Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ronaldo na maisha baada ya soka

RONALDO Pict

Muktasari:

  • Kuchezea Ureno imekuwa sehemu muhimu ya hatua za mwisho za maisha ya Ronaldo katika soka, huku nyota huyo mwenye umri wa miaka 41 akithibitisha kuwa Kombe la Dunia lijalo litakuwa la mwisho kwake, ingawa bado alikuwa na nia ya kuichezea Ureno katika Euro 2028.

LISBON, URENO: JE, ndio mwisho? Cristiano Ronaldo anaweza kuwa amefikia tamati ya safari yake katika timu ya taifa ya Ureno baada ya kuondoka kambini mwa timu hiyo kufuatia mvutano na kocha Jorge Jesus.

Kuchezea Ureno imekuwa sehemu muhimu ya hatua za mwisho za maisha ya Ronaldo katika soka, huku nyota huyo mwenye umri wa miaka 41 akithibitisha kuwa Kombe la Dunia lijalo litakuwa la mwisho kwake, ingawa bado alikuwa na nia ya kuichezea Ureno katika Euro 2028.

Sasa, Ronaldo anaanza kutazama maisha yatakuwaje baada ya soka, huku uwezekano wa kustaafu ukizidi kuwa mkubwa na mkataba wake na Al Nassr ukitarajiwa kumalizika mwakani.

Hata hivyo, si kwamba hana cha kufanya baada ya kutundika daluga. Ronaldo anatajwa kuwa na utajiri unaokadiriwa kufikia pauni 1.1 bilioni, huku akiwa amewekeza katika biashara mbalimbali ambazo zinaweza kumweka bize kwa miaka mingi ijayo.


RONAL 02

AFUNGUA MILANGO HOLLYWOOD

Moja ya miradi mikubwa zaidi aliyoingia Ronaldo ni tasnia ya filamu.

Mwaka 2025, alishirikiana na mtayarishaji na mkurugenzi wa filamu wa Uingereza, Sir Matthew Vaughn, kuanzisha studio yao ya filamu inayojulikana kama UR•Marv.

Wawili hao tayari wameripotiwa kukamilisha filamu mbili za aina ya mapigano walizozalisha pamoja, huku filamu ya tatu ikiwa kwenye mipango.

Ronaldo alisema wakati huo: “Hiki ni kipindi cha kusisimua kwangu ninapoitazama safari yangu kuelekea miradi mipya ya biashara.”

Vaughn naye alimsifu Ronaldo akisema staa huyo ameunda simulizi nyingi uwanjani ambazo yeye mwenyewe asingekuwa na uwezo wa kuziandika na kwamba anatarajia kutengeneza naye filamu zenye kuvutia.


RONAL 03

ANAVYOKUZA UFALME WAKE WA BIASHARA

Ronaldo pia amewekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya maudhui na uzalishaji wa habari.

Mwaka 2024 alianzisha kituo chake rasmi cha YouTube, UR•Cristiano, ambacho kimekua kwa kasi na kumwezesha kuzungumza na mastaa mbalimbali, akiwamo MrBeast na Rio Ferdinand, huku pia akiwaonyesha mashabiki maisha yake nje ya uwanja.

Kituo hicho pia kimempa fursa mpenzi wake, Georgina Rodriguez, kuonyesha maisha yake kupitia ukurasa unaojulikana kama UR•By Gio.

Mwaka 2025, Ronaldo aliingia pia kwenye ulimwengu wa mapambano ya MMA baada ya kununua hisa katika kampuni ya WOW FC, ambayo ni promosheni ya mapambano nchini Hispania inayohusishwa na nyota wa UFC, Ilia Topuria.


RONAL 01

HOTELI, AFYA NA TEKNOLOJIA

Ronaldo ameendelea kujenga himaya kubwa ya biashara sambamba na maisha yake ya soka.

Aliwahi kusema alianza kujiandaa kwa maisha ya baada ya soka tangu akiwa na miaka 28, akieleza kuwa amewekeza katika hoteli, kliniki na biashara za afya kwa sababu alijua soka halidumu milele.

