Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nondo sita za Miguel Gamondi

GAMONDI Pict


JULAI 3, 2025, uongozi wa Singida Black Stars ulimtambulisha rasmi aliyekuwa Kocha wa Yanga, Muargentina Miguel Gamondi, ikiwa ni baada ya kuachana na kikosi hicho Novemba 15, 2024, tangu alipojiunga nacho kwa mara ya kwanza, Juni 24, 2023.


Gamondi aliyemrithi Mtunisia Nasreddine Nabi, aliondoka Yanga baada ya kuchapwa mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu msimu wa 2024-2025, dhidi ya Azam FC bao 1-0, Novemba 2, 2024, kisha 3-1 na TRA United zamani Tabora United, Novemba 7, 2024.


Kwa msimu wa 2024-2025, Gamondi aliiongoza Yanga katika mechi 10 za Ligi Kuu Bara, ambapo kati ya hizo alishinda minane na kupoteza miwili, huku akiweka rekodi za kibabe akiwa na kikosi hicho na sasa anaziendeleza na Singida Black Stars.


GAMO 04

KOMBE LA KAGAME

Baada ya ujio wa Gamondi akaiwezesha Singida kutwaa ubingwa wa kwanza wa Kombe la Cecafa Kagame uliyofikia tamati rasmi Septemba 15, 2025, jijini Dar es Salaam kwa kushuhudia kikosi hicho kikiifunga Al-Hilal Omdurman kutoka Sudan mabao 2-1.

Singida ilifika fainali hiyo baada ya kuifunga KMC mabao 2-0, yaliyofungwa na Clatous Chama na Ande Koffi Habib Cirille, huku Al-Hilal ikifuzu kwa kuitoa APR ya Rwanda kwa mabao 3-1 ndani ya dakika 120, kufuatia dakika 90 kuisha sare ya 1-1.

Katika fainali ya mwaka huu, Singida iliongoza kundi A na pointi saba, baada ya kushinda mechi mbili na kutoa sare moja, nyuma ya Kenya Police kutoka Kenya ya pili na pointi sita, Ethiopian Coffee SC ya Ethiopia ikiwa ya tatu na pointi nne.

Garde Cotes ya Djibouti iliburuza mkiani ikichapwa mechi zote tatu, huku Gamondi akiandika rekodi ya kuipatia ubingwa wa kwanza Singida tangu michuano hiyo ilipoanza mwaka 1967, ikifahamika CECAFA Club Cup, kisha kupewa jina la Kagame 2002.

GAMO 01

MAKUNDI CAF

Gamondi baada ya kuipeleka Yanga katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2023–2024, kufuatia miaka 25, tangu iliposhiriki mara ya mwisho 1998, akaandika rekodi nyingine mpya akiwa na Singida kwenye Kombe la Shirikisho.

Kocha huyo aliipeleka Yanga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza baada ya miaka 25, kufuatia kufanya hivyo mara ya mwisho 1998, ikiwa chini ya kocha wa muda, Tito Mwaluvanda aliyempokea Mwingereza, Steve McLennan.

Mwaluvanda alipewa timu hiyo akiwa hana umaarufu wowote na aliyekuwa Mwenyekiti, Rashid Ngozoma Matunda, ambapo kikosi hicho kiliangukia kundi na ASEC Mimosas ya Ivory Coast, Manning Rangers (Afrika Kusini) na Raja Casablanca ya Morocco.

Kwa wakati huo, mechi ya kwanza tu Yanga ilichapwa mabao 6-0 na Raja Casablanca, ikachapwa 3-0 na ASEC Mimosas kwenye Uwanja wa Uhuru kisha ikaenda Afrika Kusini kupambana na Manning Rangers na kuambulia kichapo kingine cha mabao 4-0.

Baada ya hapo ikapoteza ugenini 2-1 dhidi ya ASEC Mimosas, 1-1 na Manning kisha sare ya mabao 3-3 na Raja Casabalanca kwenye Uwanja wa Uhuru na kumaliza mechi zake sita ya hatua ya makundi, ikiwa imefunga mabao matano tu na kuruhusu 19.

Gamondi aliyewahi kufundisha timu mbalimbali alifika hatua hiyo ya makundi baada ya miaka hiyo 25 kufuatia kuifunga Al

Merrikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 3-0, ikiwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo, kwani awali ilikuwa haijawahi kushinda.

Yanga ilikuwa haijawahi kuifunga Al Merrikh katika mechi za CAF ila chini ya Gamondi timu hiyo ya Sudan ilipoteza mabao 2-0, Septemba 16, 2023, yaliyofungwa na Kennedy Musonda na Clement Mzize ikiwa uwanja wake wa nyumbani jijini Rwanda.

Mechi ya marudiano iliyopigwa Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam, Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0, Septemba 30, 2023, lililofungwa na Clement Mzize, lililoiwezesha kufuzu makundi Ligi ya Mabingwa kwa jumla ya mabao 3-0.

Kocha huyo ameiwezesha Singida kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, ikiwa ni kwa mara ya kwanza msimu huu wa 2025-2026 kwa timu hiyo tangu kuanzishwa kwake, ikiwa ni mwendelezo wa rekodi nzuri kwa raia wa Argentina.

Singida ilianza hatua ya kwanza ya michuano hii kwa kuitoa Rayon Sports ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-1, kisha raundi ya pili ikaiondosha Flambeau du Centre ya Burundi kwa jumla ya mabao 4-2, hivyo, kuandika historia mpya kwa timu hiyo.


