SHANGWE: Magdalena kama Simbu, arudi akicheka Bongo
Muktasari:
- Mwanadada huyo amevunja rekodi yake binafsi na kuweka alama mpya katika ramani ya michezo ya kimataifa.
ANGA la riadha limeendelea siku chache baada ya Alphonce Simbu kurejea nchini kutoka Japan akiwa na tuzo ya dhahabu ya mbio za marathoni za dunia, kwani jina la Magdalena Shauri limeandika historia kupitia mbio za Chicago Marathon zilizofanyika Oktoba 12, 2025.
Mwanadada huyo amevunja rekodi yake binafsi na kuweka alama mpya katika ramani ya michezo ya kimataifa.
Magdalena ambaye alikuwa anashikilia rekodi ya taifa ya muda wa saa 2:18:41 aliyoiweka 2023 kwenye katika Berlin Marathon alionyesha ubora kwa kuivunja nchini Marekani baada ya kukimbia kwa saa 2:18:03 akiboresha muda wake kwa sekunde 38, licha ya kumaliza nafasi ya tatu akirudi nchini na medali ya shaba.
Mwanariadha Hawi Feysa kutoka Ethiopia aliibuka mshindi wa kwanza upande wa wanawake katika mbio hizo baada ya kutumia saa 2:14:56 akifuatiwa na mwenzake Megertu Alemu kwa 2:17:18 huku Loice Chemnung wa Kenya akimaliza wa nne kwa 2:18:23.
Kumaliza ndani ya tatu bora katika moja ya mbio kubwa sita duniani (World Marathon Majors inayojumuisha Chicago, Berlin, New York, Tokyo, London na Boston) siyo jambo dogo, bali ni matokeo ya nidhamu, bidii, ushirikiano na imani thabiti.
Kwa matokeo hayo, nyota huyo kutoka Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ), amethibitisha kuwa ni miongoni mwa wanariadha bora zaidi duniani kwa sasa katika mbio za marathoni akiweka historia nyingine muhimu kwa Tanzania katika mashindano ya hadhi ya juu duniani na kuwa Mtanzania wa kwanza kumaliza nafasi tatu za juu kwenye mbio hizo.
Hizi hapa ni sababu zilizomfanya Magdalena kufikia mafanikio hayo makubwa - kwa maana ya kuvunja rekodi ya taifa ambayo inatoa funzo sio tu kwa wanariadha wengine, bali kizazi kipya cha Watanzania wenye ndoto kubwa.
NIDHAMU, ARI YA MAFANIKIO
Magdalena ni kielelezo halisi cha nidhamu binafsi, kujitoa na azma katika kazi yake, nidhamu yake imekuwa nguzo kuu katika safari ya mafanikio yake kuanzia mazoezini hadi kwenye mashindano ya kimataifa.
Kwa muda wote wa maandalizi amedhihirisha falsafa ya “hard work pays”, kwamba mafanikio makubwa hayaji kwa bahati bali kazi ya ziada na uthabiti wa akili. Ushirikianao wake na kocha Antony Mwingereza umejenga msingi wa timu imara inayoshirikiana kwa malengo ya pamoja.
Chicago Marathon sio tukio dogo, ni mbio zenye hadhi ya dunia chini ya Shirikisho la Riadha Duniani (WA), hivyo kuweka rekodi katika uwanja huo ni ishara kwamba nidhamu na kujituma kwake sio vya kubahatisha, bali vimejengwa juu ya msingi thabiti wa maadili ya mchezo.
MASHINDANO YA CHINI
Kwa kipindi cha muda mrefu, Magdalena hakushiriki mara kwa mara mashindano makubwa ya nje ya nchi. Hata hivyo alitumia vyema mashindano ya ndani hususan yale ya majeshi (Bamata) yaliyofanyika Zanzibar yaliyomsaidia kurejesha kasi na stamina kupitia mbio za barabarani na viwanjani.
Kushiriki Bamata ambayo kwa Tanzania imekuwa kama Olimpiki ndogo, kuliimarisha uwezo wake wa spidi na kumjenga upya kisaikolojia na kimwili, kwani alishinda medali ya dhahabu jambo lililoashiria kuwa alikuwa akipanda tena kileleni.
Ushiriki ulionyesha umuhimu wa mbio za ndani kama ngazi ya maandalizi kwa wanariadha wa marathoni na kama ulipata nafasi ya kuangalia Chicago Marathon alionekana kupita na 'phase' ya kasi ya tatu-tatu mwanzoni kitu ambacho hakingewezekana bila mashindano ya mazoezi nyumbani.
PROGRAMU YA MAZOEZI
Maandalizi ya muda mrefu ni silaha kubwa ya mafanikio, na Magdalena na timu yake wamekuwa wakifanya programu ya mafunzo chini ya hali ya hewa ya Arusha, mji unaotambulika kimataifa kwa mazingira mazuri ya mazoezi ya riadha.
