Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rudini nyumbani Taifa Stars hamna baya

TAIFA Pict

Muktasari:

  • Ni mwamuzi ambaye naambiwa huwa anapewa zaidi mechi za Morocco kwa ajili ya kazi maalumu. Adel Amrouche aliwahi kutumbia hilo katika mkutano wake na vyombo vya habari kule Ivory Coast katika Afcon iliyopita kwamba Morocco huwa wanabebwa. Akaishia kufungiwa.

RUDINI tu nyumbani Taifa Stars. Imetosha. Hamtatukuta tumenuna. Kazi tumeiona. Afcon ya mwisho tuliondoka na pointi mbili. Afcon hii tumeondoka na pointi mbili, lakini tukapata bahati tukasogea. Na juzi, mwamuzi Boubou Traore alikuwa na kazi moja tu. Kuhakikisha Tanzania inatoka na Morocco inasonga mbele.

Ni mwamuzi ambaye naambiwa huwa anapewa zaidi mechi za Morocco kwa ajili ya kazi maalumu. Adel Amrouche aliwahi kutumbia hilo katika mkutano wake na vyombo vya habari kule Ivory Coast katika Afcon iliyopita kwamba Morocco huwa wanabebwa. Akaishia kufungiwa.

Pambano la juzi kuna mambo mawili. Jambo la Kwanza tujilaumu wenyewe. Tungeweza kumfunga mdomo Traore kama Simon Msuva angefunga kwa kichwa nafasi ya wazi kipindi cha kwanza. Lakini, pia tungeweza kumfunga mdomo Traore kama Fei Toto angefunga nafasi nyingine ya wazi iliyomuangukia. Sijui angekimbilia katika VAR. Sijui.

STA 01

Jambo la pili ni Traore mwenyewe. Mtazame namna alivyokuwa anatembeza kadi za njano kama njugu kwa wachezaji wa Stars. Msuva aliparamiwa vilivyo na Achraf Hakimi, lakini hakutoa kadi. Kitendo hicho hicho alifanyiwa mchezaji wa Morocco akatoa kadi kwa mmoja wa mabeki wetu.

Stars walipochezewa faulo aliminya. Lakini kwa muda mrefu alikuwa anawatafutia mipira ya adhabu wachezaji wa Morocco. Na mwishowe kabisa Idd Seleman ‘Nado’ alisukumwa katika boksi. Kama angekuwa Brahim Diaz amesukumwa katika boksi na Bakari Mwamnyeto nadhani Traore angeweka penalti.

Afadhali angeenda kuikataa penalti katika VAR, lakini wala hakuwa na mpango wa kwenda katika VAR. Kulikuwa na kila haja ya Traore kuitembelea VAR. Walau angeenda kutudanganya kule lakini alijua kwamba angekwenda kule angekutana na penalti halali. Samaki mkubwa huwa anamla samaki mdogo.

STA 02

Kwa muda mrefu wa mchezo tuliwaudhi wachezaji wa Morocco na mashabiki wao. Walidhani ingekuwa mechi ya 3-0 hadi kufikia dakika ya 18 ya mchezo. Kumbe haikuwa hivyo. Tuliwaudhi haswa. Kwanza kwa namna tulivyokaba. Tulikaba vizuri, kisha tukakaba tena, halafu tukakaba zaidi. Mipira ya hewani iliyokuwa inaingia katika boksi ilikabiliwa vyema na Ibrahim Bacca, Bakar Mwamnyeto na Dickson Job.

Upande wetu wa kushoto, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ alikuwa anatembea vyema na Hakimi kwa sababu nguvu kubwa ya mashambulizi ya Morocco ni krosi. Tulikuwa imara na kipa wetu, Hussein Masalanga amenishangaza. Ni mgeni katika shughuli kama ile ya juzi, lakini alikuwa imara. Angeweza kufanya vizuri zaidi katikaa bao la Diaz, lakini tunaweza kumsamehe.

STA 03

Akiwa kama kipa wa tatu nyuma ya Yakoub Suleiman na Zuberi Foba, lakini Masalanga ambaye hakuwa maarufu katika michuano hii anarudi nchini akiwa maarufu. Alifanya kazi nzuri katika taimingi ya mipira ya hewani. Lakini alifanya kazi katika kuchelewesha muda. Makipa wazoefu huwa wanafanya hivi kwa ajili ya kupoza presha. Yeye sio mzoefu, lakini alijua ujanja huu.

