Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sakata la Sh850 milioni Kenya, TFF inaweza kujifunza kitu

ZENGWE Pict


Kwa kawaida migogoro huonekana kama kitu kinachozuia maendeleo ya taasisi kama vile chama cha michezo au klabu, hasa inapokithiri na kukosekana suluhisho.


Lakini, kwa mujibu wa wanafalsafa, migogoro ndiyo huonyesha uhai wa jamii au taasisi kwa kuwa huthibitisha jamii haiwezi kuwa na watu wa aina moja, watu wasio na uwezo wa kuhoji au kung’amua jambo baya na kutaka lishughulikiwe.


Ukiwa na taasisi ya watu wa aina hiyo, au ukiwa na jamii ya aina hiyo, basi una taasisi au jamii iliyooza na maendeleo kwao ni ndoto isiyoweza kutimia. Kwa hiyo, wakati mwingine unaweza kufurahia migogoro si kwa ubaya, bali kwa kuwa inazindua akili za watu, hasa viongozi waone wanaongoza taasisi ambayo ina uhai huku wanajamii wakijitambua wana wajibu fulani kabla ya kupata haki fulani.

Wakati mwingine kuamka kwa watu kwenye taasisi au jamii fulani huwa ni ukombozi kwa taasisi au jamii nyingine kwa kuwa masuala ya kijamii yana tabia ya kuambukiza na kusambaa.

Hatimaye Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) limerudi tena kwenye kile kinachoonekana kitakuwa mgogoro mkubwa baada ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji kuamua kumsimamisha rais wa shirikisho hilo, Hussein Mohamed  na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) aliyekuwa akikaimu, Dennis Gicheru kwa tuhuma za ubadhirifu wa Sh850.4 milioni  zilizolengwa kutumika wakati wa fainali za Mashindano ya Ubingwa wa Afrika (CHAN) mwaka jana.

ZENG 01

Wajumbe tisa kati ya 12 wa Kamati ya Utendaji ya FKF walikubaliana na uamuzi wa kuwasimamisha vigogo hao ili uchunguzi huru ufanyike dhidi ya tuhuma zao. Nafasi ya Hussein itakaimiwa na nyota wa zamani wa taifa hilo, McDonald Mariga huku nafasi ya CEO itakaimiwa na mjumbe wa kamati hiyo, Abdilahi Yusuf Ibrahim.

Imethibitika katika tuhuma hizo, zilizoibuliwa na raia mwema (whistle blower) Ustadh Okello Kimathi, FKF iliilipa kampuni ya bima ya Riskwell Dola 328,738 za Kimarekani kutimiza sharti la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa wenyeji kuweka bima ya mashindano hayo.

Lakini kampuni hiyo haikuwa imesajiliwa na Mamlaka ya Usajili wa Bima (IRA) kufanya kazi hiyo ya bima mwaka 2025. Fainali hizo zinazoshirikisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani ya nchi za Afrika, zilitakiwa zifanyike mwaka 2024, zilifanyika Kenya, Tanzania na Uganda kuanzia Agosti 2 hadi 30 mwaka jana.

Malipo hayo yalifanyika kwa jina la FKF lakini anuani ya mawasiliano ya baruapepe ilisomeka [email protected].

ZENG 02

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo gazeti la Daily Nation iliziona, kampuni tatu kubwa zilizosajiliwa, Takaful Insurance of Africa, Old Mutual General Insurance Kenya Limited na Britam Insurance ziliomba zabuni hiyo na kuweka viwango vya chini, lakini zikaambulia patupu na badala yake ikapewa Riskwell ambayo pamoja na kusajiliwa kama kampuni mwaka 2024, haikupata leseni ya kufanya kazi za bima hadi mwishoni mwa mwaka jana, jambo lililoibua maswali.

Kamati ya Utendaji ya FKF imesema wakati Hussein na mwenzake wakiwa wamesimamishwa, CAF na serikali wamealikwa kufanya uchunguzi wa sakata hilo ili kubaini ukweli.

Hii ni hatua kubwa kwa FKF katika suala la uwajibikaji na uwezo wa wajumbe wachombo cha juu katika kuendesha soka, kuhoji mienendo ya kiongozi wao na kuchukua hatua pale inapobidi. Hata Kamati ya Maadili ya FKF kwa sasa inafanya uchunguzi wa sakata hilo ili iweze kuchukua hatua zinazostahili.

Hatua kama hii ni ngumu kwa vyombo vilivyo ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa sababu mabadiliko makubwa ya katiba yaliyofanywa mwaka 2021, yalilenga kumwongezea rais madaraka makubwa, kiasi kwamba hawezi kuwa na Kamati ya Utendaji yenye nguvu ya kuhoji mienendo yake.

ZENG 03

Kwa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) kuwa chombo cha TFF, ni vigumu kwa mwenyekiti wake, ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji kuhoji jambo lolote la rais. Kwa kuwa katiba inampa rais wa TFF mamlaka ya kuteua mtu yeyote kuwa makamu wa rais, mtu huyo hawezi kuwa na nguvu ya kumuhoji rais wake aliyemteua.

Kwa rais kuwa na mamlaka ya kuteua wajumbe wawili kunamfanya awe na watu zaidi wa kutompinga wala kuhoji mienendo yake. Kwa kuwa na wajumbe watokanao na kamati za waamuzi na madaktari pamoja na soka la wanawake, pia kunaongeza idadi ya watu wanaomuunga mkono.

Ukishakuwa na kundi hilo la wanaomuunga mkono pamoja na kampeni ndogo ya kuwavuna wengine kutoka wajumbe wanaochaguliwa kwenye kanda, ni wazi ni vigumu kumhoji rais hata kama anafanya mambo tofauti na sheria au kanuni.

Ili kuzuia mkutano mkuu kuchukua uamuzi wowote dhidi ya rais, mabadiliko hayo ya katiba yalipunguza idadi ya wajumbe wanaopiga kura wa mkutano mkuu na kubakia ile inayowezekana kuimudu, idadi ambayo inaweza kupiga kura hata kabla kufika siku ya uchaguzi.

Kenya wamepitia magumu ndiyo maana wakawa na muundo wa uongozi unaoweza kumuwajibisha rais. Muundo huo ulishakuwepo Tanzania lakini mabadiliko hayo ya katiba yaliuondoa na kuurudisha kulekule kilikokuwa Chama cha Soka Tanzania (FAT).

ZENG 04

Ni dhahiri sasa TFF si shirikisho tena kwa kuwa kuna mabadiliko mengi yanayoondoa uhuru wa vyama vya mikoa kuendesha mambo yake na sasa vinategemea matamko kutoka makao makuu.

Ni muhimu kwa watu wa soka kutambua kunahitajika mfumo wa uongozi unaoweka nguvu kwa vyombo tofauti kudhibitiana, unaoweka uwajibikaji na unaoweka uwazi ili mambo yasiendeshwe kiimla au kwa lile neno la ‘uchawa’, bali kwa weledi na nia thabiti ya kuleta maendeleo. Kama Kenya wameamka, basi watu wa mpira nao hawana budi kuamka.

Na kuamka si kuanza harakati za kuwaondoa madarakani viongozi. La hasha! Bali ni kutafuta nguvu iliyopotea ya kuhoji kila jambo lisiloeleweka linapotokea.

Na raia wema kama Okello wanapotokea na kuibua uozo, ni muhimu vyombo husika vikachukua hatua kuchunguza kupata ukweli badala ya kujificha kwenye vile visingizio kuwa “hizo ni fitina za wasiomtaka fulani”.