Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tunahitaji 'kiburi' kumsimamisha Victor Osimhen na wenzake

HISIA Pict


HAKUNA kingine. Tunahitaji kuwa viburi tu leo tutakapoingia uwanjani kucheza na kina Victor Osimhen. Labda nasi tuna nafasi ya kuonyesha ni namna gani mpira wa Afrika umebadilika katika soka hili la Afrika wakati tutakapocheza na Nigeria pale Rabat.


Huku mtaani kwetu huwa tunasema 'maiti imemng'ang'ania muoshaji'. Inawezekana. Binafsi sina uoga sana na Nigeria ya sasa wala Tunisia ya sasa. Sina wasiwasi. Wameshuka kwa kiasi kikubwa. Labda ni vile tu nasi wenyewe hatupandi kwa kasi kama ilivyo kwa nchi nyingi za Afrika ambazo zamani zilikuwa chini.


Kwa wale wanaotandika mkeka wanajua namna gani mpira wa Afrika katika timu za taifa hautabiriki. Kucheza na Comoro siku hizi sio jambo rahisi. Kucheza na Madagascar siku hizi siyo kazi rahisi. Ghana ikicheza na Comoro pambano ni gumu na ghafla unasikia Ghana imefungwa. Taifa Stars inaweza kufanya hivyo leo? Inawezekana.

Nigeria hii sio ya Jay Jay Okocha, Sunday Oliseh, Nwankwo Kanu wala Celestine Babayaro. Bado wachezaji wao wametupita viwango lakini kwa viwango walivyojiwekea wenyewe na wakubwa wenzao nadhani Wanigeria wameshuka. Ni vile tu nina wasiwasi na sisi hatuwasogelei.

Mataifa ambayo nayaogopa zaidi kwa sasa Afrika ni Morocco na Senegal. Wana wachezaji walioiva wakicheza katika kiwango cha juu zaidi wakiongozwa na kina Achraf Hakimi na Sadio Mane. Nahisi moja kati ya mataifa haya atakwenda moja kwa moja kucheza fainali au kuchukua taji lenyewe.

HISI 01

Kwa sasa sisi Tanzania tunaweza kujivunia mambo manne. Kuna ongezeko la wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya mipaka yetu, ingawa hawachezi katika kiwango cha juu. Ni Mbwana Samatta na Novatus Dismas ndio ambao wanacheza katika ligi kubwa. Wakati Samatta akiwa anacheza Le Havre ya Ligi Kuu ya Ufaransa, Novatus anacheza Gotzepe ya Ligi Kuu ya Uturuki.

Wengine hawa kina Haji Mnoga wanacheza nje ya mipaka yetu lakini hawapo ligi kubwa. Hata hivyo, tumejitahidi kiasi kuanzia wakati ule Taifa Stars ilipokuwa chini ya Marcio Maximo. First Eleven yake ya Ivo Mapunda, Shadrack Nsajigwa, Mecky Maxime, Victor Costa, Salum Swedi 'Kussi', Shaaban Nditi, Henry Joseph, Athuman Idd 'Chuji' Nizar Khalfan, Said Maulid 'SMG' na Gaudence Mwaikimba yote ilikuwa inacheza Ligi ya ndani.

Kitu kingine ni kwamba wachezaji wetu wengi wa sasa wamepitia katika timu za vijana. Wamecheza U17, U21 na U23. Wamekutana na timu za taifa za nje kwa muda mrefu, hivyo wana kile kitu kinaitwa 'exposure'.

HISI 02

Mpira unatembea kwa kiasi kikubwa hata kama hatupati matokeo ambayo tunayahitaji. Zamani ilikuwa tunabutua zaidi lakini sasa hivi walau tunajaribu kutembeza mpira.

Kitu kingine ambacho tunaweza kujivunia kwa sasa ni hata wachezaji wetu wa ndani wanacheza kiushindani katika mechi za vilabu michuano ya CAF.

Timu zao, hasa Simba, Yanga na Azam zinajaribu kwenda mbali katika mechi za Ligi ya Mabingwa na Shirikisho. Wachezaji wanajiongezea idadi kubwa ya mechi wanapofika makundi kisha wakatinga robo fainali.

HISI 03

Wapo wengine waliocheza fainali za Shirikisho katika miaka ya karibuni. Kina Shomari Kapombe, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Bakar Mwamnyeto, Dickson Job, Kibu Dennis na wengineo hawawezi kushangaa sana mechi kama hizi za kishindani. Kina Chuji walikuwa wanaishia hatua za awali tu wakati ule.

Labda hii inasaidia kwa kiasi fulani kuona mpira unatembea tofauti na zamani inaweza ikawa sababu nyingine ya maiti kumng'ang'ania muoshaji leo.

Naamini tunaweza kufanya jambo kama wachezaji watakuwa na viburi chanya huku pia tukijikumbusha mpira wa Afrika umebadilika na hawa kina Nigeria sio wale kama wa zamani.

HISI 04

Hakuna kundi ambalo Tanzania itapangwa na wataiona michuano kuwa mepesi. Michuano iliyopita pale Ivory Coast tulipangwa na Morocco, Zambia na DR Congo. Wote hawa wametuzidi mpira, lakini tulifanikiwa kuambulia pointi mbili. Haikuwahi kutokea katika historia yetu kukusanya pointi mbili katika michuano hii.

Silaha nyingine ambayo tunaweza kuwa nayo ni kocha mkuu, Manuel Gamondi. Bado ametuachia kumbukumbu nzuri ya soka zuri ambalo Yanga walikuwa wanacheza. Anaweza kuviunganisha vipaji vya Tanzania na kufanya jambo katika michuano hii akianzia na pambano la kesho dhidi ya Nigeria? Binafsi naweka matumaini kwake.

Kuhusu suala la kushambulia na kutengeneza nafasi sina wasiwasi sana na Gamondi. Nataka tu tupime nidhamu yake ya ulinzi dhidi ya kina Osimhen. Hili ni jambo ambalo litatuokoa katika michuano hii. Licha ya kwamba tunajifariji Nigeria hawa sio kama wale kina Okocha, lakini tunalazimika kuwapa heshima yao. Bado wametuzidi.

HISI 05

Gamondi amekaa na timu muda mrefu pale Misri na nadhani ameijua vema timu yake. Uzuri ni kwamba anawajua wachezaji wetu kwa sababu sio kocha mpya nchini. Hata wale ambao hakuwafundisha Yanga na Singida Big Stars anawafahamu. Hata wakati anakubali kazi ya kuifundisha Stars alikuwa anajua nini cha kutarajia kutoka kwa wachezaji wake.

Sijui anaitamani hii kazi iwe ya kudumu au vinginevyo, lakini Stars wakibadilika kimchezo tu basi Gamondi kazi inaweza kumganda. Tuanze na le dhidi ya wakubwa Nigeria halafu tutaulizana tena nini cha kufanya dhidi ya Tunisia. Nao sina hofu nao. Ni wachezaji gani wakubwa wa Tunisia wanaotamba Ulaya? Ilikuwa zamani. Sasa hivi wana timu ya kawaida tu labda kwa vile na sisi hatusogei juu kwa kasi.

Eneo pekee linalonitia wasiwasi katika kikosi cha Taifa Stars ni langoni. Yakoub Suleiman ndiye kipa wetu namba moja, lakini hajatimiza mwaka tangu alipokaa kwa mara ya kwanza katika lango la Taifa Stars. Na wala hana miezi tangu alipocheza pambano lake la kwanza la michuano ya CAF akiwa na jezi ya Simba. Ajiandae kisaikolojia katika michuano hii.