Maslahi yake ya kibiashara yamejikita zaidi katika sekta za hoteli, afya na ustawi wa mwili pamoja na teknolojia na vyombo vya habari.

Mlolongo wake wa hoteli za Pestana CR7 tayari una matawi katika miji mbalimbali, ikiwamo Lisbon, Funchal, Madrid, New York na Marrakech, huku mipango ikiwa ni kufungua hoteli nyingine Paris na Riyadh mwaka 2027.

Mwaka 2019, Ronaldo alishirikiana na Paulo Ramos kuanzisha kliniki ya kupandikiza nywele ya Insparya, ambayo kwa sasa ina shughuli nchini Hispania, Ureno na Mashariki ya Kati.

Pia anaendesha vituo vya mazoezi vya CR7 Crunch Fitness nchini Hispania na Ureno, huku akiwa amewekeza katika chapa ya maji ya madini ya URSU9.

Katika eneo la afya na ustawi wa mwili, mwaka 2024 alizindua programu ya Erakulis, huku pia akiwa mwekezaji mkubwa katika kampuni ya afya ya Bioniq inayotumia takwimu za afya kutengeneza virutubisho vinavyolenga mahitaji binafsi ya mtumiaji.

Februari 2026, Ronaldo alipanua ushirikiano wake wa miaka 13 na Herbalife kwa kuwekeza pauni5.6 milioni na kupata asilimia 10 ya hisa katika kampuni yake tanzu ya Pro2col.

Mbali na hayo, Ronaldo pia anaendelea kunufaika na biashara yake ya mavazi ya ndani inayozalisha aina mbalimbali za nguo hizo.


RONAL 05

MAISHA NA GEORGINA

Ronaldo, ambaye amekubali kuwa mwisho wa safari yake ya soka unakaribia, aliiambia Vogue Agosti iliyopita kuwa tayari ana mpango wa maisha yake baada ya soka pamoja na Georgina na watoto wao watano.

“Huenda huu ukawa mwaka wangu wa mwisho kucheza soka na nataka kuacha urithi wa kipekee,” alisema.

Aliongeza: “Nimepanga maisha yangu ya baadaye. Nina mambo mengi ya kunishughulisha kiasi kwamba ni vigumu kutaja jambo moja tu.

“Kwa sababu soka likiondoka linaweza kuacha pengo kubwa, ni lazima ujaze muda wako kwa mambo mbalimbali. Nataka pia kufurahia zaidi, kusafiri, kutazama na kucheza padel, ambayo naipenda sana, na kuendelea kufurahia nilichokipata tulichokipata.

“Baada ya yote, imekuwa miaka 25 ya kujitoa na kujinyima mengi.”


RONAL 04

AINGIA KWENYE UMILIKI WA KLABU

Ronaldo amekuwa akisisitiza mara kadhaa kuwa hana mpango wa kuwa kocha baada ya kustaafu.

Hata hivyo, baada ya kuona mafanikio ya David Beckham katika umiliki wa Inter Miami, ameanza kujihusisha na umiliki wa klabu.

Februari mwaka huu, Ronaldo alithibitisha kuwa amenunua asilimia 25 ya hisa za klabu ya Almeria inayoshiriki soka nchini Hispania.

Katika taarifa yake, alisema: “Imekuwa ndoto yangu ya muda mrefu kuchangia katika soka nje ya uwanja. Natarajia kufanya kazi pamoja na uongozi wa klabu kusaidia hatua yake inayofuata ya ukuaji.”

Ronaldo pia aliwahi kuwafanya mashabiki wa Manchester United kuota kuhusu uwezekano wa siku moja kuwa mmiliki wa klabu hiyo.

Akizungumza katika tuzo za Dubai Globe Soccer mwaka 2024, alisema tatizo la Manchester United si kocha pekee, bali ni jambo kubwa zaidi na kwamba endapo angekuwa mmiliki angefanya mabadiliko na kurekebisha maeneo ambayo yana matatizo.

Kwa Ronaldo, inaonekana kustaafu soka hakutamaanisha kustaafu shughuli. Uwanja unaweza kuwa unafungwa, lakini himaya yake ya biashara ndiyo inaanza kupata nafasi kubwa zaidi.