Prime
Rafiki yangu Folz mtaani huku watu wanaguna
LABDA watu wa karibu watamwambia rafiki yangu, Roman Folz kwamba mtaani huku watu wanaguna. Yanga wanashinda kila mechi wanayocheza, lakini mashabiki wao wanaguna. Hakuna mechi ambayo hawajashinda tangu walipoingia msimu mpya.
Mechi ya kwanza dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda, Yanga walishinda mabao 3-1. Mashabiki hawakuona tatizo la msingi sana. Nilipouliza habari za ndani nikaambiwa kwamba kocha alikuwa hajaanza mazoezi ya mbinu. Kwamba wachezaji walikuwa wanapitia kipindi cha mazoezi magumu. Miili ilikuwa haijafunguka.
Wakacheza pambano lao la Wiki ya Mwananchi dhidi ya Bandari ya Mombasa. Timu ya kawaida kabisa iliyomaliza ya nane katika Ligi Kuu yao msimu uliopita. Ilikuwa mechi ya kawaida kabisa. Walifunga bao la mapema la Celestin Ecua na baada ya hapo wakageuka kuwa Coastal Union uwanjani. Tukaambiwa walikuwa wameficha mbinu kwa sababu walikuwa wanakabiliwa na pambano dhidi ya mtani ndani ya siku nne zijazo.
Yanga wakacheza mechi na mtani. Pambano la ufunguzi wa msimu. Ilianzia kwa wazungu kule kwamba pambano hili linaitwa Ngao ya Hisani au Ngao ya Jamii. Yanga walishinda 1-0 katika pambano ambalo kwa matokeo waliendelea walipoishia, lakini kwa kiwango hawakuendelea walipoishia. Pambano la mwisho kabla ya hilo Yanga walikuwa wameupiga mwingi.
Wakati Clement Mzize alipofunga bao la pili na la mwisho kabisa la msimu kwa timu yake na msimu mzima wa Ligi, Simba waliondoka uwanjani wakiwa wameridhika kwamba walikuwa hawawawezi Yanga. Mashabiki na viongozi waliambiana ukweli kwamba walipaswa kwenda katika msimu mpya na kujipanga.
Pambano hili la kwanza la msimu huu baina yao, Pacome Zouzoua akifunga bao la ushindi, Simba hawakuridhika na Yanga hawakuridhika. Simba hawakuridhika kwamba walikuwa wamefungwa na timu bora na Yanga hawakuridhika kwamba walikuwa wameshinda mechi kwa sababu walikuwa timu bora uwanjani. Mashabiki wakaguna kwa Roman Folz.
Ikaja mechi dhidi ya Wiliete ugenini wakashinda mabao 3-0, kisha wakacheza na Pamba wakashinda mabao 3-0 nyumbani, halafu juzi wameshinda mabao 2-0 dhidi ya Wiliete pambano la marudiano. Mechi hizi tatu ukijumlisha ile ya Simba mashabiki wameondoka wakiwa hawajaridhika. Wameguna kwa kiasi kikubwa.
Kwanini wameguna? Yanga wanaijua timu yao. Na wanaijua timu yao kwa sababu nyingi. Wameijua timu yao kwamba huwa inacheza inashinda, huku ikiwa inacheza kwa swaga. Kwa sasa inacheza huku ikiwa haina swaga. Na cha kushangaza zaidi wamekuja wachezaji wengi walio bora katika dirisha kubwa lililopita la uhamisho wa wachezaji.
Kuna wanaojaribu kujali kwamba kitu muhimu ni ushindi, lakini kuna kundi ambalo naliona ni kubwa ambalo halitaki aina ya ushindi ambao unapatikana kwa sasa. Wanataka waende mtaani wakiwa na kelele za kiwango cha timu na idadi ya mabao. Tangu msimu huu hawajaweza kupiga kelele hizo.
Na labda kwa muda mrefu sasa hawajawahi kuwa katika hali hiyo. Chini ya Nasreddine Nabi, Miguel Gamondi, Sead Ramovic na kisha Miloud Hamdi, Yanga wamekuwa na swaga fulani hivi na mechi zao. Muda pekee ambao walikwenda chini ni pale walipochapwa na Al Hilal ya Sudan wakiwa nyumbani na kisha wakafungwa na Tabora United. Vinginevyo Ramovic alipoichukua timu moto uliendelea.
