Prime
Barker akaza kamba hatma ya Doumbia
WAKATI mashabiki wengi wakitazama matokeo ya suluhu dhidi ya Mogadishu City katika mchezo wa kwanza wa CECAFA Kagame Cup, kocha wa Simba, Steve Barker anaonekana kuwa na malengo makubwa zaidi ya kushinda mechi za maandalizi, huku akisisitiza anachokifanya ni kuwaingiza wachezaji wapya kwenye falsafa ya timu ili kuelewa mapema aina ya uchezaji unaotakiwa.
Katika wachezaji wapya wa Simba waliosajiliwa dirisha hili kubwa kuelekea msimu wa 2026-2027, yupo mshambuliaji raia wa Mali, Ibrahim Doumbia ambaye alitokea benchi mechi iliyopita ya Kombe la Kagame dhidi ya Mogadishu City, akiingia dakika ya 76 kuchukua nafasi ya Inno Loemba.
Mbali na Doumbia, majembe mapya ya Simba katika usajili wa dirisha hili ni beki wa kulia Nathaniel Chilambo, kiungo wa Nigeria, Ibraheem Jabaar, winga Keletso Makgalwa kutoka Afrika Kusini, kiungo mkabaji Kelvin Nashon na winga Bakari Msimu.
Katika mechi hiyo, wachezaji wapya walioanza kikosini ni Chilambo, Nashon na Msimu ambao baadaye walifanyiwa mabadiliko. Kati ya walioingia kutokea benchi, alikuwepo pia Makgalwa.
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini, anaitumia kambi ya Kigali nchini Rwanda yanapofanyika mashindano ya Kagame kama sehemu ya kuendeleza kile alichofanya msimu uliopita, akianza kuwaingiza taratibu wachezaji wapya katika mfumo wake kabla ya msimu wa 2026-2027 haujaanza ambapo Simba itaanzia kwa kucheza Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, Agosti 12, 2026. Kisha itakabiliwa na mashindano mengine ikiwemo Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la CRDB na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Barker amesema maandalizi ya Rwanda hayalengi tu kupata matokeo, bali kujenga uelewano kati ya wachezaji wapya na wale waliokuwepo, kuhakikisha kila mmoja anaelewa falsafa ya timu kabla ya msimu kuanza.
“Maandalizi yanaendelea vizuri. Tunataka kila mchezaji aelewe mfumo wetu wa uchezaji, namna tunavyotaka kujilinda, kushambulia na kubadilika haraka tunapopoteza mpira. Hiki ni kipindi cha kujenga timu, si kuangalia matokeo pekee,” amesema Barker.
Kocha huyo pia anaamini usajili uliofanywa umeongeza ushindani mkubwa ndani ya kikosi, jambo ambalo litamlazimu kila mchezaji kupigania nafasi yake.
“Tulihitaji kuongeza ubora katika baadhi ya maeneo. Wachezaji wapya wana uwezo tofauti na kila mmoja ataleta kitu kipya ndani ya timu. Sasa ushindani wa nafasi utakuwa mkubwa na hilo litatusaidia kuongeza kiwango cha timu.”
Miongoni mwa wanaotarajiwa kuvutia macho ni Jabaar ambaye tayari anaifahamu vizuri falsafa ya Barker baada ya kufanya naye kazi Stellenbosch, Makgalwa anayejulikana kwa kasi na uwezo wa kutengeneza nafasi, pamoja na Doumbia anayewasili akiwa na sifa ya ufungaji kutoka Mali.
Leo Simba itakuwa na nafasi nyingine ya kuonyesha hatua ya maendeleo itakapokutana na Jamus SC ya Sudan Kusini, timu iliyofanya vizuri katika mchezo wake wa kwanza kwa kuifunga Singida Black Stars mabao 2-0.
Hivyo, Barker atatumia mchezo huo kupima kama maandalizi ya wiki za mwanzo yanaanza kuzaa matunda huku akitarajiwa kuwapa dakika zaidi baadhi ya nyota wapya ili kuongeza maelewano ndani ya kikosi.
Akizungumzia namna ambavyo Simba iliwapa upinzani mkubwa katika mchezo wa kwanza wa CECAFA Kagame Cup, kocha wa Mogadishu City, Dadir Amin Ali amesema walikutana na wakati mgumu hasa eneo la kiungo ambapo aliwataja baadhi ya wachezaji walioonekana kuwa tishio kwa timu yake.
Amesema kiungo Hussein Daudi Semfuko alikuwa miongoni mwa wachezaji waliowasumbua zaidi kutokana na uwezo wake wa kuunganisha mchezo na kuisukuma Simba mbele mara kwa mara. Kwa mujibu wa kocha huyo, timu yake ililazimika kufanya kazi kubwa kumdhibiti katika dakika nyingi za mchezo. “Nilimuona kuwa ni mchezaji hatari pale kati, alitupa wakati mgumu na kazi ilikuwa ngumu zaidi kwetu kipindi cha pili walipoongeza presha kubwa, hasa kwa wachezaji walioingia akiwemo mmoja aliyekuwa akicheza pembeni (Keletso), pamoja na mshambuliaji wao mmoja ambaye aliingia alikuwa mwenye nguvu na kasi (Doumbia),” amesema Ali.