Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mzuka umerudi upya Mapinduzi Cup

MAPINDUZI Pict

Muktasari:

  • Timu 10 zinatarajiwa kushiriki Kombe la Mapinduzi 2026 zikiwamo tano za Tanzania Bara na nne kutoka Zanzibar, pia moja ya Uganda.

SIKU 17 za kuwania ubingwa wa Kombe la Mapinduzi 2026, tunaanza kuzihesabu Jumapili hii Desemba 28, 2025 pale kipute kitakapoanza kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja, kisha tamati yake itakuwa Jumanne ya Januari 13, 2026 kwenye Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba.

Timu 10 zinatarajiwa kushiriki Kombe la Mapinduzi 2026 zikiwamo tano za Tanzania Bara na nne kutoka Zanzibar, pia moja ya Uganda.

Zanzibar ambayo ni mwenyeji wa michuano hiyo inayokwenda msimu wa 20 tangu mwaka 2007, inawakilishwa na mabingwa mara mbili Mlandege, Mwembe Makumbi na KVZ zinazopatikana kisiwani Unguja na Fufuni ya Pemba.

MAPI 02

Tanzania Bara zipo Azam, Simba, Yanga, Singida Black Stars na TRA United wakati URA ikitokea Uganda ikiwa ni timu pekee kutoka nje ya mipaka ya Tanzania.

Kinachosubiriwa msimu huu wa michuano hiyo, ni kuona nani anakwenda kuwa bingwa mpya baada ya 2025 kushirikisha timu za taifa na Zanzibar Heroes kunyakua taji ikiifunga Burkina Faso 2-1.

Kabla ya hapo, misimu yote zilikuwa zikishiriki timu za klabu na Mlandege ilikuwa ya mwisho kubeba ubingwa mara mbili mfululizo mwaka 2023-2024.

MAPI 01

KWA NINI FAINALI PEMBA?

Imekuwa kawaida mashindano hufanyika kama Pemba basi inakuwa mwanzo hadi mwisho, lakini ikiwa Unguja, hali ni hiyo hiyo.

Safari hii, hatua ya makundi na nusu fainali, mechi zitachezwa Unguja, fainali itapelekwa Pemba.

Sababu za fainali kupelekwa Pemba zinawekwa wazi na Katibu wa Kamati ya Kombe la Mapinduzi 2026, Rashid Said Suleiman alipozungumza na Mwanaspoti.

Suleiman anasema kabla ya kuchezwa fainali hiyo Januari 13, 2026 kwenye Uwanja wa Gombani, kisiwani Pemba, litafanyika tukio la uzinduzi wa uwanja huo uliofanyiwa maboresho makubwa.

"Fainali kama kawaida imekuwa ikichezwa Januari 13 kila mwaka na safari hii itafanyika Pemba kwenye Uwanja wa Gombani.

"Tunamshukuru Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi kwa kuufanyia maboresho Uwanja wa Gombani ambao umekuwa wa kisasa zaidi kama alivyofanya Uwanja wa New Amaan Complex ambao leo hii mechi kubwa za kimataifa zinachezwa hapa Zanzibar," anasema Suleiman.

Hii itakuwa ni mara ya pili mfululizo fainali ya michuano hiyo kuchezwa Uwanja wa Gombani baada ya Kombe la Mapinduzi 2025 kufanyika hapo kuanzia hatua za mwanzoni hadi mwisho ikishirikisha timu za taifa.

MAPI 03

FEDHA ZAONGEZEKA

Kumekuwa na ongezeko la fedha katika misimu kadhaa ya Kombe la Mapinduzi kutoka Sh10 milioni anayokabidhiwa bingwa miaka hiyo ilipoanza hadi Sh100 milioni mara ya mwisho ilipofanyika 2025.

Kwa Kombe la Mapinduzi 2026, bingwa anatarajiwa kukabidhiwa Sh150 milioni, kukiwa na ongezeko la Sh50 milioni kutoka ile ya awali. Pia mshindi wa pili atapewa Sh100 milioni kutoka Sh70 milioni.

Suleiman anasema: "Thamani ya Kombe la Mapinduzi ni kubwa, hiyo ndio sababu ya kuongeza fedha kwani mwenye mapinduzi yake, Rais Mwinyi ameona hilo ni jambo muhimu kuipa heshima michuano hii kwa kuanzia mwaka huu.

"Lakini pia wadhamini wameipa thamani kubwa Mapinduzi Cup ya safari hii, tunawashukuru sana kwa mchango wao kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri."

MAPI 04

USHIRIKI WA TIMU

Kila mmoja anajiuliza kuna vigezo gani vinatumika kuzichagua timu zinazoshiriki Kombe la Mapinduzi kila mwaka, tukiwa tunaelekea kushuhudia kuanza kwa michuano hiyo, ukweli umefichuliwa.

