Simba, Singida Black Stars kusaka ushindi tu
Muktasari:
- Singida Black Stars ndiyo itakuwa ya kwanza kushuka Uwanja wa Kigali Pele saa 10:00 jioni kumenyana na Mogadishu City ya Somalia, ikisaka kufufua matumaini ya kutetea ubingwa wao baada ya kuanza vibaya kwa kufungwa mabao 2-0 na Jamus FC ya Sudan Kusini.
BAADA ya kuanza kwa matokeo yasiyoridhisha, wawakilishi wa Tanzania Bara, Simba na Singida Black Stars, leo wanarejea dimbani kusaka ushindi wa kwanza katika michuano ya CECAFA Kagame 2026 inayoendelea jijini Kigali, Rwanda.
Singida Black Stars ndiyo itakuwa ya kwanza kushuka Uwanja wa Kigali Pele saa 10:00 jioni kumenyana na Mogadishu City ya Somalia, ikisaka kufufua matumaini ya kutetea ubingwa wao baada ya kuanza vibaya kwa kufungwa mabao 2-0 na Jamus FC ya Sudan Kusini.
Baadaye saa 1:00 usiku, Simba itaikabili Jamus FC ikiwa na lengo la kuondoa presha ya sare ya bila mabao dhidi ya Mogadishu City katika mchezo wake wa kwanza. Wekundu wa Msimbazi wanahitaji ushindi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele.
Kocha wa Simba, Steve Barker, amesema kikosi chake kilitengeneza nafasi nyingi katika mchezo wa kwanza lakini kilikosa umakini wa kuzitumia na kusisitiza kuwa makosa hayo hayatarudiwa dhidi ya Jamus.
“Tulitawala sehemu kubwa ya mchezo lakini hatukutumia nafasi tulizozipata. Tunapaswa kuwa makini zaidi mbele ya lango ili kuwa na makali zaidi ambayo tunahitaji kwa ajili ya msimu ujao,” amesema Barker.
Kwa upande wa Singida Black Stars, kocha Papy Okitankoyi Kimoto, amesema kipigo dhidi ya Jamus kimewapa somo na tayari wamefanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza, akiamini wachezaji wake wataonyesha utofauti dhidi ya Mogadishu City.
“Bado tuna nafasi ya kupambana. Tumefanyia kazi makosa yetu na naamini wachezaji wataingia uwanjani wakiwa na ari na nidhamu kubwa zaidi. Tunahitaji ushindi ili kurejesha matumaini yetu kwenye mashindano,” amesema.
Matokeo ya michezo hiyo yanaweza kuwa na mchango mkubwa katika hatima ya timu hizo mbili za Tanzania, kwani ushindi utazifanya ziendelee kuwa na matumaini ya kutinga hatua ya mtoano huku matokeo mengine yasiyo mazuri yakiongeza ugumu wa safari yao katika CECAFA Kagame 2026.