GAMO 02

MATAJI MANNE

Tayari akiwa nchini, Gamondi ametwaa mataji manne akiwa na timu mbili tofauti, ambapo aliipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2023-2024, ukiwa ni wa 30 kwa kikosi hicho tangu mwaka 1965, Kombe la Shirikisho FA na Ngao ya Jamii 2024.

Taji lingine la nne amelichukua na Singida Black Stars ambalo ni la michuano ya Kombe la Cecafa Kagame 2025, ukiwa ni ubingwa wa kwanza, ingawa ni wa 14 kwa timu za Tanzania kuchukua huku Simba ikiwa ndio inayoongoza ikichukua mara sita.

GAMO 06

MECHI 11

Tangu Gamondi ateuliwe kuiongoza timu hiyo, imecheza mechi 11, za mashindano mbalimbali msimu huu wa 2025-2026, kuanzia Kombe la Kagame, Shirikisho Barani Afrika na Ligi Kuu Bara, ambapo kati ya hizo ameshinda tisa na kutoka sare miwili tu.

Singida chini ya Gamondi haijapoteza mechi ya kimashindano tangu ilipochapwa mara ya mwisho na Yanga mabao 2-0, katika fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, Juni 29, 2025.

Katika mechi hizo ambazo Singida imecheza tangu mara ya mwisho ilipochapwa na Yanga kwa maana ya msimu uliopita wa 2024-2025, safu ya ushambuliaji ya timu hiyo imefunga mabao 16, huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara tano tu hadi sasa.

Rekodi hiyo ni bora kama alivyokuwa na Yanga ambapo aliiongoza katika jumla ya mechi 40 za Ligi Kuu Bara kuanzia msimu wa 2023-2024, hadi wa 2024-2025, ambapo kiujumla kati ya hizo alishinda 34, akitoka sare miwili na kupoteza pia minne.

Katika mechi hizo 40 za msimu wa 2023-2024 na 2024-2025, safu ya ushambuliaji ya Yanga chini ya Kocha, Gamondi, ilifunga jumla ya mabao 85 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 18, ambapo kiujumla kwa misimu miwili tu alikusanya pointi 104.


GAMO 05

REKODI YA ROBO FAINALI

Ushindi wa mabao 4-0, ilioupata Yanga dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria Februari 24, 2024, katika hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, ulimfanya Gamondi kuandika rekodi mpya ya kuivusha robo fainali kwa mara ya kwanza kwenye historia.

Gamondi aliandika rekodi nyingine mpya ya kibabe kwa kuifanya Yanga iwe ya kwanza nchini kushinda mabao mengi zaidi kwa timu za Kaskazini.

Ushindi huo wa mabao 4-0, dhidi ya CR Belouizdad uliifanya kuivuka rekodi iliyokuwa inashikiliwa na Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018-2019 ambapo ilikuwa ya kwanza nchini kuifunga JS Saoura ya Algeria kichapo cha mabao 3-0.

Mabao ya Simba yalifungwa na nyota wa zamani wa timu hiyo, Emmanuel Okwi na Meddie Kagere aliyefunga mawili na kuifanya kumaliza nafasi ya pili katika kundi la ‘D’ na pointi tisa nyuma ya vinara, Al Ahly ya Misri iliyomaliza na pointi 10.

GAMO 03

Kwa mara ya kwanza Yanga ilicheza robo fainali enzi hizo ikiitwa Klabu Bingwa Afrika mara mbili, 1969 na 1970 na kucheza makundi 1998, ingawa tangu hapo haikuwa na maajabu hadi msimu wa 2022-2023, ilipocheza fainali ya Shirikisho Afrika.

Kwa msimu huo wa 2022-2023, Yanga ilicheza fainali na USM Alger, ambapo mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam ilichapwa mabao 2-1, Mei 28, 2023, kisha kushinda Algeria 1-0, Juni 3, 2023, ingawa ilikosa ubingwa kwa faida ya bao la ugenini.

Pia, iliishia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2016 na 2018, huku ikifika robo fainali ya Kombe la Washindi Afrika 1995, ingawa kwa Gamondi na Singida ana kazi nyingine ya kufikia huko na kuandika rekodi nyingine mpya kikosini.


GAMO 07

KUIPIGA SIMBA TANO

Moja ya jambo kubwa litakalokumbukwa kwa Gamondi ni kuiwezesha Yanga kushinda kwa mabao 5-1, dhidi ya Simba Novemba 5, 2023, yaliyofungwa na mastaa, Kennedy Musonda, Stephane Aziz KI na Pacome Zouzoua huku Maxi Nzengeli akifunga mawili.

Kichapo hicho kilimfukuzisha kazi Kocha, Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’, ambaye alikuwa na rekodi nzuri mbele ya Yanga, akiifunga mara tatu kwenye mechi tofauti ikiwemo ya Ligi Kuu Bara na Ngao ya Jamii, japo mambo yote yalibadilika.

Simba ilikuwa haijawahi kufungwa na Yanga idadi kama hiyo kubwa ya mabao tangu ilipolazwa 5-0 mwaka 1968, kipigo ambacho Simba ilikilipa kwa kishindo mwaka 1977 kwa kuifunga Yanga 6-0 kisha kupigilia msumari mwingine wa mabao 5-0 mwaka 2012.