"Kwanza watu watambue yale mambo ya zamani ya tunazialika timu kuja kushiriki hayapo tena, kwa muda mrefu klabu zenyewe zimekuwa zikituma maombi ya kushiriki na kamati inakaa kuangalia vigezo tunavyoweka.

"Kama hivi sasa tunavyoongea naweza kukwambia tayari tuna maombi ya timu zinazotaka kushiriki Kombe la Mapinduzi 2027, hii inatoa taswira mashindano haya ni makubwa na yanafuatiliwa kwa kiwango kikubwa.

"Lakini klabu zinapotuma maombi ya kushiriki, kigezo kikubwa ambacho huwa tunakiangalia ni kama zinakidhi haja ya kusherehesha katika sherehe zenyewe za Mapinduzi. Hatuchukui timu ilimradi imeomba, lazima tuchuje.

"Jambo lingine ambalo huwa tunaangalia, timu lazima iwe inashiriki Ligi Kuu katika sehemu inayotokea.

"Pia kuna nafasi ya wajumbe kutoa maoni kwa timu wanazoona zinafaa baada ya mchujo kupita huwa tunapiga kura.

"Katika jambo lingine muhimu zaidi, kwa sababu haya ni mashindano ya Mapinduzi, basi lazima timu shiriki iwe kutoka Pemba, Unguja, Tanzania Bara na nyingine ya Afrika Mashariki," anasema Suleiman.

MAPI 05

MATARAJIO

"Tunatarajia msimu huu tutakuwa na mashindano bora zaidi kwa sababu ya vitu vingi ambavyo tunakwenda kuvifanya.

"Kwanza zawadi zenyewe zinatoa nafasi kwa timu kuonyesha ushindani wa hali ya juu ambao utaibua msisimko wa mashindano yenyewe.

"Pia kuna sapraizi ambayo Desemba 27 (leo Jumamosi) tunakwenda kuitangaza katika mkutanao na waandishi wa habari utakaofanyika Posta jijini Dar es Salaam.

"Lakini jioni yake siku hiyo kwenye Uwanja wa Mao kisiwani Unguja, kutakuwa na shamrashamra za awali za ufunguzi wa mashindano hayo kabla ya siku yenyewe Desemba 28 kufanyika rasmi pale New Amaan Complex.

"Niwaambie tu mashabiki watarajie furaha na wataona ufunguzi wa kiwango kikubwa ambacho hawajawahi kukiona katika mashindano haya.

"Nasema hivyo kwa sababu tumejifunza vingi kupitia ufunguzi wa AFCON mwaka huu inayofanyika Morocco, pia ufunguzi wa African Football League uliofanyika Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam (Oktoba 20, 2023) lakini hata ufunguzi wa CHAN 2024.

"Kwa kupitia mashindano hayo, watu wataona namna ufunguzi wa Kombe la Mapinduzi 2026 utakavyofanyika na kuvutia zaidi.

MAPI 06

"Pia hata katika kufunga mashindnao yenyewe pale Gombani, kutakuwa na sapraizi kibao zitaenda kufanyika.

"Kutokana na kwamba siku hiyo pia utafanyika uzinduzi wa uwanja wenyewe, hivyo tutarajie kitu kikubwa na cha tofauti kinakwenda kufanyika," anasema Suleiman.


RATIBA

Desemba 28, 2025

Mlandege vs Singida BS (Saa 10:15 jioni)

Azam vs URA (saa 2:15 usiku)


Desemba 29, 2025

Fufuni vs Mwembe Makumbi (Saa 10:15 jioni)

KVZ vs TRA (Saa 2:15 usiku)


Desemba 31, 2025

Mlandege vs URA (Saa 10:15 usiku)

Singida BS vs Azam (Saa 2:15 usiku)

MAPI 07

Januari 2, 2026

Azam vs Mlandege (Saa 2:15 usiku)


Januari 3, 2026

Singida BS vs URA (Saa 10:15 jioni)

Simba vs Mwembe Makumbi (Saa 2:15 usiku)


Januari 4, 2026

Yanga vs KVZ (Saa 2:15 usiku)


Januari 5, 2026

Fufuni vs Simba (Saa 2:15 usiku)


Januari 6, 2026

Yanga vs TRA (Saa 2:15 usiku)


Januari 8, 2026

Nusu Fainali ya Kwanza (Saa 2:15 usiku)


Januari 9, 2026

Nusu Fainali ya Pili (Saa 2:15 usiku)


Januari 13, 2026

Fainali (Saa 2:15 usiku)


MAKUNDI

Kundi A: Mlandege, Azam, Singida Black Stars, URA

Kundi B: Simba, Mwembe Makumbi, Fufuni

Kundi C: Yanga, KVZ, TRA United