Prime
TAFCA mko wapi makocha wazawa wananyanyasika
SELEMANI Matola ndiye kocha mkuu wa Simba ambaye sio kocha mkuu...hii inatatanisha kidogo. Ni kwamba Simba imemsajili Seleman Matola kama kocha wake mkuu kwenye vitabu vya TFF na CAF, lakini uwanjani yeye sio kocha mkuu.
Nafasi hiyo imeenda kwa Dimitar Pantev, ambaye hata hivyo amesajiliwa kama meneja mkuu. Hii ni kwa sababu raia huyo wa Bulgaria hana vigezo vya kumfanya asajiliwe kama kocha mkuu...yaani hana vyeti. Kwa hiyo vyeti vya Matola vitatumika kwenye vitabu vya TFF na CAF huku Pantev ambaye hana vyeti ndio atakuwa akifundisha.
Huu ni muendelezo ya unyanyasaji wa makocha wa wazawa hapa nchini. Tulikuwa tunasema makocha wazawa hawapewi timu kuziongoza kwa sababu hawana elimu ya kutosha. Haya, wamesoma na wana vyeti vikubwa...bado tunawaleta makocha wa kigeni wasio na vyeti. Kuna orodha kubwa sana ya makocha wazawa ambao wamekuwa wakinyqnyasika katika nchi yao licha ya kufanya kazi zilizotukuka.
Fred Felix 'Minziro' aliipandisha Singida United mwaka 2017, akaondolewa kisha timu kukabidhiwa kwa Mdachi Hans van der Pluijm. Akaipandisha KMC 2018, akaondolewa tena na timu ikakabidhiwa kwa mrundi Ettiene Ndayiragije.
Mbwana Makata aliipandisha Alliance ya Mwanza, lakini akawekwa pembeni na timu ikakabidhiwa kwa Mnyarwanda Baptista Kayiranga. Msimu huu wa 2025/26 kuna makocha sita tu wazawa katika timu 16 za ligi kuu.
Mbeya City - Malale Hamsini (Tanzania)
Simba - Mapicha picha
Singida BS - Miguel Gamondi (Argentina)
JKT Tanzania - Hamad Ally (Tanzania)
Namungo - Juma Mgunda (Tanzania)
Pamba Jiji - Francis Baraza (Kenya)
Yanga - Patrick Mabedi (Malawi)
Azam FC - Florent Ibenge (Ufaransa/DRC)
Mtibwa Sugar - Yusuf Chipo (Kenya)
Coastal Union - Mohamed Muya (Tanzania)
Dodoma Jiji - Mashami Vicent (Rwanda)
Mashujaa - Salum Mayanga (Tanzania)
TZ Prisons- Zedekiah Otieno (Kenya)
KMC - Marcio Maximo (Brazil)
Fountain Gate - Mohamed Laiza (Tanzania)
TRA Utd. - Kefa Kisala (Uganda)
Hii sio dalili nzuri kwa kesho ya soka letu.
TAFCA MKO WAPI
Mtu anayeweza kuwapambania makocha wazawa ni Chama cha Makocha Tanzania (TAFCA). Chama hiki kilianzishwa mwaka 1975 na Mjerumani Bert Trautmann aliyekuja Tanzania mwaka 1974 katika mpango wa msaada wa maendeleo ya kiufundi wa iliyokuwa Ujerumani Magharibi. Trautmann aliona mfumo wa mpira wa Tanzania una makosa mengi hivyo alianza na kuupanga upya.
Hii ligi yetu ya sasa ni matokeo ya mawazo ya Trautmann, kabla ya ujio wake, Tanzania ilikuwa na ligi ya timu 20 zinazocheza kwa mtoano. Akashauri zipunguzwe hadi 12 na ligi ichezwe kwa madaraja na kuhesababu alama kwa mechi za nyumbani na ugenini...mfumo unaotumika hadi sasa. Akaanzisha kliniki za mafunzo ya ukocha kwa wazawa nchi nzima.
Abdallah Kibadeni, kocha aliyefanikiwa kuliko makocha wote waliowahi kufundisha mpira nchini, alianzia kwenye kozi hizi mwaka 1975 Arusha mara tu alipostaafu kuichezea timu ya taifa.
Makocha waliofanya vizuri kwenye mafunzo ya nchini, walipelekwa Cologne Ujerumani na Trautmann mwenyewe, kwa ajili ya mafunzo zaidi...mmoja wao ni marehemu Joel Bendera, ambaye aliporudi akawa kwenye benchi la ufundi la Taifa Stars iliyofuzu kwa AFCON 1980.
Ili kuhakikisha mafunzo yanaendelea hata atakapoondoka, Trautmann alianzisha chama kitakachosimamia na kuendesha mafunzo kwa makocha, chama hicho ndiyo TAFCA. Leo hii ni miaka 50, TAFCA haijazalisha Kibadeni mwingine, wala Bendera mwingine, ipo ipo tu. Makocha wachache walioibuka kibahati bahati wananyanyaswa...TAFCA haisemi kitu. Matokeo ya haya yote ni kukosa makocha washindani kwenye tasnia.
Pata picha ni kocha mmoja tu Mtanzania ambaye amewahi kufundisha timu ya taifa jingine, naye ni Dani Korosso aliyefundisha Botswana. Na ni kocha mmoja tu Mtanzania ambaye alitwaa ubingwa nje ya nchi, naye ni Sunday Kayuni aliyeshinda ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya mwaka 1998.
Kocha wa mwisho mzawa kushinda ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania ni John Semkoko aliyeshinda akiwa na Mtibwa Sugar mwaka 20000 (na 1999). Hizi rekodi ni mbaya sana kwa makocha wazawa, na TAFCA ipo tu.
Juma Mwambusi ndio kocha pekee mzawa kuwahi kumaliza ligi kwenye nafasi za juu. Alimaliza nafasi ya pili akiwa na TZ Prisons msimu wa 2008/09. Akiwa na Mbeya City alimaliza nafasi ya tatu msimu wa 2013/14, sawa na Mecky Mexime msimu wa 2016/17.
Kama chama cha kitaalamu chenye majukumu ya kusimamia ustawi na maslahi ya makocha wazawa, TAFCA inapaswa kujipanga na kuhakikisha inabadili hali ya upepo. Sasa hivi ni kawaida kuona timu zikiajiri makocha wakuu na wasaidizi wao wote kutoka nje ya nchi. Tuichukulie Azam FC kama mfano:
Kocha mkuu: Florent Ibenge (DRC)
Msaidizi namba 1: (Addis Worku (Ethiopia)
Msaidizi namba 2: Aniceth Kaniziyad (DRC)
Msaidizi namba 3: Kassim Liogope (Tanzania).
Sasa hapo unadhani makocha wazawa wana nafasi gani ya kufanikiwa? Hapa ndipo chama cha makocha kinatakiwa kusimama imara na kupeleka pendekezo TFF wakati wa matayarisho ya utungaji wa kanuni za ligi hili suala liangaliwe. Yaani Mtanzania anakuwa msaidizi namba tatu...tutafika wapi?
Bert Trautmann alifariki dunia 2013, lakini TAFCA yake unaweza kusema ilishajifia siku nyingi kabla, limebaki jina tu. TAFCA, amkeni kutoka usingizi mzito muwasaidie makocha wazawa.