Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ubora anaoingiza Damaro pale Yanga

DAMARO Pict


KLABU ya Yanga imekamilisha usajili wa kiungo nyota, Mohamed Damaro Camara, aliyejiunga na timu hiyo katika dirisha hili dogo lililofunguliwa rasmi kuanzia Januari 1, 2026, baada ya mchezaji huyo kuachana na kikosi cha Singida Black Stars.


Kiungo huyo anayesifika kwa ukabaji amekuwa ni mchezaji wa pili wa Yanga kusajiliwa  dirisha hili dogo baada ya mshambuliaji Emmanuel Mwanengo aliyeachana na TRA United (zamani Tabora United kwa makubaliano ya pande mbili.


Damaro aliyejiunga na Singida kwa mara ya kwanza Julai 27, 2024, akitokea Hafia FC ya kwao Guinea, ni miongoni mwa nyota watatu waliopewa uraia wa Tanzania, baada ya Josaphat Arthur Bada aliyezaliwa Ivory Coast na Emmanuel Keyekeh wa Ghana.

Usajili wa Damaro katika kikosi cha Yanga chini ya Kocha, Pedro Goncalves, ni miongoni mwa nyota wanaotazamwa zaidi ili kuongeza ushindani kwenye nafasi ya kiungo mkabaji, japo licha ya ubora wake ila ataongeza kitu gani kingine cha ziada?

DAMA 01

USHINDANI WA NAFASI

Kuongezeka kwa Damaro kunaongeza faida ya ushindani kati ya mchezaji mmoja na mwingine kwani itatoa wigo mpana kwa kocha kufanya mabadiliko pale itakapomlazimu, kutokana na kikosi hicho kushiriki michuano mingi msimu huu ya ndani na nje pia.

Ujio wa Damaro unatoa ushindani kwa viungo wengine ambao mara kadhaa wamekuwa wakitumika kucheza eneo la kiungo mkabaji, akiwemo Aziz Andabwile na Duke Abuya ambaye ameonekana akicheza nafasi hiyo, licha ya kiasili kusogea zaidi namba nane.

Kiungo, Moussa Balla Conte aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu akitokea CS Sfaxien ya Tunisia, ni miongoni mwa nyota walioaminika wangeleta ushindani, ingawa mambo yamekuwa ni tofauti na sasa anataka kutolewa kwa mkopo dirisha hili dogo.

Conte aliyekuwa akihusishwa na Simba pia kipindi cha, Fadlu Davids kabla ya Yanga kuinasa saini ya nyota huyo Julai 18, 2025, ameshindwa kupenya kikosi cha kwanza, tangu uwepo wa Kocha, Mfaransa Romain Folz na hata, Mreno Pedro Goncalves.

Folz aliyejiunga na Yanga Julai 23, 2025, alitarajiwa angemtumia kiungo huyo kutokana na ushindani mkubwa uliokuwepo wa kumpata kutoka kwa Simba iliyomuhitaji pia, ingawa hadi anaondoka Oktoba 18, 2025, alimtumia, Aziz Andabwile eneo hilo.

DAMA 02

KULINDA SAFU YA KUJILINDA

Miongoni mwa sifa kubwa kwa Damaro ni kuweza kulinda vizuri safu ya kujilinda na hilo amelionyesha akiwa na kikosi cha Singida Black Stars, jambo linaloweza kuipa Yanga faida kutokana na ubora wa nyota waliopo katika kuunganisha timu hiyo.

Damaro hajaanza vizuri msimu huu na Singida kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara yaliyokuwa yanafanywa na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi ambaye kwa sasa amepewa tena majukumu mapya ya Mkurugenzi wa Ufundi wa kikosi hicho.

Kiungo huyo amethibitisha hilo wakati akicheza na nyota mwenzake, Josaphat Arthur Bada anayeichezea kwa sasa JS Kabylie ya Algeria, aliyojiunga nayo Julai 27, 2025, ambapo wawili hao walitengeneza pia uimara katika kikosi hicho cha Singida.

Bada aliyejiunga na Singida kwa mara ya kwanza Agosti 1, 2024, akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast, kiwango chake bora alichokionyesha msimu uliopita akishirikiana na Damaro, ndicho kilichopelekea mabosi wa JS Kabylie ya Algeria kumsajili.

DAMA 03

KUTULIZA MASHAMBULIZI

Sifa nyingine kwa Damaro ni ubora mkubwa alionao wa kukaa na mpira mguuni ambao husaidia sana kutuliza mashambulizi ya timu pinzani tofauti na baadhi ya viungo wengine, jambo litakaloongeza zaidi ubunifu ndani ya kikosi hicho cha Yanga.

Pia, Damaro ana uwezo mkubwa wa kuanzisha mashambuliaji kwa kutoa pasi sahihi kwa viungo wa mbele na wachezaji wanaotoka pembeni, kitu ambacho kinaweza kuisaidia Yanga kipindi inatengeneza mashambulizi na wakati huohuo ikiwa kwenye kuzuia.

DAMA 04

NIDHAMU YA KIUFUNDI

Damaro ni miongoni mwa viungo wanaocheza eneo la katikati na lenye hekaheka nyingi zaidi kwa sababu mashambulizi mengi huwa yanaanzia hapo, ingawa ni mmoja wa kiungo anayejua kucheza kwa nidhamu kubwa ili kuilinda safu yake ya kujilinda.

Kiungo huyo pia ana uwezo wa kudhibiti kasi ya mchezo kutokana na mashambulizi yanayotengenezwa na timu pinzani, ambapo ameonyesha hilo kwa vitendo kwani sio mchezaji utakayemuona akipewa kadi za mara kwa mara, licha ya eneo analolicheza.

DAMA 05

KUJIFUNZA, KUJIENDELEZA

Kuichezea Yanga inaweza ikawa nafasi nzuri pia kwa kiungo huyo kujifunza na kukiendeleza zaidi kiwango chake kutokana na kukutana na uwepo wa wachezaji wakubwa kikosini humo, licha tu ya presha iliyopo ndani ya timu hiyo tofauti na Singida.

Kiungo huyo amecheza na nyota wakubwa tena kwa kiwango kikubwa, ingawa kujiunga kwake na Yanga inaweza ikawa fursa pia nyingine ya kuzidi kuonekana kutokana na ukubwa wa timu hiyo, ikiwa ataonyesha tu ushindani kwa viungo wengine waliopo.


UTAYARI WA KUPAMBANA

Nyota huyo anapaswa kuonyesha utayari wa kupambania namba kila atakapopata nafasi ya kucheza na hili litawezekana ikiwa atakuwa tayari kukabiliana na changamoto mpya, baada ya msimu huu kuuanza vibaya na Singida tofauti na msimu uliopita.

Usajili wa Damaro unaonyesha nyota huyo anaenda kucheza kikosi cha kwanza moja kwa moja kutokana na Moussa Balla Conte aliyetua kwa matarajio makubwa kushindwa kuonyesha ubora, jambo linalosubiriwa kumuona pia atachokifanya.