Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Usajili wa Tshabalala... Baba afichua siri nzito

TSHABALA Pict


MASHABIKI wa Simba bado wanaendelea kumuota beki wa kushoto na nahodha wa zamani wa kikosi hicho cha Msimbazi, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ a.k.a Zimbwe Jr.


Hii ni kwa sababu ameondoka katika klabu hiyo kama utani, ikiwa ni baada ya kuitumikia kwa misimu 11 tangu alipojiunga nayo mwaka 2014 akitokea Kagera Sugar.


Kinachowauma siyo kuondoka kienyeji bila kutarajiwa, bali kitendo cha kuhamia mtaa wa pili kwa watani wao, Yanga ambao kwa misimu minne mfululizo imekuwa ikiwaburuza katika michuano ya ndani ikiwamo Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (FA) mbali na kuwafunga katika Dabi ya Kariakoo.

Kwa sasa beki huyo anaendelea na majukumu yake akiwa na kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kinachoshiriki michuano ya CHAN 2024 ikitinga robo fainali kabla ya kujiunga na mabingwa hao wa Tanzania tayari kwa msimu mpya wa mashindano ya msimu wa 2025-2026.

Hata hivyo, wakati Tshabalala akisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa Yanga kumwona akiwa katika uzi wa rangi ya kijani na njano zinazotumiwa na timu hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kumkosa mara kadhaa katika madirisha ya usajili, baba mzazi wa nyota huyo amefichua siri ya usajili huo.

Hussein Mohamed ‘Sr’, ndiye baba mzazi wa beki huyo mpya wa kushoto wa Yanga, amefunguka ukweli namna ilivyokuwa ngumu kwa Tshabalala kuiacha Simba na kutua Yanga, huku akifichua alivyoamua kuweka pembeni mahaba ya ushabiki aliokuwa nao kwa masilahi ya kijana wake huyo.

Mzee Mohammed amefanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam na kusema yeye ni shabiki wa Yanga kindakindaki, lakini linapokuja suala la maisha ya kijana wake hata alipokuwa Simba hakusita kumuunga mkono na kukiacha kipaji chake akitumie kwa uhuru.

“Kabla ya kujiunga na Yanga kwa ajili ya msimu ujao, niliwahi kusema napenda Yanga iifunge Simba, lakini Tshabalala akiifunga Yanga nitafurahia na kumuunga mkono, ila kwa sasa namkaribisha kwa moyo mmoja kwenye chama langu pendwa.”

Ni moja ya kauli ya Baba Tshabalala katika mahojiano hayo...ebu endelea naye...!

TSHABAL 01

ALITAMANI ASALIE SIMBA

Baba Tshabalala anasema japo yeye ni shabiki wa Yanga lialia, lakini alitamani kuona Tshabalala anamalizia soka lake akiwa Simba, aliyodumu nayo kwa misimu 11 tangu alipojiunga nayo mwaka 2014 akitokea Kagera Sugar.

“Simba imempa hatua kubwa katika maisha yake, watu wasichojua ni kwa mara ya kwanza alikuja kuniuliza, Simba, Yanga na Azam zinahitaji huduma yangu nisaini wapi? Nikamwambia ushabiki wangu hauwezi kufanya nififishe ndoto zako, kasaini unapoona una nafasi ya kucheza,” anasema Mzee Mohammed na kuongeza:

“Yanga ilionyesha nia kwa Tshabalala tangu muda mrefu, miaka minne nyuma, ilibakia kidogo imchukue, lakini alikuwa amebakiza siku chache mkataba wake kuisha, hivyo Simba ikapata nguvu ya kuendelea naye, ninachoweza kukiri, Simba imempa hatua kubwa. Tshabalala itaendelea kusalia katika kumbukumbu za maisha yake na familia kwa jumla.”

TSHABAL 04

YANGA 5-1 SIMBA

Anasema tangu Tshabalala aanze kuichezea Simba, mechi iliyomuumiza ni ile ya Dabi ya Kariakoo ambayo Yanga ilishinda mabao 5-1 ikipigwa Novemba 5, 2023 hasa kwa kitendo cha kumuona kijana wake anatoa machozi, kwani kilifanya akose amani na kujiuliza beki huyo anapitia wakati gani.

“Kitendo cha kumuona analia, furaha ya ushindi wa timu yangu iliingia hitilafu, baada ya mechi nikampigia simu na kumwambia ajikaze, ndio mpira una matokeo ya kikatili,” anasema Mzee huyo na kuongeza;

“Mechi ya Juni 25, 2025 alinipigia simu kuniambia, baba jiandae kuumia, awamu hii tutalipa kisasi kwa bahati mbaya Simba ikafungwa tena mabao 2-0, bado ikawa hali mbaya kwake, tangu nianze kuishabikia Yanga sijawahi kuiona dabi ambayo Simba imefungwa mara tano mfululizo.”

