoa motisha nzuri, hii yote inatia matumaini kwamba vikombe vinakuja.”
Wakati wa uzinduzi wa bajeti ya michezo mwaka 2022, Mwigulu akiwa Waziri wa Fedha, alinukuliwa akisema: “Michezo si burudani tu, ni uchumi, ni ajira, ni diplomasia. Tutahakikisha vijana wanapata mazingira ya kustawi kupitia michezo.”
ANAVYOZI SAPOTI KLABU
Mwanzoni mwa msimu huu, Simba ilimsajili mshambuliaji Jonathan Sowah, akitokea Singida Black Stars, timu aliyoitumikia kwa takribani miezi sita tu akifunga mabao 13 katika Ligi Kuu Bara.
Akizungumzia usajili wa Sowah ndani ya Simba, Mwigulu alisema: “Unajua mimi ni mlezi wa klabu zote, wakati huo usajili unafanyika, serikali ilikuwa bado kazini, wakati serikali ikiwa kazini, Simba nao waziri wao wa fedha nilikuwa mimi huyuhuyu, kwa hiyo mimi kama mdau tukazungumza tuiunge mkono na yenyewe ifanye vizuri kwenye mashindano ya kimataifa. Tukawaachia Sowah.”
ALIVYOMPELEKA FEI TOTO YANGA
Julai 12, 2018, Singida United ilitangaza kumsajili Feisal Salum ‘Fei Toto’ saa 5 asubuhi, lakini ilipofika saa 10 jioni, Yanga iliita vyombo vya habari na kumtambulisha kama mchezaji wao ikidai kufuata taratibu zote.
Kwa mujibu wa Mwigulu ambaye wakati huo alikuwa Rais wa Singida United, alisema hakuna mgogoro wa kiusajili kuhusiana na nyota huyo kuhusishwa kusaini mikataba katika timu hizo mbili na kuweka wazi kuwa alitoa ridhaa kwa mchezaji kwenda kusajili na alishakubaliana na viongozi wa Yanga.
“Baada ya kutoa ridhaa kwa mchezaji pia nilifanya makubaliano na viongozi wa Yanga kumpa mkataba mchezaji huyo ambapo makubaliano yangu na uongozi yalikuwa ni kama mchezaji hatakuwa na kiwango cha kubaki Yanga basi watamleta Singida,” alisema Nchemba.
WASIFU WAKE
Mwigulu aliyezaliwa Januari 7, 1975, ni mchumi na mwanasiasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye amekuwa Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi tangu mwaka 2010. Novemba 13, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alimteua kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akichukua nafasi ya Kassim Majaliwa. Kabla ya uteuzi wake wa sasa, aliwahi kuhudumu kama Waziri wa Fedha katika Baraza la Mawaziri la Tanzania tangu Machi 2021.
Kabla ya kuingia kwenye siasa, Mwigulu alifanya kazi kama mchumi katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Baadaye, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete alimteua kuwa Waziri katika Wizara ya Fedha na Mipango ya Uchumi.
Desemba 2015, Rais wa Awamu ya Tano, hayati John Pombe Magufuli, alimteua kuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Kufuatia kifo cha Balozi, Dk Augustine Phillip Mahiga, Mwigulu aliteuliwa kushika wadhifa wa Waziri wa Katiba na Sheria.
Baada ya kuundwa kwa Baraza la Mawaziri la Awamu ya Sita, Machi 31, 2021, ambapo Dk Philip Mpango alipandishwa kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, Mwigulu alichukua nafasi yake kama Waziri wa Fedha na Mipango.
Julai 4, 2023, alibakishwa katika nafasi yake ya Waziri wa Fedha, ingawa majukumu ya Mipango yalihamishiwa chini ya Ofisi ya Rais.
Novemba 13, 2025, baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Mwigulu aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania.