Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mzungu wetu Allarakhia yupo daraja la tano na anatusaidia

JICHO Pict


KIPENZI cha mashabiki wa Tanzania, Tarryn Allarakhia. Ametuvutia wengi katika michuano ya Afcon ambayo inaendelea kule Morocco. Tunamuita mzungu sio kwa sababu za kibaguzi, hapana. Tunamuita mzungu kwa sababu ya kumsifu na kumtofautisha na wengine pale tunapotaka kumsifia.


Nawakumbusha tu kwamba mzungu wetu anacheza klabu ya Rochdale iliyo daraja la tano kwa ngazi za mpira wa England. Imenifikirisha sana. Ligi yao inaitwa National League na kuanzia ile Ligi Kuu ya kina Arsenal mpaka kufika daraja lake kuna ngazi nne katikati. Kuna pengo kubwa kati ya kina Bukayo Saka na yeye.


Kwanza imenifikirisha safari yetu ya kisoka ilivyo ngumu. Kwa sasa hatuna vipaji vingj vya soka kiasi kwamba mchezaji wa daraja la tano England kwetu ana msaada mkubwa. Wakati wenzetu wakiwategemea wachezaji mbalimbali wa ligi kubwa za soka Ulaya na kwingineko, sisi tunamtegemea mchezaji wa daraja la tano England.

Na kwanini tusimtegemee? Kuna wachezaji gani wa kumuzuia tusimtegemee? Sisi sio Senegal yenye kina Idrissa Gana Gueye.

Sisi sio Morocco yenye kina Achraf Hakimi na wengineo. Sisi ni Tanzania tu. Alichukua uamuzi kuja kucheza kwenye asili yake kwa sababu nafasi zipo. Juhudi zake tu.

JIC 01

Kilichonifikirisha kingine ni namna ambavyo wachezaji wetu wa ndani na nje walivyo na safari ndefu kufikia mafanikio ya kucheza kiwango cha juu.

Huwa tunadanganyana kwamba mchezaji fulani wa Ligi Kuu yetu anaweza kucheza katika timu fulani za Ligi Kuu England. Kama mzungu wetu yupo daraja la tano licha ya kipaji hiki unajiuliza wachezaji wa Ligi Kuu ya NBC watawezaje?

Sio yeye tu. Mtazame Haji Mnoga anavyocheza. Ana nguvu ana akili ya mpira lakini anacheza klabu ya daraja la nne Salford FC. Kabla haujafikiria kucheza ligi kubwa za Ulaya jaribu kwanza kulinganisha kiwango chako na cha Allarakhia na Mnoga. Wanaibeba timu yetu lakini wapo katika madaraja la chini kabisa.

JIC 02

Ukifika hapo inabidi umuheshimu Mbwana Samatta. Hata kina Allarakhia wanamuheshimu Mbwana Samatta wanapogundua kwamba alifika ngazi ya Ligi Kuu England na sasa anacheza Ligi Kuu ya Ufaransa.

Sio kitu rahisi sana kwa sababu wao malengo yao ni kucheza katika ligi kama hizo lakini wameishia kucheza madaraja ya chini England licha ya vipaji vyao.

Nawaza tu kwamba kama kina Allarakhia wangekuwa walau wanacheza lile daraja la pili maarufu kama Championship basi wangetusaidia zaidi na zaidi. Hivi tu wapo madaraja ya chini zaidi wanatusaidia, vipi kama wangekuwa wanacheza walau Championship au katika ligi za kawaida za Ubelgiji, Russia au Ireland?

JIC 03

Mchezaji mwingine ambaye amegeuka kuwa kipenzi cha Watanzania ni Alphonce Mabula. Ana nguvu kubwa katikati ya dimba na shukrani wa kocha wa Taifa Stars, Miguel Gamondi ambaye amekuwa akimpa nafasi katika mechi zote.

Mabula ameonekana mgeni katika macho ya mashabiki ambao mara nyingi wanawakariri kwa haraka wachezaji wanaocheza Simba, Yanga na Azam.

Mabula amekuja kuwashangaza lakini nawakumbusha tu kwamba anacheza soka la kulipwa katika Ligi Kuu ya Azerbaijan. Sio ligi kubwa Ulaya. Ni ligi ya kawaida tu.

Fikiria licha ya kucheza katika ligi ya kawaida tu pale Ulaya akiwa katika klabu ya Shamakh bado ana msaada mkubwa kwetu. Wenzetu wakubwa wa Afrika huwa wanaringa kwamba mchezaji akicheza katika ligi hizo hawawezi kumuita katika kikosi cha timu ya taifa.

JIC 04

Kuna vijana hawana ubavu kama wa Mabula na wanatudanganya kwamba wanataka wakacheze katika Ligi Kuu ya England.

Kabla haujafikiria kucheza Leeds United jikumbushe kwamba pamoja na mbavu zake lakini Mabula anacheza Ligi Kuu ya Azerbaijan. Tumuombee tu aonwe na mawakala wa klabu zilizo katika Ligi Kuu kama ya Ubelgiji, Italia au Ufaransa. Kwetu itatutosha sana. Wakati huu Taifa Stars ikiwa inasaka ushindi wake wa kwanza wa michuano ya Afcon tujikumbushe pengo lililopo baina ya wakubwa wengine na sisi.

Tusijidanganye katika mambo mengi. Tunahitaji kuzalisha wachezaji wengi ambao watacheza nje. Kama kina mzungu wapo madaraja ya chini Ulaya na wanatusaidia kwa mambo mengi, vipi kama tungekuwa nao wengi zaidi?

Nadhani hii ndio njia kubwa zaidi ya kuisaidia Taifa Stars kama wenzetu wanavyofanya. Misri ndio taifa pekee la Afrika ambalo liliwahi kuunyanyasa mpira wa Afrika kupitia wachezaji wa ndani.

 Wakati huo ligi yao ilikuwa bora zaidi na ilikuwa na wachezaji wengi ambao walikuwa na viwango vya kucheza Ulaya lakini wakaamua kuishia nyumbani.

Sisi wengine msaada wetu utatoka zaidi kwa kina Allarakhia. Wachezaji wa ndani wapungue kadri inavyowezekana.

Tatizo sioni hili likitokea kwa sababu kwanza hatufanyi biashara ya kuuza wachezaji, lakini pili hata wachezaji wenyewe hawana mpango wa kwenda huko nje kuongeza ujuzi na ubora wao. Kitu kibaya zaidi ni kwamba inasemwa kwamba ligi yetu ina pesa.

Kila siku ni mwendo wa wachezaji wetu kusaini mikataba mipya katika klabu zao kubwa. Kina Fei Toto, Clement Mzize na wengineo kila siku wanasaini mikataba mipya na hawaonekani kama wanataka kucheza nje na kutuletea kitu kipya kama kina Allarakhia walivyotuletea katika michuano hii.

Klabu nazo zinawabakiza kwa sababu zinataka kupimana ubavu na wakubwa wa Afrika Kaskazini. Kwa ajili ya Stars iliyo imara tunahitaji wachezaji wanaocheza nje. Wakati mwingine sio lazima iwe Manchester United au Barcelona.

Kuna timu za kawaida kama Leece, Bologna, Wigan Athletic, Mainz na nyinginezo zinaweza kukupa kikosi imara cha timu ya taifa. Ligi yetu haijafikia ubora wa kutupa kikosi imara cha kushindana na kina Morocco.

Mwakani tutaandaa michuano hii nyumbani. Sioni kitu ambacho tunaweza kubadili kwa sasa. Kocha wetu Gamondi ataweza kufanya anachofikiria lakini kuna wakati uwezo wa wachezaji unaamia mechi. Aina ya wachezaji pia inaamua mechi. Aina ya ligi ambazo wachezaji wanatoka pia zinasaidia kuamua mechi.