Miloud Hamdi alipoichukua timu moto uliendelea vile vile. Na Miloud aliiacha timu vizuri katika pambano la mwisho dhidi ya mtani wakati Yanga walipofanya mambo mawili. Kwanza kumfunga mtani kwa mara ya tano mfululizo, lakini hapo hapo kutwaa ubingwa wa Ligi kwa mara ya nne mfululizo. Kifupi hakuna deni aliloacha nyuma yake.
Kwa matokeo, Folz ameendelea pale Miloud alipoishia, kwa kiwango cha timu Folz hajaendelea pale ambapo Miloud alipoishia. Nini kinatokea? Yanga wanaijua timu yao. Zamani walikuwa wamezoea kutawala mechi ambayo pia walikuwa wanatengeneza nafasi nyingi na kumfanya mpinzani ajione mnyonge uwanjani.
Ilikuwa inaanzia kwa namna walivyokuwa wanaumiliki mpira wakati wanao, namna walivyokuwa na kasi katika maeneo ya katikati na pembeni, lakini pia namna walivyokuwa wanatengeneza nafasi na pia kuwa bora wakati hawana mpira. Haya yote hayajaonekana sana kwa sasa na Folz amesababisha watu wagune.
Mfano ni pambano dhidi ya Pamba. Dakika 45 za kipindi cha kwanza mabeki wa Yanga na viungo wao walitumia muda mrefu kupiga mipira mirefu kwa mshambuliaji wao, Andy Boyeli pamoja na wachezaji wengine waliokuwa mbele. Yanga walikuwa wameusahau mpira huo kwa muda mrefu tangu wakati ule walipokuwa wanapiga pasi ndefu wa Mrisho Ngassa akimbie.
Kina Thaban Scara Kamusoko wakaanzisha tabia ya Yanga kuuweka mpira chini. Tabia ikaendelea kwa wengineo hadi ikamfikia Khalid Aucho. Lakini pambano hili dhidi ya Pamba Yanga walikuwa wanapiga mipira mirefu tu. Kipindi cha pili wakaingia Mohamed Doumbia na Pacome Zouzoua wakauweka mpira chini na Yanga wakawa bora bila ya kubutua.
Watetezi wa kocha wanaamini kwamba zilikuwa mbinu za kocha, lakini watu wengine wakaamini kwamba zilikuwa mbinu binafsi za wachezaji hawa wenye vipawa. Hata pambano la juzi lilikuwa ni aina ya pambano lile lile la dhidi ya Pamba ya Mwanza.
Na hadi sasa mashabiki wamegawanyika hapo. Wasimame upande wa kocha au wasimame upande ule ambao hauamini katika kiwango kinachoonyeshwa chini ya kocha huyu? Huku mtaani kwetu ambao hawapo na kocha wapo wengi. Hili inabidi ligonge kengele katika vichwa vya viongozi. Inabidi wamvute Folz kando wamwambie ukweli.
Kitu ambacho hatujui kama ni kibaya au kizuri kwa mashabiki ni ukweli kwamba mashabiki wa siku hizi wanazijua timu zao. Na kuna mashabiki wengi ambao wameacha tabia ya zamani ya kufurahia ushindi ili mradi timu imeshinda. Kuna kundi kubwa la mashabiki ambao wanachambua mpira ulivyokuwa. Hawa ndio wale ambao wameiona timu yao ikishinda mechi zote tangu msimu uanze lakini hawana furaha.
Baadaye wanaweza kupeleka presha kubwa kwa Injinia Hersi Said na wenzake. Presha ikiwa kubwa viongozi hawawezi kuhimili. Hii ipo hata kwa watani wao. Ipo hata katika klabu zao. Lakini kabla hali haijawa mbaya ndipo ambapo viongozi wanaweza kumnong'oneza Folz kwamba mtaani kuna watu wanaguna. Haelewi Kiswahili vizuri kwahiyo inabidi wamwambie ili aelewe.
Asidhani kwamba timu inashinda na mashabiki wana furaha sana. Hapana. Mashabiki wanaijua timu yao vema. Halafu huwa wanajua pia wachezaji wao vema. Wanajua ubora wa wachezaji walioingia na waliotoka. Unaweza kuwadanganya kwa muda mfupi lakini hauwezi kuwadanganya kwa muda mrefu sana.