Pamoja na ushabiki kwa Yanga, anakiri Simba ina timu nzuri na kinachotakiwa kwao ni utulivu, ili iweze kurejea kuwania mataji ya ndani na nje.

“Mechi ya mwisho dhidi yao na Yanga ndio iliyoamua ubingwa, imefika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, huwezi kuibeza na kuiona timu mbaya, hawakupaswa kuwaacha wachezaji wao kirahisi, badala yake wangewapa muda wa kuzoeana na wangetengeneza timu ya ushindani mkubwa.”

TSHABAL 03

ALIMZUIA KWENDA NJE

Anasema kwa mara ya kwanza aliiona ofa iliyokuja ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, lakini alimzuia kijana wake aendelee kusalia nchini kwa sababu pesa aliyokuwa anapewa ilizidi kidogo ile anayopata Tanzania.

“Ni kweli ingemuongezea CV katika maisha yake ya soka, lakini anacheza ili atengeneze maisha ya familia yake iishi vizuri, nikamkalisha chini na kumshauri akanielewa kwa sababu ni kijana msikivu pia ana washauri wanaomsimamia,” anasema.

TSHABAL 02

SIRI YA KUTUA YANGA

Mzee huyo anafichua kilichomfanya Tshabalala kutua Yanga, akisema kabla ya kwenda katika jukumu la timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inayoshiriki CHAN 2024, alitamani kumalizana na Simba kabisa, lakini haikuwa hivyo.

“Mkataba wake ulikuwa umeisha kabisa, alitamani anapoenda kuitumikia Stars asiwe na mambo mawili mawili, wakati huo kulikuwepo na ofa ya Yanga na Kaizer Chiefs, badala yake Simba wakaacha aende bila kufikia mwafaka,” anafichua mzee huyo na kuongeza;

“Yanga ikaweka nguvu zaidi ya kuhitaji huduma yake, meneja wake ikabidi aikubali ofa hiyo, baada ya kuona mambo yanasuasua. Mashabiki wa Simba wakawa wananitania umeamua kumshawishi kijana wako ili aje timu unayoishabikia, wafuasi wa Yanga walikuwa na furaha hali halisi ilikuwa ni wao wenyewe (Simba) kushindwa kulimaliza jambo hilo mapema.”

Anafichua ukweli ni kwamba haikuwa rahisi kwa beki huyo kutua Jangwani, kwani akili yake ilikuwa ni kuendelea kuitumikia Simba, ndio maana aliipa kipaumbele, ila mabosi wa klabu walichukulia poa ndipo akaona isiwe tabu na kutua Jangwani, jambo ambalo kama mzazi analifurahia kwa vile ni Yanga damu na ana kiu ya kuona ikizidi kufanya vizuri zaidi kuliko misimu minne waliyoiburuza.

TSHABAL 05

FAIDA, HASARA ZA UMAARUFU

“Tshabalala ni kijana wa ujana wangu, baada ya kuanza kupata umaarufu niliachana na mambo mengi sana ili kulinda brandi yake, huwezi kunikuta na kunjana na mtu ili nipigane ama najiachia kunywa pombe. Nahofia inaweza ikapigwa picha bila kujua ikamchafua mwanangu,” anasema mzee huyo na kuongeza:

“Kuna gharama ya kutumia umaarufu wa mtu, mfano kuna mwingine anaweza akaja hapa katika biashara zangu ninazouza samaki wakavu, akataka nimpe pesa. Nikimwambia sina anaanza kusema, yaani kijana wako katoka kusaini unakosa pesa. Kipindi yupo Simba walikuwa wanasema anacheza timu kubwa, huwezi kukosa pesa.

“Kuna siku niliongozana naye kwenda kufanya mahitaji ya vifaa mjini kwenye duka la Wahindi, watu walijaa na kuanza kuomba kupiga naye picha, akashindwa hata kunisaidia kuchagua vitu nilivyokuwa navitaka na ilikuwa ngumu kuwakataza  wale ni mashabiki zake.”

Kwa upande wa faida, anasema kuna maeneo akifika anapata huduma kirahisi kutokana na ukubwa wa jina la kijana wake:

“Nakumbuka wakati Tshabalala yupo Simba, mimi nilifiwa na mama mzazi (bibi wa Tshabalala), alikuwa ameolewa Burundi hivyo nilitakiwa kusafiri.

“Tshabalala alikuwa anajiandaa na mechi ya kimataifa, hivyo viongozi wa Simba wakawa na hofu wakidhani nahitaji kusafiri naye, nikawaambia aendelee na majukumu yake, aliyefariki ni bibi yake na sio mama yake.

