Simba Queens inavyojengwa upya kurudisha utawala wake
Muktasari:
- Katika kujipanga huko, Simba Queens inataka heshima iliyoiweka misimu miwili mfululizo 2022-2023 na 2023-2024 kwa kubeba ubingwa wa ligi hiyo, inarejea.
KITENDO cha Simba Queens msimu uliopita kuukosa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara (WPL) uliochukuliwa mikononi mwao na JKT Queens, mabosi wa timu hiyo wakaumiza kichwa, wakajipanga upya wakiwa na lengo la kurudisha ufalme wao.
Katika kujipanga huko, Simba Queens inataka heshima iliyoiweka misimu miwili mfululizo 2022-2023 na 2023-2024 kwa kubeba ubingwa wa ligi hiyo, inarejea.
Mpango wa kwanza ulikuwa ni kupitisha fagio kwa wachezaji ambao iliamini hawawezi kuisaidia na kuingiza wapya kutoka katika ligi mbalimbali ili kuongeza nguvu katika kikosi hicho cha kinadada cha Wekundu wa Msimbazi.
Timu hiyo imeachana na wachezaji 13 na tayari imeshatambulisha wapya 11 ili kuziba mapengo ya walioondoka na Mwanaspoti linakuchambulia nyota hao na rekodi kutoka timu walizotoka.
1. Cynthia Musungu
Siyo mgeni kwenye ligi ya Bongo kwani aliwahi kuitumikia Fountain Gate Princess na ameshatambulishwa Msimbazi akitokea Besiktas ya Uturuki.
Mkenya huyo aliichezea Fountain Gate Princess ambako alikuwa msaada mkubwa akiifanya kuwa timu tishio nchini huku akiwa mwiba mkali kwa Yanga Princess akiifunga katika michezo yote aliyokutana nayo msimu wa 2021/22.
Cynthia ni miongoni mwa usajili ambao kama atapata nafasi ya kuanza kikosini anaweza kuwa msaada mkubwa kwa timu hiyo kwani tayari ameshacheza na anaifahamu ligi. Kasi, nguvu, uamuzi sahihi na uwezo mkubwa wa kufumania nyavu ni miongoni mwa sifa zilizowavutia mabosi wa Msimbazi.
Kabla ya Besiktas, alicheza Kryvbas FC ya Ligi Kuu ya Wanawake Ukraine 2023 akiisaidia kunyakua makombe ya ligi yaliyoifanya icheze michuano ya UEFA Women’s Champions League.
2. Ruth Aturo
Simba imewapa mkono wa kwaheri makipa wawili Carolyne Rufaa aliyekuwa nje ya uwanja kwa takriban msimu mzima akiuguza majeraha na Gelwa Yona, lakini ikiendelea na Janet Shija na Winifrida Ceda.
Kipa Ruth Aturo amesajiliwa akitokea Tausi iliyopanda daraja msimu huu akitajwa kuwa mbadala wa Mkenya Carolyne.
Ruth ni miongoni mwa makipa wenye uzoefu hasa kimataifa hivyo anaweza kuisaidia Simba msimu ujao ambao imepanga kuanza upya. Mbali na kuwa kiongozi uwanjani ni kipa anayejua kucheza mipira ya juu, mguuni na mzuri wa kuanzisha mashambulizi kutokea chini.
Hii ni mara yake ya kwanza kucheza Tanzania na ndani ya muda mfupi aliisaidia Tausi kupanda daraja. Amewahi kupita Kawempe Muslim na UCU Lady Cardinals za Uganda, FC KTP ya Finland, Al Shabab na Altaqadum za Saudia Arabia na Vihiga Queens ya Kenya.
Ndiye kipa namba moja wa timu ya taifa Uganda na amekuwa na mafanikio binafsi ikiwemo kuchukua tuzo ya mchezaji bora wa kike Uganda (2018), kipa bora wa Cecafa kwa wanawake (2018) na kipa bora wa Cosafa Women’s Championship mwaka huohuo.
3. Zawadi Usanase
Ni mshambuliaji mwenye kasi, nguvu na uamuzi mzuri anapolikaribia lango na alikuwa na takwimu nzuri alipoitumikia AS Kigali ya Rwanda. Uwepo wake Msimbazi unakwenda kuongeza ushindani na Jentrix Shikangwa.
