Prime
Sasa Matola asimame kwa miguu yake
KAMA kuna kocha wa mpira wa miguu aliyefanya kazi kwa muda mrefu akiwa msaidizi, basi atakuwa ni Seleman Matola, kiungo wa zamani wa timu ya Simba. Matola alicheza kwa mafanikio akiwa Simba na baadaye Supersport ya Afrika Kusini ambako alistaafia. Hakuwa na mafanikio sana katika ngazi ya timu ya taifa ambayo alimudu kucheza mechi mbili.
Kama alivyokuwa anatulia kwenye klabu moja wakati akisakata soka, Matola hajawa na tabia ya kutangatanga tangu aanze kufundisha. Ameshabeba majukuku kwenye klabu mbili tu yaani Simba na Lipuli ya Iringa ambako pia alikuwa kocha msaidizi.
Kwa jicho la ndani, kimajukumu wakati akiwa Lipuli kiungo huyo wa zamani alikuwa ni kama kocha mkuu ingawa alikuwa chini ya Amri Said, mchezaji mwingine wa zamani wa Simba.
Amekuwa akitumikia nafasi hiyo ya usaidizi kwa kuwa hakuwa na vyeti vinavyotakiwa kusimama kwenye benchi la ufundi kama kocha mkuu. Ili kuongoza klabu ya Ligi Kuu kocha anatakiwa awe na leseni A ya CAF kama kanuni zinavyotaka. Lakini kuanzia 2022 alianza kusomea leseni hiyo na sasa ana sifa zote za kusimama katika benchi la ufundi la klabu yoyote.
Lakini, hadi sasa hajaweza kusimama kwa miguu yake. Pengine ni mapenzi makubwa aliyonayo kwa klabu ya Simba yanayosababisha aone kosa kuondoka klabu hiyo au maslahi mazuri yaliyo kwenye klabu hiyo kongwe, au ni uhusiano mzuri alionao na viongozi wa klabu hiyo ndio unaosababisha aendelee kubaki Mtaa wa Msimbazi.
Wiki iliyopita, Simba ilimtangaza Matola kuwa kaimu kocha mkuu baada ya kocha raia wa Afrika Kusini, David Fadlu kuiacha timu hiyo ikiwa Botswana ambako ilikwenda kucheza mechi ya kwanza ya raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.
Wakati viongozi wakisaka kocha mwingine, Matola alipewa jukumu la kuiongoza Simba katika mechi ya Ligi Kuu huku kocha wa Taifa Stars, Hemed Morocco akipewa jukumu la kuiongoza katika mechi ya marudiano. Sababu ilikuwa rahisi tu; Matola alikuwa na adhabu ya kukosa mechi moja kutokana na sekeseke lililotokea katika mechi dhidi ya Al Masry msimu uliopita.
Baada ya hapo Simba imemleta kocha Mbulgaria Dimitar Pantev. Lakini imebainika kuwa Mbulgaria huyo hana leseni ya UEFA Pro A ambayo ndiyo inatumika kulinganisha na leseni A ya CAF kwa makocha wanaotoka nje ya Bara la Afrika.
Kwa maana hiyo, Pantev amepachikwa cheo cha meneja mkuu ambacho kinaonekana ni danganya toto kwa kuwa ni vigumu kwa klabu ya Tanzania kumleta mgeni kuja kufanya kazi ya kusimamia masuala yote ya usajili wa wachezaji, ajira za benchi la ufundi na kuweka malengo ambayo yatatakiwa yatekelezwe na kocha mkuu.
Kwa kifupi, kazi ya meneja ni kuangalia masuala yote yahusuyo fedha katika timu kusaka vipaji, usajili wa wachezaji na kuzungumza na vyombo vya habari wakati kazi ya kocha ni kujikita kwenye timu na mechi zake, kufundisha na kuendeleza mbinu za timu, kuongoza mazoezi kuiandaa timu kushinda huku masuala ya nje ya uwanja yakishughulikiwa na meneja mkuu.
Kwa Mbulgaria aliyekuja na wasaidizi wake huwezi kutegemea akae jukwaani kuangalia jinsi kocha mkuu anavyotafsiri mikakati yake wakati atakapokuwa kwenye mazoezi na mechi.
Ni dhahiri Simba hawakuangalia tofauti hizo za majukumu ya wawili hao, bali wametaka kutumia cheo cha meneja kama kinavyotumika Ulaya ambako ndiye anahusika na majukumu yote ya timu akiwa na wasaidizi wake kama kocha wa kikosi cha kwanza, wa makipa na wa viungo.
Kwa vyovyote vile, Matola hatakuwa na majukumu ya kocha mkuu kama anavyotambulishwa nje. Badala yake atakuwa pale kwa ajili ya kuunganisha viongozi na benchi la ufundi na si kusimama kama kocha mkuu. Kadiri atakavyoendelea kupewa majukumu ya namna hiyo kwa namna moja atanufaika na mbinu tofauti za makocha wanaokuja kuwa mabosi wake, lakini kwa jicho kubwa zaidi atakuwa anaendelea kudhoofisha stadi zake na kutoaminika kubeba majukumu makubwa.
Akiwa na miaka 47, Matola sasa anatakiwa aondoke kwenye kivuli cha wageni na kuanza maisha mapya kama kocha mkuu. Anatakiwa aanze kuonyesha uwezo wake. Anatakiwa aanze kutengeneza chapa yake kama kocha mkuu. Anatakiwa aanze kuonyesha falsafa yake ya mpira na aanze kukaa meza za mazungumzo kujadili kazi akitanguliza maslahi yake kama kocha mwenye taaluma anayejua thamani yake.
Matola anatakiwa ageuze fikra za viongozi wa klabu ili wamuone kuwa mtaalamu anayetakiwa kufuatwa kwa tahadhari na si yule wa kumuomba aende kushika timu kwa muda au yule wa kuwa msaidizi kila siku. Nimefurahi kusikia kocha wa JKT Tanzania, Ahmed Ali amekataa dau la Simba la kumtaka aende kuwa msaidizi pamoja na Matola akisema alishapita majukumu ya usaidizi. Tungependa kumsikia Matola akitoa maneno kama hayo kwamba usaidizi sasa basi asimame kwa miguu yake na siyo kuwa kivulini mwa wageni.
Ameshasaidia sana makocha wengine na huu ni wakati wake kuanza kusimama kwa miguu yake kwa kuwa ameshamaliza mafunzo ya kumuwezesha kuwa huru.