“Wakati nafuatilia mambo ya pasipoti, nikakuta Simba wamelipia kila kitu, hivyo nikaondoka kwa uharaka, ndio maana nasema naiheshimu klabu hiyo, imemfanyia mengi mwanangu.

“Kuna siku Simba ilikuwa Afrika Kusini, nilibanwa na homa kali, sina kawaida ya kumwambia changamoto anapokuwa na majukumu mbele yake, mdogo wake akampigia simu kumwambia, mzee anaumwa sana, akawatuma marafiki zake wanne kuja kuniona, hiyo ni faida ya umaarufu wake.”


ZAWADI KUBWA

Anasema zawadi kubwa aliyopata kutoka kwa Tshabalala ni nyumba ya kifahari, ukiachana na pesa za hapa na pale anazompa kwa ajili ya mahitaji mbalimbali.

“Nakumbuka alinipa pesa ili nimnunulie nyumba kadhaa ikiwemo na ya kwangu, nikazinunua za kwake, baada ya kutoka safari akaja akaziona na kuzipenda sana, akaniuliza ya kwako ipo wapi, nikamjibu bado natafuta, akasema sasa nitakuuzia moja kati ya hizo ulizoninunulia,” anasema Baba Tshabalala na kuongeza:

“Nikamjibu nyumba zako nimenunua kwa gharama kubwa, tofauti na pesa ambazo uliniambia ninunue nyumba ya kwangu, akasema kalete pesa hizo, akazichukua na kuniachia Sh5 milioni mezani na kwenda kubadilisha hati ya nyumba yake na kunipa mimi, kifupi anapenda zaidi anifanyie vitu vya maendeleo na sasa naishi nyumba ya kifahari.”

TSHABAL 07

NAFASI YAKE YANGA

Anasema anatambua katika nafasi ya beki ya kushoto anayokwenda kucheza  Yanga, kuna beki anayefanya vizuri, Chadrack Boka raia wa DR Congo, ila ana imani atakwenda kupambana na kuendeleza kiwango chake.

“Natambua si kitu chepesi unapohamia timu ambayo kuna wachezaji wana ufalme wao, ila Tshabalala anajitambua anataka nini katika kazi yake ni mchezaji anapenda mazoezi binafasi hata akiumwa atafanya tu, kwa upambanaji wake ataonyesha uwezo wa kuisaidia timu yake mpya,” anasema.


TABIA ZA TSHABALALA

“Tangia akiwa mdogo ni mkimya, msikivu, havuti sigara wala kunywa pombe ni vitu ambavyo nilimsimamia kwa nguvu zangu zote, kwani nilijua vinaweza vikamtoa katika mstari wa kazi anayofanya,” anasema Baba Tshabalala na kuongeza;

“Jambo lingine ninalomsimamia hadi sasa ni kufanya maendeleo yake, mfano, nikimwambia umepata pesa wekeza kitu fulani kitakusaidia baadaye, anafanya kwa nguvu zake zote ili asiniangushe siyo mbishi.”


KAMRITHI MJOMBA

Anasema familia yake sio ya soka na wakati Tshabalala akiwa mdogo alikuwa hapendi acheze, lakini kipaji hicho anaona amekirithi kutoka kwa mjomba wake, beki wa kati wa zamani wa Yanga, Said Zimbwe Mwaibambe (sasa marehemu ).

“Huyo ni kaka yake mkubwa na mama yake Tshabalala, ndiye alikuwa mchezaji beki namba tano, ingawa Tshabalala anacheza beki ya kushoto, binafsi nikaja nikamuunga mkono acheze soka baada ya marafiki zangu kuona kipaji na kunisisitiza nisimkataze,” anasema.

TSHABAL 06

ANAUZA SAMAKI

Licha ya jina la Tshabalala kuwa kubwa, hajaacha kufanya kazi yake ya kuuza samaki katika soko la Manzese Midizini, ndiko yalikofanyika mahojiano na Mwanaspoti akiwa katika shughuli zake.

“Kufanya shughuli zangu hakumanishi Tshabalala hanipi pesa, nimeanza kuuza samaki kwa muda mrefu, maisha yana kupanda na kushuka, hivyo ziwezi kumtwisha mzigo mzito kijana wangu, hilo soko siwezi kulala na njaa naondoka na chakula cha ndani bila hata kulipia pesa,” anasema Baba Tshabalala na kuongeza

“Mwanzoni Tshabalala alikuwa anakuja kutembela katika soko hilo, alikuwa anapewa zawadi mbalimbali na marafiki zangu na mashabiki wake, lakini kwa sasa haji kutokana na ratiba zake kumbana.”