Ndani ya misimu mitatu aliyocheza Simba, Shikangwa msimu wa kwanza aliipa timu hiyo ubingwa na akaibuka mfungaji bora akitupia kambani mabao 17. Msimu uliofuata alimaliza na mabao manane akicheza mechi nane na uliopita amemaliza na mabao 24. Licha ya takwimu nzuri alizokuwa nazo Mkenya huyo lakini Simba imeachana naye. Ndiye anayetazamwa kuchukua nafasi yake ni Usanase akitokea Kigali.
Katika ligi ya Rwanda msimu ulioisha Usanase alimaliza na tuzo ya mfungaji bora akitupia mabao 28. Kiasili ni mshambuliaji wa kati, lakini anamudu kucheza nafasi ya winga zote mbili kwa kasi, nguvu na ubora wa kufunga.
4. Neema Mtunzi
Neema Mtunzi ni moja ya silaha itakayokuwa lulu kwa taifa miaka ijayo kutokana na uwezo wa kuzuia mipira ya juu na mzuri wa kupiga faulo na kona.
Simba imemsajili akitokea Mount Hanang ya mkoani Manyara ambayo inashiriki Ligi Daraja la Kwanza. Eneo analocheza wapo wachezaji kama Ruth Ingosi, Ester Mayala na wengineo ambao wamekuwa na namba kwenye kikosi wakicheza mechi mbalimbali za ligi na kimataifa.
Kinda huyo bado hana uzoefu mkubwa kwani michuano aliyoshiriki pekee ni ya Ligi Daraja la Kwanza. Kwa ufupi, Simba ndiyo timu ya kwanza kuchezea kwenye Ligi Kuu.
5. Odoma Amarachi
Huu ni msimu wake wa kwanza kuitumikia Ligi Kuu ya Wanawake Bara akisajiliwa kutokea Edo Queens ya Nigeria.
Amarachi anamudu kucheza nafasi ya kiungo mkabaji na beki zote za pembeni, na ndiye mbadala wa kiungo Ritticia Nabbosa ambaye aliachwa msimu huu akatimkia Yanga. Ni mchezaji wa timu ya taifa Nigeria, ingawa mara ya mwisho hakuitwa kwenye kikosi hicho kilichocheza mashindano ya Wafcon ambapo Nigeria 'Super Falcons' waliibuka mabingwa.
Odoma ametoka katika Ligi Kuu ya Nigeria ambayo haina ushindani kama ilivyo Tanzania kwa sasa, na miongoni mwa vitu vilivyowashawishi mabosi wa Simba kumsajili ni uwezo wa kupiga pasi na wepesi wa kuonekana kwenye matukio muhimu uwanjani.
6. Elizabeth Nashon
Eliza anamudu kucheza kama kiungo mkabaji, kiungo mshambuliaji na beki zote za pembeni huku sifa yake kubwa ikiwa ni kasi na akili ya mpira.
Simba imemsajili mchezaji huyo kutoka Ceasiaa Queens ambayo aliitumikia kwa miezi sita akitokea Gets Program. Licha ya kucheza kwa kiwango bora Ceasiaa, kwenye nafasi ya kiungo wapo nyota watano wa kigeni hivyo kama ataonyesha ubora wake na huenda akaaminiwa ndani ya timu hiyo.
7. Nandede Zainah
Nyota mwingine aliyetambulishwa Msimbazi ni Nandede ambaye anamudu kucheza nafasi ya winga zote mbili kwa ufanisi akisifika zaidi kwa nguvu, kasi na maarifa. Ujio wa winga huyo unakuja kuziba nafasi ya Asha Djafar aliyepewa mkono wa kwaheri ambapo aliitumikia Simba kwa takriban misimu minane.
Mchezaji huyo aliyemaliza mkataba na Kampala Queens ya Uganda na kuibuka na tuzo ya mchezaji bora wa ligi ya nchi hiyo anakwenda kuongeza nguvu eneo la winga kutokana na kasi yake. Akiwa na Kampala Queens msimu uliopita alifunga mabao manane na kutoa asisti mbili akiisaidia kutwaa ubingwa wa ligi.
8. Elizabeth Joseph
Kiungo huyo amejiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Alliance Girls iliyompa nafasi baada ya kumuona akiwa na Singida Warriors.
Elizabeth anamudu kucheza nafasi ya kiungo mkabaji, kiungo mshambuliaji na nafasi zote za beki, na ni moja ya mastaa chipukizi waliofanya vizuri wakiwa na Alliance Girls msimu uliopita.
Mchezaji huyo anasajiliwa Simba ambayo imeongeza wachezaji kibao kwenye eneo lake, na ina matarajio makubwa ya kusawazisha kile ilichofanya msimu uliopita baada ya kupoteza taji mbele ya JKT.