Ushirikiano wa karibu kati yake, kocha na wanariadha wenzake umewafanya kuwa na mazingira chanya ya maendeleo kwani wote hufanya mazoezi ya pamoja, kusaidiana kisaikolojia na kimwili, huku kila mmoja akiwa na lengo la kubeba bendera ya Tanzania kimataifa.
Mazoezi hayo ya muda mrefu yamefanyika kwa utaratibu yakijumuisha vipindi tofauti ambao ndio msingi uliomwezesha kuwa na uthabiti wa mwili na akili kwenye mbio ndefu kama za Chicago.
SAPOTI KAZINI
Magdalena ni mwanajeshi, na kazini kwake anapata sapoti ya hali ya juu kutoka Jeshi la Ulizi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kwani wamemruhusu kushiriki kwenye programu za mazoezi bila vikwazo wakimpa nafasi ya kujiandaa ipasavyo.
Jeshi limekuwa mstari wa mbele kumtia moyo, kumpa ruhusa za mazoezi na hata kushughulikia changamoto zingine, lengo likiwa ni kutoa nafasi kwake kuiwakilisha vyema nchi na huo ndio mfano mzuri wa jinsi taasisi za kijeshi zinavyoweza kusaidia kukuza michezo nchini. Na kwa maana hiyo mafanikio yake siyo binafsi tu, bali pia ni sifa kwa JWTZ kama taasisi inayowezesha.
BONASI, MOTISHA
Motisha ni sehemu muhimu ya mafanikio na serikali imeanzisha utaratibu wa kuwapa bonasi wanamichezo wanaofanya vizuri kimataifa mfano bora ni Alphonce Simbu aliyepewa zawadi baada ya kushinda mashindano ya dunia.
Motisha hiyo imekuwa kichocheo kwa wanariadha wengine akiwemo Magdalena, kwani inawapa matumaini kwamba juhuzi zao hazitapotea bure.
Matokeo yake, wanariadha wengi sasa wanafanya mazoezi kwa nidhamu na bidii wakijua kwamba mafanikio yatawapa heshima na thawabu kutoka serikalini na hii imeibua ushindani chanya unaoinua hadhi ya riadha nchini.
HALI YA HEWA NA MAFUNZO
Arusha imekuwa kituo cha maandalizi bora kwa wanariadha wa Tanzania kutokana na hali yake ya hewa yenye uwiano wa baridi na joto, kocha Mwingereza amekuwa akitumia mbinu ya kuwazowesha wanariadha mazingira tofuati ya hali ya hewa (asubuhi, mchana, jioni) ili miili iwe na uwezo wa kustahimili mabadiliko yoyote.
Mbinu hiyo imemsaidia Magdalena kuzoea hali mbalimbali, iwe joto kali au baridi jambo lililompa faida kubwa aliposhiriki Chicago Marathon kwenye hali ya hewa isiyotabirika.
Mfano mzuri ni wakati Simbu akishiriki mashindano ya dunia Tokyo, Japan, Septemba mwaka huu ambako hali ya hewa ilibadilika ghafla lakini hakuyumba kwa sababu ya aina hiyo ya maandalizi, na sasa mbinu hiyo imeonyesha matokeo makubwa kwa Magdalena.
MAANDALIZI YA DUNIA
Kabla ya kwenda Chicago, Magdalena alikuwa sehemu ya programu ya maandalizi ya mashindano ya dunia 2025 pamoja na wanariadha wengine wakiwamo Simbu, Failuna Abdi na Josephat Gisemo.
Ingawa hakufanikiwa kushiriki kutokana na kuchelewa kufanyiwa vipimo vya jinsia, mazoezi hayo ya hali ya juu hayakwenda bure kwani yalijenga msingi wa uimara wa mwili na akili uliomsaidia katika Chicago Marathon.
Kwa maneno mengine, maandalizi hayo ndiyo yaliyohamishwa moja kwa moja kwenye mashindano ya Chicago na yakazaa matunda.
Ufanisi hauji kwa bahati, unahitaji maono, nidhamu na moyo wa kupambana bila kuchoka, hivyo kuvunja rekodi ya taifa na kumaliza nafasi ya tatu kwenye mbio za Chicago ni ushindi wa kitaifa.
Ni ushahidi kwamba Tanzania ina uwezo wa kutoa wanariadha wa viwango vya dunia kama tu mazingira ya mafunzo, ushirikiano, motisha vitatunzwa. Magdalena si tu mwanariadha, bali ni nembo ya ujasiri wa mwanamke Mtanzania anayepambana kwenye medani ya kimataifa kwa uadilifu, bidii na nidhamu na mafanikio yake yanafungua ukurasa mpya wa matumaini kwa wanariadha chipukizi nchini.