Kitu kingine ambacho tuliwaudhi Wamorocco ni uwezo wetu wa kukaa na mpira wakati tunapookoa mashambulizi. Timu kubwa zinapenda zikikushambulia ubutue mpira. Wana bahati mbaya kwamba Tanzania ya leo wachezaji wanazidi kuimarika katika kukaa na mpira. Uhamishaji wa mpira kwenda kutengeneza shambulizi kwa sasa tunao. Zamani rafiki zangu kina Kevin Yondani walikuwa wanapiga mbele kwa jazba.

STA 04

Mpira wa Miguel Gamondi ndio huu. Umesababisha tutengeneze mashambulizi mengi. Umesababisha tufunge bao katika kila pambano la hatua ya makundi. Na juzi tungeweza kutoka uwanjani na mabao zaidi ya mawili kama Simon na Feisal wangekuwa makini na kama Traore angetupa penalti ya Idd Nado.

Kilichobaki kwa sasa ni ukweli kwamba Morocco wapo mbele yetu mbali kisoka. Kuanzia historia hadi sasa, lakini juzi hali ingeweza kuwa tofauti. Hata hivyo, Traore hakutaka na nadhani alikuwa na maagizo kutoka kwa wakubwa. Mpira wa Afrika una ujinga mwingi. Mwenyeji anabebwa ili mashindano yaendelee kunoga. Mwenyeji anabebwa ili ari ya michuano isishuke.

Na kwa kampuni zilizodhamini michuano pia hazitaki wakubwa watoke. Tanzania kwao ni samaki mdogo. Wao wanataka samaki wakubwa waendelee kuwepo na majina makubwa yaendelee kuwepo ili michuano iwe na mvuto. Wanataka kina Morocco, Cameroon, Nigeria, Ivory Coast waendelee kuwepo mpaka nusu fainali.

STA 05

Mpira una umafia mwingi. Huu wa kwetu huku Afrika kuna vitu ambavyo vinafanyika hadharani bila ya vificho. Ndio maana wazungu wanatushangaa. Dunia nzima juzi ilikuwa imejua kwamba Morocco walikuwa wameinyonga Tanzania kwa makusudi. Wana kila sababu. Wao ndio wanaimiliki CAF sasa hivi.

Kilichobaki sasa hivi turudi nyumbani. Ingekuwa idhini yangu ningempa Gamondi mkataba wa kudumu. Angetuandalia timu nzuri wakati tunashiriki michuano hii tukiwa wenyeji mwakani. Niliwahi kusema hapa kwamba tuna faida ya kuwa na Gamondi. Anawafahamu wachezaji wetu. Na amewafahamu wengine kina Alphonce Mabula na ameweza kuwatumia vyema.

Kitu kingine ni kwamba tukikutana na wachezaji wetu huko mitaani tuwaambie wazi kwamba wametuheshimisha. Kuanzia mechi ya Nigeria, kisha Uganda halafu Tunisia na mwishowe dhidi ya Morocco. Wametuheshimisha na waendelee hivi hivi. Taifa Stars ndio kitu pekee kinachotuunganisha zaidi Watanzania kwa sasa. Kwingineko tupo vipande vipande kama taifa.

Niliandika mahala katika mitandao ya kijamii. Wachezaji wa Taifa Stars kama walivyo wachezaji wa timu nyingine za taifa, pesa nyingi wanapata katika klabu zao. Wanajenga nyumba na kununua magari mazuri kwa sababu ya klabu zao. ‘Signing fee’ na mishahara. Timu ya taifa haina signing fee wala mshahara. Kuna posho za hapa na pale.

Wachezaji wanachofanya ni kuipambania jezi na bendera ya taifa. Tusiwavunje sana mioyo kwa kauli mbalimbali kali pindi wanapofanya makosa ya hapa na pale.

Niliandika kitu kuhusu Mbwana Samatta wiki iliyopita. Inawezekana anashuka au ameshuka. Lakini kuna kauli zinazotumika dhidi yake ambazo zinakuacha mdomo wazi. Angeweza kubaki Ufaransa akala raha zake, lakini yupo Morocco. Zaidi ni kwa sababu ya mapenzi na sio pesa.

Kwa sasa acha tu vijana warudi nyumbani. Kitu cha msingi mwakani tutakuwa tunashiriki Afcon ya tatu mfululizo. Zamani tulikuwa tunaota ndoto tu kuishi maisha kama haya. Sasa hivi tumejenga mazoea. Vijana warudi tu. Hawana baya. Sisi na wao wote tunatembea vifua mbele.