9. Zanga Brice
Huu unakuwa usajili wa kwanza kwa timu hiyo kusajili beki wa kati kutoka Cameroon ambaye atakwenda kusaidiana na Ester Mayala.
Beki huyo anakwenda kuchukua nafasi ya nahodha Violeth Nickolaus aliyetimka kikosini hapo baada ya kupata ofa FC Masar ya Misri.
Zanga ambaye anatumia mguu wa kushoto anamudu kucheza nafasi mbalimbali ikiwemo beki wa kati, kiungo mkabaji na beki wa kushoto akiwa na uwezo mkubwa wa kuzuia na kucheza mipira ya juu. Kutokana na faida ya kimo chake na kama atapata nafasi ya kucheza, huenda akatengeneza pacha na Mayala.
10. Zuhura Waziri
Ni usajili ulioonekana mapema mwishoni mwa msimu uliopita baada ya Simba kukutana na Ceasiaa na Zuhura kuonyesha kiwango bora cha kupiga mashuti na baadhi ya mashabiki waliohudhuria mechi waliwahi kushawishi mabenchi ya ufundi ya timu zao kumsajili.
Zuhura aliitokea Ceasiaa ambayo ilimaliza nafasi ya sita msimu uliopita kwenye WPL na kabla ya hapo aliwahi kuitumikia Tiger Girls na Fountain Gate Princess iliyomlea kwa muda mrefu.
Usajili huo unaweza kuwa na faida kubwa kwani bado ana umri mdogo, hivyo kuwepo katika kikosi hicho kunaweza kumpa uzoefu zaidi na kuwa na faida baadaye.
Kitu kinachomtofautisha Zuhura ni uwezo wake mkubwa wa kutumia miguu akiwa na uwezo wa kuanzisha mashambulizi kutokea golini kwa usahihi jambo ambalo ni nadra kwa makipa wa kike nchini.
11. Asha Omary
Wakati akiwa Yanga Princess hakuwa anapata nafasi kubwa ya kucheza kutokana na ushindani kikosini, na akaishia kusugua benchi mbele ya Protasia Mbunda aliyeonyesha kiwango bora.
Lakini mambo yalibadilika baada ya kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ‘Twiga Stars’ kilichocheza mashindano ya Cecafa Women Championship alikocheza vizuri.
Kocha wa Twiga Stars, Bakari Shime alimjumuisha tena kwenye kikosi kilichocheza mashindano ya Wafcon nchini Morocco alikocheza mechi zote za makundi.
Uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali kuanzia beki ya kushoto, kulia na hata winga zote mbili ulianza kuwavutia mabosi wa timu mbalimbali na Simba ikashinda vita na kumsajili. Eneo la ulinzi la Simba linamtegemea Doto Evarist, hivyo kuongezeka kwa Asha ambaye ni mzuri kwenye kukaba na kushambulia kwa kasi kutaongeza ushindani.
12. Fasila Adhiambo
Msimu uliomalizika wa Ligi Kuu Kenya alifunga mabao saba na kutoa asisti 17 akitajwa kuwa miongoni mwa wachezaji waliofanya vizuri.
Awali, ilielezwa Simba ilimfuata, lakini kulikuwa na ugumu hasa upande wa baba yake mzazi aliyetamani bintiye aendelee kucheza Ulinzi Starlets ili aajiriwe jeshini badala ya kucheza soka la kulipwa.
Katika eneo la kiungo mshambuliaji ambalo ndilo asili analocheza Adhiambo Wekundu wa Msimbazi tayari wameachana na Precious Christopher, hivyo ujio wake unaweza kuongeza kitu kwenye kikosi hicho.
Akiwa na umri wa miaka 20 na uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi na kufunga, ataisaidia Simba ambayo kwenye eneo hilo ilikuwa na changamoto hasa za ufanisi mbele ya lango.
DONDOO
2016 Msimu ambao Ligi Kuu ya Wanawake iliasisiwa na Mlandizi Queens ilibeba ubingwa
04 Idadi ya mataji ya Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) iliyotwaa Simba ikilingana na JKT Tanzania
2020 Mwaka wa kwanza kwa Simba Queens kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL)
2024 Ndio mwaka wa mwisho kwa Simba Queens kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake.
03 Idadi ya timu pekee zilizotwaa ubingwa katika misimu tisa ya Ligi Kuu ya Wanawake tangu 2016.